TAZAMA WAUMINI WALIVYOLOWA WAKIMWAGA MAOMBI KULAANI VIBAKA WAOTIKISA DARAJA MBILI ARUSHA,WANANCHI WAISHIWA PUMZI, WADAI VIONGOZI WAO WAMELALA USINGIZI WA PONO, WATAKA RPC AHAMISHIE MAKAZI YAKE HUKO

Na Joseph Ngilisho ARUSHA 

Waumini wa makanisa katika mtaa wa Sanare kata ya Daraja mbili Jijini Arusha, wameungana na kufanya maombi ya pamoja kulaani vibaka wanaosumbua mtaani hapo kutokana na matukio nbalimbali ya uhalifu ikiwemo kubaka mchana kweupe huku viongozi wa mtaa huo wakiwa kimya kufumbia macho.


Waumini hao wakiongozwa na mwinjilisti Evance Minja wa kanisa la KKKT usharika wa Ungalimited,jijini hapa,walidai hawaoni haja ya kuwa na viongozi wakati wameshindwa kutatua kero dhidi ya vibaka, wanaosumbua mtaani hapo kwa matukio ya wizi,matusi,ulevi, kubaka na ulawiti, uvutaji wa dawa za kulevya na uuzaji wa  bangi na mirungi hadharani.
Akitoa mahubili katika maombi hayo mwinjilisti Minja aliiomba serikali ya mtaa huo itoe tamko iwapo imeshindwa kukomesha uhalifu mtaani hapo ,ili waweze kuingilia kati kwani wanaamini mungu hashindwi kwa lolote katika vita hiyo.
Mwinjilisti Minja 
"Katika maombi haya tumewaalika viongozi mbalimbali akiwemo Diwani Prosper Msofe,Mwenyekiti wa mtaa,Afisa Mtendaji wa kata, polisi kata na wengine lakini hakuna hata mmoja aliyefika kuwa na sisi hii inaonesha wazi kwamba hawapo na sisi"

Baadhi ya waumini hao Rehema Mbeswa kutoka kanisa la KKKT usharika wa Ungalimited na Margaret Philipo  wa kanisa Katoliki la Moyo safi Ungalimited, walisema wameamua kufanya  maombi hayo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na uhalifu kwa njia za kiroho baada ya kuona vitihada za viongozi wa serikali ya mtaa kudhibiti vibaka hao  zimeshindikana huku wananchi wakizidi kuteswa na makundi hayo ya uhalifu yanayosumbua mtaani hapo usiku na mchana bila kuchukuliwa hatua.

"Lengo kuu la kukutana hapa ni kwa ajili ya kumlilia mungu kutokana na matukio ya uhalifu yanayofanywa na magenge ya uhalifu yanayotishia maisha yetu ili mungu akatende muujiza wa kuwabadilisha vijana hao na mtaa wetu na mitaa ya jirani waondokane na uhalifu"

Naye kiongozi wa jumuiya wa kanisa katoliki Ungalimited ,  Salvador Makoi alisema mtaa huo wa Sanare umekuwa kitovu cha uhalifu kutokana na makundi ya uhalifu kutoka mitaa mbalimbali kufanya mtaaa huo kama kambi yao ya uhalifu.

Aliishauri serikali ya mtaa huo kufanya jitihada za ziada katika kukabili makundi hayo ya uhalifu ikiwemo kuishirikisha serikali ya wilaya na mkoa ili wananchi waweze kuishi kwa amani kwani kwa sasa wamekuwa hawalali au kupata usingizi  kutokana uhalifu unaoendelea mtaani hapo. Alimwomba kamanda wa polisi Mkoa Kuhamishia makazi yake katika mtaa huo ili kusaidiana kupambana na vibaka hao.

Naye mjumbe wa serikali ya mtaa huo,Aaron Samweli aliwatoa hofu waumini hao kwa kuwataka wawe watulivu kwani serikali haijashindwa na tayari jitihada zimefanyika za kuwakabili vibaka hao na kuwataka wananchi kutokuwa waoga kutoa ushirikiano ikiwemo kuwataja wahusika na kutoa ushahidi pale wanapohitajika mahakamani.

"Kuna kikao tulikaa na RPC na kila mtaa tumekabidhiwa askari polisi lakini tatizo la huu mtaa wananchi hawatoi ushirikiano wa kuwataja wahalifu"

Alisema jitihada zimefanyika ikiwemo kuchukua majina ya vijana wanaosumbua kwa uhalifu ambao  wanatukana watu wazima matusi ya nguoni  akidai yanafanyiwa kazi na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano bila woga kuwafichua wahalifu .






Ends...








.

Post a Comment

0 Comments