Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Wananchi wa kijiji cha Moita Bwawani wilaya ya Monduli Mkoani Arusha,wameiomba serikali kuingilia kati mgogoro wao wa Ardhi wakimtuhumu mwenyekiti wao Bruno Joseph kuuza maeneo yao ya malisho na kubadilisha kuwa maeneo ya makazi kinyume na utaratibu.
Hatua hiyo imeibua mgogoro mkubwa na vitendo vya uvunjifu wa amani kiasi cha wananchi hao kupigana na wengine kujeruhiwa huku askari polisi kata aliyetambuliwa kwa jina la Mathew akishushiwa kipigo Kikali wakati alipofika kijijini hapo kwa lengo la kufuatilia sakata hilo.
Wakiongea kwa jazba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo,wananchi hao ambao wameungana na wenzao wa vijiji jirani ,wamedai kushangazwa na jeuri ya mwenyekiti wao kumega maeneo ya malisho na kuyauza huku akitanguliza maslahi binafsi wakati mkuu wa wilaya hiyo Joshua Nasary aliwahi kuzuia uuzwaji wa maeneo ya malisho kijijini hapo.
Baadhi ya wananchi hao ,Lali Moikani na Eliya Kisiri walisema na kuiomba serikali kusitisha zoezi hilo kwa Mwenyekiti wao ambaye amekuwa hajali matakwa ya wengi hususani wananchi wenye mifugo, kwani eneo hilo zaidi ya hekari 3000 lilitengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo na sio vinginevyo.
"Mwaka 2023 mwenyekiti huyo alianzisha kitu kinachoitwa jembe la busara kwa lengo la kumega ardhi na amekuwa akichukua fedha za watu akiwaahidi kuwapatia ardhi ya wananchi kinyime na maelekezo ya mkuu wa wilaya "alisema Moikani
Naye Kisiri alisisitiza kuwa serikali ya kijiji cha Moita chini ya uongozi wa mwenyekiti huyo inamega maeneo ya malisho kwa kisingizio cha kuyaendeleza na badala yake amekuwa akiyauza kwa wananchi wakazi na wageni na hivyo kuibua mgogoro usio koma unaoashiria uvunjifu wa amani.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ndoipo Mollel maarufu kwa jina la Ndoipo Maskini Mollel alisema kitendo kilichofanywa na Mwenyekiti kutoa eneo hilo kwa ajili ya maendeleo ya makazi kinapaswa kulaaniwa kwa kuwa alijali maslahi yake na sio maslahi ya wafugaji.
"Tumekutana hapa kwa lengo la kuzuia uuzwaji wa maeneo ya malisho kunakofanywa na mwenyekiti wa kijiji, tangia ameingia madarakani amekuwa akitapeli fedha wananchi na kugawa maeneo ya malisho"
Mollel alisema ardhi ni mali ya watanzania wote na sio ya baadhi ya watu hivyo wao wanaungana na wananchi wa vijiji vingine kupinga kumegwa kwa ardhi hiyo ili eneo hilo liendelee kuwa eneo la malisho na sio vinginevyo.
Naye Mwanakijiji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ndekui Laizer yeye alisema kuwa utaratibu anaotumia Mwenyekiti Mollel wa kumega ardhi ya malisho akidai ni kwa ajili ya makazi sio sahihi kwani hakujali na kuzingatia maslahi ya wafugaji juu ya kutengwa eneo hilo kwa ajili ya malisho.
Alisema Mwenyekiti ameweka mbele tamaa zake na masilahi yake binafsi bila kuzingatia jamii anayoiongoza inayojali eneo la malisho kuliko makazi hivyo maazimio yote yaliyopitishwa yanapaswa kusitishwa na kubadilishwa kwa maslahi ya wananchi wa vijiji vyote vya Arumeru na Monduli. na Paulo Mwikani walimtaka mkuu wa wilaya hiyo kufika katika kijiji hicho kwa lengo la kutatua mgogoro huo ili kuepusha uvunjifu wa amani unaoonesha viashiria.
Katika hatua nyingine wananchi hao wamelalamikia hatua Jeshi la polisi wilayani humo kufumbia macho vitendo vya vurugu zinazoendelea kijijini hapo kwa kumekuwa na matukio kadhaa ya wananchi kupigwa akiwemo askari polisi kata ambaye pia alishambuliwa vibaya wakati akifuatilia vurugu hizo.Wananchi hao walimtaka mkuu wa wilaya ya Monduli Joshua Nasari kuingilia kati ili kunusulu uvunjifu wa amani unaonukia.
Akijibu shutuma hizo Mwenyekiti wa kijiji hicho,Bruno Joseph Mollel alisema kuwa mgogoro huo unasababishwa na baadhi ya wanasiasa na kumtuhumu mmoja ya wafanyabiashara na mfugaji mkubwa wa mifugo Sanare Mollel kuchochea mgogoro huo .
Mwenyekiti wa Kijiji cha Moita Bruno JosephAlisisitiza kuwa tangu ameingia madarakani amekuwa na utaratibu wa kupima maeneo kwa lengo la kuyaendeleza ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu.
.
Alisema amekuwa akifanya hivyo kuondoa migogoro ya ardhi na wananchi wake ila mgogoro huo kwa sasa unachochewa na baadhi ya wanasiasa na wafugaji wakubwa wenye mifugo mingi eneo hilo.
"Mh Mkuu wa wilaya tunatamani aje aseme anavyotaka kusema ila akienda kinyume na sisi hatutakubaliana naye"alisema Mwenyekiti huyo
Akijibu shutuma hizo mfanyabiashara Sanare Mollel alisema shutuma zinazoelekezwa kwake na mwenyekiti wake ni hoja dhaifu zisizo na mashiko na kusema kuwa wananchi wenyewe wameamua kutetea ardhi yao kwa ajili ya kulinda vizazi vyao na malisho .
Mollel alisema watanzania wa sasa hususani wafugaji wa jamii ya kimasai wamekuwa welevu na wenye kujitambua na kujua thamani ya eneo la malisho hivyo kumega kwa ajili ya makazi sio hoja yenye mashiko kwani taratibu zote hazikufuatwa hivyo aliiomba serikali kuhakikisha hilo linasitishwa kw amaslahi ya wananchi wa Moita na vijiji vya jirani.
Mfanyabiashara huyo aliwataka viongozi wa Kjiji cha Moita kujibu hoja za wananchi na sio kumsingizia yeye eti naleta chokochoko na vurugu kwani wananchi wa jamii ya kifugaji wanajali eneo la malisho kuliko makazi.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli aliyetambuliwa kwa Anaeli Mbise aliwaeleza wananchi hao kuwa suala lao liko mikononi mwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli,Joshua Nassari na kuwataka wananchi hao kuwa watulivu wakati mkuu wa wilaya hiyo akitarajiwa kufika kijijini hapo mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.
Ends .
0 Comments