Na Joseph Ngilisho Arusha
HALMASHAURI ya jiji la Arusha imetishia kuwaondoa kwa mabavu wafanyabiashara wa maduka wasiotaka kuingia mkataba mpya wa upangaji kupitia mfumo mpya wa kukusanya mapato ya serikali wa TAUSI .
Akiongea na waandishi wa Habari baada ya kutembelea maduka ya wafanyabiashara katika eneo la standi ndogo,Mkurugenzi wa jiji hilo,Mhandisi Juma Hamsini alisema halmashauri hiyo imejipanga kupiga mnada maduka yake ambayo wapangaji wake hawatakuwa tayari kujaza mkataba mpya na kujisajili kupitia mfumo huo wa Tausi.
Alisema jiji la Arusha limepandisha kodi kwenye maduka yake tangu Julai mwaka huu kutoka sh,200,000 hadi 250,000 lakini baadhi ya wafanyabiashara wanaojiita wajenzi wanaendesha kampeni ya kugomea ongezeko hilo la kodi ikiwemo kukataa kujisajili katika mfumo Tausi kwa madai kwamba wao ni wajenzi.
"Tumegundua kuna baadhi ya wafanyabiashara wamepangishwa kwenye maduka yetu na watu wanaojiita wajenzi kwa sh 500,000 wakati halmashauri inalipwa 200,000 na wengine wanatumia leseni moja kiendesha maduka mawili na wengine hawana leseni kabisa"
Alisema wataalamu wa jiji wamejipanga kwa kuweka kambi katika eneo la maduka ili kuwasajiri wafanyabiashara kupitia mfumo wa TAUSI na wale wasiotaka kujisajiri na kulipa kodi mpya maduka yao yatapigwa mnada ili kuwapa watu wengine ambao wapo tayari kuingia mkataba na jiji hilo.
Hata hivyo mhandisi Hamsini alishindwa kujizuia baada ya kuamua kuwachapa noti kama sehemu ya kuhamasisha na kuwashukuru wafanyabiashara waliokutwa na leseni hai,waliojaza fomu za mkataba mpya na wale waliojisajili kupitia mfumo mpya wa serikali wa TAUSI.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo alidai kwamba jiji hilo limetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kujenga uwekezaji wa maduka katika eneo la Themi ili baadhi ya wafanyabiashara waende huko .
Aidha alisema halmashauri hiyo ipo katika hatua ya kuwalipa fidia ndugu wa marehemu ili kuhamisha makaburi yaliyopo katikati ya jiji na eneo hilo kutumika kwa ajili ya miradi ya biashara.
Naye naibu meya wa jiji la Arusha Abrahamu Mollel alisema kumekuwepo na wimbi la madalali wanaowapangisha wafanyabiashara kwenye maduka ya halmashauri kwa bei ya juu huku halmashauri ililipwa kiasi kidogo cha sh, 200,000 kuwa hali hiyo haikubaliki na kutoa onyo kali kwa madalali hao kuwachukua hatua.
Ends........
0 Comments