Na Joseph Ngilisho ARUSHA
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof.Jamal Katundu kuhakikisha anawachukulia hatua stahiki watendaji wa wizara hiyo wanaofanya kazi kwa mazoea na kuacha kuwaonea haya.
Waziri Aweso alitoa agizo hilo jana wakati alipokuwa kwenye mkutano wa kuwashukuru wadau wa sekta ya maji nchini, kwa mchango wao mkubwa wa hali na mali katika kuwezesha mafanikio yaliyopatikana, sambamba na kutoa fursa ya maoni ya mapendekezo ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 yoleo la mwaka 2023 na mpango mkakati wa wizara.
Alisema licha ya mafanikio mengi yaliyofikiwa, lakini bado kuna baadhi ya watendaji baadhi ya maeneo lazima wakubali kubadilika na kusimama kama kiongozi kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Alitoa mfano wa baadhi ya maeneo mkoani Mbeya vijijini, baadhi ya watendaji wamepelekewa fedha zaidi ya Sh.milioni 300 ya mradi wa maji na kuamua kugawana, huku mradi ukitelekezwa.
"Katibu Mkuu chukulia hatua wote wanaokwamisha miradi yetu au wanaofanya kazi kwa mazoea usionee mtu haya na ukicheka na nyenyere atakung'ata kwenye makwapa, ni lazima watendaji msimame katika nafasi zenu za kazi na mtoe taarifa kwa wakati sehemu sahihi,"alisema.
Alisema zipo kazi nzuri zinafanyika kwenye usimamizi wa miradi na kusababisha mwenge wa Uhuru mwaka huu ulikagua miradi zaidi ya 170 hakuna hata mradi mmoja uliokwama jambo ambalo zuri la kujivunia.
Aidha alisema siku za nyuma kulikua na miradi 177 kichefuchefu ambayo ilimladhimu kuweka nguvu za pamoja na wadau wa sekta ili kuhakikisha inamalizwa kabla ya kuanza miradi mipya.
"Miradi hii tuliitia ndimu ili kichefuchefu kiishe maana tusingeweza kwenda katika miradi mipya wakati kuna miradi lukuki ya kichefuchefu,"alisema
Aidha alisema wizara ya maji ishirikishe kwa kiwango kikubwa sekta binafsi katika kufanya mageuzi ya sekta ya maji nchini na hususani kuyafanyia kazi maoni yao ya mapendekezo ya rasinu ya sera ya Taifa ya maji na mpango mkakati wa wizara.
"Nilazima wizara yetu tukubali kubadilika ili kuruhusu kupata mawazo ya watu binafsi.Zipo baadhi ya hoteli kubwa hazina mita na wanatumia maji na vipo baadhi ya viwanda vikubwa vinatumia maji hawana mita za maji.
"Ninawaomba watendaji hili eneo linahitaji uzalendo,ushirikishwaji na lazima tushirikishe wadau wetu wa maendelo ili tufanye mageuzi makubwa katika sekta yetu ya maji,"alisema.
Aweso aliwataka wataalamu kuheshimisha taaluma zao, kwenyebutekelezaji wa maji ili kuepusha gharama kubwa kutumika katika miradi bila sababu
"Haiwesekani eneo moja miradi ikatekelezwa kwa fharama tofauti na kubwa hili halipo sawa lazima tukubali kubadilika na kutenguliza uzalendo, sababu maendeleo ya sekta ya maji yanaanza na kila mmoja,"alisema.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji,Prof.Jamal Katundu,alisema kupitia kikao hicho cha siku mbili,wadau hao watajadiliana masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo muhimu ya maji ikiwemo fursa na changamoto, pamoja na rasimu ya sera mpya ya maji.
Amesema maoni na mapendekezo ya wadau wa Sekta ya Maji ni muhimu sana katika kuandaa Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002,toleo la 2023 katika kutekeleza dhana ya ushikishwaji.
Mkutano wa wadau wa sekta ya maji, pamoja na wengine, umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Taifa, Wenyeviti wa Bodi za Mabonde ya maji na wa Mamlaka za maji, RUWASA,Uongozi wa Chuo cha Maji, viongozi wa chama na serikali mkoa wa Arusha,Menejimenti ya Wizara ya Maji na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za maji wa Mikoa na Wilaya.
0 Comments