WAZIRI BITEKO HATAKI UTANI AAGIZA TANESCO KUKATA UMEME TAASISI ZA SERIKALI NA WAWEKEZAJI WANAOONGOZA KWA MADENI SUGU YA UMEME, ARUSHA PEKEE INADAIWA BILIONI 7.7 ,

Na Joseph Ngilisho,Arusha

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwakatia umeme wadaiwa sugu yakiwemo mashirika ya umma ,taasisi za serikali, wawekezaji wa viwanda na watu binafsi ,ambapo kwa mkoa wa Arusha Tanesco inadai zaidi ya sh,Bilioni 7.7 za malimbikizo ya ankara za bili za umeme.

Dkt Biteko ameyasema hayo wilayani Arumeru mkoani Arusha, wakati alipotembelea na kujionea mradi wa kituo cha  umeme cha Lemuguru , ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 98, na ni sehemu ya mradi  wa ujenzi  wa njia  kuu ya umeme  ya msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea Kenya (KTPIP).

“Hapa Arusha , TANESCO inadai wateja wake shilingi bilioni 7.7, na mara nyingi wanaodaiwa si wananchi wadogowadogo bali Taasisi za Serikali na Wawekezaji wanaojiita wawekezaji wakubwa ambao ukiwakatia umeme wanakwambia unaua ajira,  wepesi wa kujificha kwenye kisingizio cha kulipa kodi na ajira; TANESCO anahitahi fedha ili awekeze na kisha awapelekee umeme wananchi, TANESCO nawaambia kateni umeme kwa mtu yeyote mnayemdai ili mradi unamdai kwa haki.” Alisema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko pia ameagiza wadaiwa wote wa madeni ya bili za umeme wakalipe madeni hayo ili zipatikane fedha za kuwahudumia wananchi na ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za umeme nchini kwa aina mbalimbali ikiwemo kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme ukiwepo wa Julius Nyerere (MW 2115), ambao umefikia asilimia 94 ambapo amesema kuwa, Mkandarasi ameshafunga mashine mbili tayari kwa kuanza majaribio ya kuzalisha umeme.





Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amekemea vikali watu wote wanaohujumu miundombinu ya umeme akitolea mfano wizi wa shaba na mafuta ambapo kati ya tarehe 25 Novemba, 2023 na 26 Novemba, 2024 kuna matukio 14 katika Ukanda wa Pwani ya kuharibu au kuhujumu miundombinu ya umeme, ambapo ameeleza kuwa, Serikali itawashughulikia kwa kuendesha msako na watakapopatikana sheria itachukua mkondo wake.

Aidha, ameitaka TANESCO kuwasikiliza na kuwapatia majibu kwa haraka wananchi wanaopiga simu kwenye Shirika hilo ili kupata huduma za umeme na mahali penye matatizo waambiwe, “huu utaratibu wa watu kupiga simu anaambiwa subiri, hii tumekubaliana kuwa haiwezekani ikaendelea na ndio maana nimewaambia kituo cha Huduma kwa Mteja tukiimarishe kutoka miito 65 na ziongezwe kufika 100 na zaidi.” 

Kuhusu utekelezaji wa kituo hicho cha umeme cha Lemuguru kilichopo wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, Dkt. Biteko alisema kuwa mradi huo ni mkubwa na unagharimu Dola za Marekani milioni 258.8 na kina faida mbalimbali ikiwemo kupelekea wananchi umeme usiokatika mara kwa mara na kituo kitaimarisha hali ya umeme mkoani Kilimanjaro na Arusha.

Dkt. Biteko vilevile ameipongeza TANESCO kwa hatua mbalimbali inazochukua ili kupunguza makali ya mgawo wa umeme pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuongeza kiwango cha Gesi Asilia kinachozalisha umeme.

Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa njia Kuu ya kusafirisha umeme wenye msongo wa Kilovoti 400 kutoka Singida hadi Namanga kuelekea Kenya, Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Peter Kigadye, alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda mikoani na migodi ya uchimbaji madini na hivyo kuwezesha kufikia uwezo wa juu wa megawati 2000 katika kusafirisha umeme.

Alisema, utekelezaji wa mradi unahusisha vipengele Sita  ikiwemo ujenzi wa njia 8 za laini ya kV 400/33 kutoka Kituo kipya cha kupoza umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Arusha yenye urefu wa kilomita 414.3, Babati -Arusha kilomita 150, Arusha –Namanga, Kilomita 114.3 ambao umefikia asilimia 96.

Alisema mradi huo pia unahusisha, upanuzi wa vituo vya kupoza umeme ambao umefikia asilimia 98.72, mradi wa usambazaji umeme kwa vijiji vilivyopitiwa na mradi vijiji na ujenzi wa vituo vyq kupoza umeme vya Dodoma, Singida, ambavyo vimekamilika.


Naye mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela alisema vijiji 351 vya mkoa wa Arusha, sawa na asilimia 95.38 vimefikiwa na miundombinu ya umeme, huku wakandarasi wakiendelea na kazi ya kukamilisha usambazaji wa umeme kwenye vijiji 17 vilivyosalia ili kukamilisha vijiji vyote 368 vya mkoa huo na kufikia asilimia 100.

Mongella, kwa niaba ya wananchi wa mkoa huo,  ameishukuru Wizara ya Nishati na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuijali Arusha, kwa kutoa  fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo huku ikitoa kipaumbele kwa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya umeme kupitia mradi wa umeme vijijini (REA), miradi ambayo  iko hatua za ukamilishaji na kuvifikia vijiji vyote 368 vya mkoa wa Arusha.








Ends....

Post a Comment

0 Comments