Na Joseph Ngilisho ,Arusha
Jopo la Mawakili wanne wakiongozwa na Wakili Mkongwe,Mpaya Kamala jana waliwasilisha sababu saba mbele ya Jaji Angaza Mwipopo wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na kumwomba Jaji kumwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha,Dkt John Pima na wenzake wawili kwa madai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilikosea kisheria katika mwenendo mzima wa kesi hiyo.
Agosti 31 mwaka huu Piama na wenzake wawili aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji Miriamu Mshana na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango,Takwimu na Ufuatiliaji Innocent Maduhu walihukkumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na shitaka la uhujumu Uchumi.
Katika rufaa hiyo wakata rufaa walikuwa wakiongozwa na wakili Mpaya na wenzake ,Mosses Mahuna,Sabato Ngogo na Fridorin Bwemelo walitoa sababu hizo mbele ya Jaji Mwipopo anayesikiliza rufaa hiyo katika Mahakama Kuu kanda ya Arusha.
Kwa upande wa wajibu rufaa Jopo la Mawakili wa Jamhuri lilikuwa likiongozwa na Patrick Mwita akisaidiwa na Erasto Anosyisye,Timotheo Mmari na Hemed Khalid .
Wakili Mahuna alidai Pima ni Mteule wa Rais kwani aliteuliwa mara mbili kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha mara ya kwanza aliteuliwa na Rais marehemu Dkt John Magufuli na mara ya pili aliteuliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hivyo hati ya mashitaka iliyomtia hatiani ilikuwa na kasoto kwani mteule huyo wa Rais hati yake ya mashitaka ilipaswa kupata kibali na baraka na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Nchini}DPP}.
Mahuna aliendelea kudai kuwa mbali ya hilo hati ya mashitaka ilikuwa na kasoro nyingi na kufanyiwa marekebisho mara kwa mara lakini hati ya mashitaka ya mwisho ya februali 27 mwaka huu iliyomtia hatiani Pima haikuwa mahakamani.
Alidai na kumwambia Jaji Mwipopo kuwa kesi iliyosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ilikuwa na kasoro nyingi na ukiukwaji mkubwa wa sheria hivyo alimwomba Jaji kuwaachia huru Pima na wenzake kwa kuwa kesi hiyo haikuzingatia misingi na miongozo ya kisheria.
Hakimu Seraphin Nsana wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha alifunga Pima na wenzake wawili katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 5/2022 kwa maelezo kuwa watuhumiwa hao walikutwa na hatia katika muenendo mzima wa kesi hiyo.
"Kwa kuzingatia maombi ya mawakili wa upande wa washtakiwa, ikiwemo kutokuwa na rekodi ya makosa ya nyuma, utegemezi wa familia na ushirikiano mlioutoa katika kipindi chote cha uendeshaji wa kesi hii, mahakama inawapa adhabu ya kutumikia miaka 20 jela huku miezi 14 mliokuwa kizuizini ukizingatiwa" alisema Hakimu Nsana
Mwisho....
0 Comments