Na Joseph Ngilisho,Moshi
Mahakama Kuu Kanda ya Moshi,Mkoani Kilimanjaro,imeliamuru baraza la Ardhi wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro,kurejea upya mgogoro wa Ardhi wa familia maarufu ya chifu Marealle kwa kutembelea eneo linalobishaniwa na wanandugu hao na kurekodi upya mipaka na kisha kutoa maamuzi chini ya mwenyekiti mwingine wa baraza hilo
Akisoma hukumu hiyo leo Jaji wa mahakama kuu,Lilian Mongella katika kesi namba 51/2023 ya mrufani Frank Mareale dhidi ya Ackley Mareale ambao wote ni wanandugu, Jaji Mongella alisema mahakama imepitia ushahidi na maamuzi ya Baraza la Nyumba na Makazi la Mji wa Moshi chini ya Uenyekiti wa Reginald Mtei yaliyotolewa mei 5 mwaka huu na kusema kuwa maamuzi hayo yalikuwa na kasoro za kisheria.
Jaji Mongella alisema kuwa moja ya mapungufu katika maamuzi ya Baraza ni pamoja na baraza hilo kushindwa kuonyesha au kurekodi mipaka ya ardhi ya ekari mbili inayogombaniwa na wanafamilia hao hivyo ametengua maamuzi hayo na kuamuru kesi hiyo isikilizwe upya chini ya Mwenyekiti Mwingine.
Mlalamikaji Frank Mareale kushoto akiwa na wakili wake
Wakili Julias Semali
Alisema katika mapitio ya maelezo ya mashahidi wa kesi hiyo katika Baraza la Ardhi Nyumba na Makazi hakuona kama Baraza hilo limeonesha mipaka ya eneo la mgogoro na kusema kuwa kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
"Nimeamua kesi hii ya wanafamilia wa Mareale isikilizwe upya kwa sababu Baraza la Ardhi lilikosea kisheria kwa kushindwa kuonyesha mipaka ya ekari mbili inayogombaniwa"
Katika kesi ya awali iliyofunguliwa na Frank Mareale katika Baraza la Ardhi Nyumba na Makazi katika Mji wa Moshi, alikuwa na madai matatu moja wapo ni ombi la Baraza hilo litamke kuwa eneo la ekari mbili yeye ni mmiliki halali, Pili Baraza litoe amri ya kufukuliwa kwa mwili wa mama yake mdogo marehemu Veronica Mareale aliyeishi katika eneo hilo miaka 80 na kufariki mwaka 2020 na pia alitaka alipwe gharama za kesi.
Mei 5 mwaka huu chini ya mwenyekiti wa Baraza hilo la Ardhi Nyumba na Makazi ,Reginald Mtei lilitupilia mbali madai hayo ya Frank Mareale na kusema kuwa Ackley Mareale ni mmiliki halali wa eneo hilo na sio vinginevyo.
Akizungumza nje ya Mahakama,Wakili wa Ackley Mareale,Julius Semali alisema kuwa hana pingamizi na uamuzi wa Mahakama kwani ana uhakika kuwa mteja wake ni mmiliki halali wa eneo hilo kwa kuwa mama yake alipata kihalali na alizikwa katika eneo lake.
Wakili alisema hana shaka na uamuzi wa awali wa Baraza hilo na kusema kuwa usikilizwaji mwingine utathibitisha kuwa haki ya mtu huwa haipotea ila inacheleweshwa tu.
Naye Wakili wa frank Mareale,Modest Njau aliishukuru Mahakama Kuu kwa uamuzi wake wa kuiagiza Baraza la Ardhi Nyumba na MakaziMoshi kusikiliza upya kesi hiyo na aliamuru Mwenyekiti wa Baraza na wajumbe wake wabadilishwe.
Njau alidai Mahakama Kuu iliona jinsi haki ilivyokuwa ikitaka kuchezewa katika usikilizwaji wa awali nayeye na mteja wake wameridhika na maamuzi hayo.
Ends....
0 Comments