ARUSHA,KIWANDA CHA RAHA BEVERAGE (BANANA)CHAFUNGWA ,CHANZO NI KUPANDA KWA BEI YA SUKARI, WAFANYAKAZI 200 WAANGUA KILIO KUKOSA AJIRA

Na Joseph Ngilisho ARUSHA 

Kiwanda cha kutengeneza mvinyo na pombe kali cha Raha Beverage Co. Ltd maarufu Banana kilichopo Olorien jijini Arusha kimetangaza kusitisha shughuli za uzalishaji kwa kile kinachodaiwa ni changamoto ya uhaba wa sukari inayopanda kiholela.

Kufungwa kwa kiwanda hicho maarufu jijini hapa, kunaenda sanjari na kusitisha mikataba ya wafanyakazi zaidi ya 200 waliokuwa na ajira ya kudumu na yamuda, uongozi umedai upo katika mchakato wa kutafuta fedha ili kuwalipa mafao yao .

Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho Adolf Olomi amesema tayari  wafanyakazi hao wamejulishwa juu ya mpango huo na kuwataka waanze kujiandaa kisaikolojia.
Mkurugenzi kampuni ya RaHa Beverage Adolf Olomi

Akiongea ofisini kwake mapema leo Olomi amesema wamelazimika kukifunga kiwanda hicho ifikapo februali 1 mwaka huu,kwa kile alichodai ni upatikanaji haba wa sukari inayouzwa kwa bei ya juu jambo alilodai wameshindwa kumudu gharama za uendeshaji .

"Ni kweli tunakusudia kusimamisha uzalishaji kwa muda tukiwa na sababu mbili , moja ni kupanda kwa gharama ya sukari ambayo ndio malighafi kuu ya kiwanda chetu , oktoba mwaka jana tulinunua mfuko kwa sh,120,000 na sasa imepanda hadi sh, 155,000 na tena  haipatikani ndio maana tumeona haina haja ya kuendelea na uzalishaji kwa sababu haitulipi"

Aidha Olomi alikanusha taarifa kwamba kiwanda hicho kimefungw kutokana na kuelemewa na madeni ila alikiri kudaiwa na taasisi mbalimbali  za fedha na kuwataka wafanyakazi watulie wakati mchakato wa kuwalipa madai yao ukifanyika.


Hata hivyo alisisitiza kwamba kiwanda jicho hakijafungwa moja kwa moja ila wamesimamisha uzalishaji kwa muda ili kupisha hali ya sukari hapa nchini kutengemaa na wanatarajia   ifikapo juni mwaka huu kitafungiliwa .

"Wakati kiwanda chetu tukiwa tumesimamisha uzalishaji hatutaweza kuwalipa wafanyakazi kwa sababu hatutakuwa na uzalishaji  tutakachokifanya ni kuandaa mafao na tumeanza mazungumzo na mifuko ya hifadhi ya jamii na idara za wafanyakazi"

"Tutakapoanza  uzalishaji moja ya changamoto ya kampuni hii ni gharama za uendeshaji zinazotokana na uwepo wa vituo vingi vya mauzo ambavyo havifanyi vizuri hivyo tumekusudia kuvifunga baadhi ya vituo hivyo katika mikoa ya Tanga,Dar es salaam na Morogoro tutavifunga ili kupunguza gharama za uendeshaji"

Olomi alisema suala la kufunga kiwanda hicho sio jambo geni kwani mwaka 2019 waliwahi kukifunga kwa muda wa miezi mitatu ili kutatua  changamoto mbalimbali  za uendeshaji.

Kufungwa kwa kiwanda hicho kikongwe jijini Arusha,kumezua sintofahamu kwa wafanyakazi ambao walionesha kuangua kilio na kububujikwa machozi wasijue hatima yao wakati uongozi wa kiwanda hicho ukitoa taarifa juu ya kusudio la kusimamisha shughuli za uzalishaji ifikapo februali mosi mwaka huu.


Ends...










Post a Comment

0 Comments