WAZIRI MKUU MAJALIWA ATUA ARUSHA,ATOA MAAGIZO MAZITO WIZARA YA FEDHA

Na Joseph Ngilisho,Arusha

Waziri Mkuu,Kassimu Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa {TAMISEMI} kuwa ifikapo januari 15 mwakani kuhakikisha halmashauri zote kote nchini zinarudia utaratibu wa kukopesha asilimia 10 kwa vikundi vya vijana,akina mama na walemavu kutumia huduma za kifedha.


Majaliwa alisema hayo jana Jijini Arusha wakati akizindua wiki ya Maadhimisho ya Huduma za Kifedha Kitaifa na kusema kuwa utaratibu wa zamani ulisitishwa  wa utoaji mikopo kwa vikundi kwa kuwa baadhi ya taratibu zilikiukwa na Serikali iliagiza kuwepo utaratibu mzuri wa utowaji mikopo kupitia huduma za kifedha.


Alisema toka ilipotangazwa kusitishwa na serikali ana uhakika umewekwa utaratibu mzuri wa vikundi kunufaika na fedha hizo na sasa hivyo basi ifikapo januari 15 mwakani shughuli za ukopeshaji vikundi uwe umeanza.


Waziri Mkuu alisema Serikali ilikuwa inatoa fedha nyingi katika vikundi hivyo lakini kuna baadhi ya watumishi ambao sio wema walikuwa wakitumia mwanya wa utaratibu mbovu kujinufaisha hivyo mianya hiyo itakuwa imefungwa na vikundi vya jamii hiyo vitakuwa vikinufaika ifikapo mwakani.


Akizungumzia wiki ya Maadhimisho hayo aliitaka Wizara ya Fedha kuhakikisha elimu inatolewa hasa maeneo ya Vijijini kwa njia za Sinema,matangazo kwa njia ya mitandaoni,vyombo vya habari vya kidigital,redio na televisheni.


Hata hivyo ,Majaliwa alisema asilimia 53.8 ya watumia huduma ya fedha iliyopo sasa bado haitoshi kwani kuna uwezekano mkubwa elimu ya huduma hiyo haijawafikia wananchi wa Vijijini hivyo kuna wajibu wa Wizara ya Fedha kujikita huko ili kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.


Waziri Mkuu aliikumbusha Wizara hiyo kuhakikisha inazingatia na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa Taifa kwa ajili ya kuinuwa uchumi wan chi.


Vilevile alizitaka taasisi zote za fedha zitambulishe mahali zilipo ili wajasirimali wadogo na wakati ili waweze kukopesheka kwa lengo la kukuza mitaji yao na kujikwamua kiuchumi.


Naye Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba,alisema alifurahishwa na maandalizi ya maadhimisho hayo kwa kuwa yanatoa fursa kwa wadau wa taasisi za kifedha kutoa elimu kwa wananchi kutumia huduma za kifedha.


‘’Kutokana na maadhimisho haya Watanzania watanufaika na elimu hii kwa kuwa watapata elimu ambayo iatawasaidia kuongeza kipato na kukuwa kiuchumi’’alisema Mwigulu.


Waziri huyo ,alisema jamii ikiwa na uelewa sahihi wa elimu ya huduma za kifedha itawasaidia wananchi kutokukopa mikopo umiza na kuingia mikataba ambayo itawabana pasipo kutambua kwani wengi wao hawasomi mikataba hiyo bali wanakimbilia kutia saini na kuchukua fedha bila kusoma na kuielewa.


‘’Watanzania wengi hatuna nidhamu ya mikopo na tunakopa kwa malengo yaliyokusudiwa lakini tukichukua fedha tunaishia kuzipeleka katika matumizi yasiyokuwa rasmi na baadae kujijutia wakati wa urejeshaji wa mikopo hiyo’’alisema


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,Natu Mwamba alisema kuwa Maadhimisho hayo ya tatu Kifaifa yamelenga kutoa elimu zaidi kwa watanzania kujikwamua kiuchumi kswa kutumia huduma za kifedha.


Pia alisema maadhimisho hayo yameandaliwa Wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wa huduma za kifedha na imeshirikisha jumla ya benki 35 na kampuni za simuhapa nchini.


Mwisho     


Post a Comment

0 Comments