TFA YATANGAZA GAWIWO NONO LA HISA KWA WANACHAMA WAKE, MTAJI WAPAA NANKUFIKIA BILIONI 52

Na Joseph Ngilisho Arusha.

Chama cha wakulima Tanganyika (TFA) kinatarajia kuanza kuwapatia gawio la hisa wanachama wake baada ya kusimama kwa muda kutokana na kutopata faida. 


Akizungumza jijini Arusha kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wakulima Tanganyika (TFA) mkurugenzi mtendaji Justine Shirima amesema kuwa kwa mwaka wa fedha ulioanza octoba 2023 hadi 2024 wanachama hao wataanza kupata gawio.


“Miaka mingine kampuni ilishindwa kutoa gawio kutokana na ilikuwa inajiendesha kwa hasara huku gharama za uendeshaji na matumizi yakiwa makubwa kulinganisha na mapato yaliyokuwa yanaingiza” alisema na kuongeza …


“Kuanzia mwakani wanahisa wa kampuni ya TFA wataanza kunufaika na gawio kutokana kupungua kwa hasara na kuongezeka kwa ufanisi na nidhamu ya matumizi na udhibiti wa gharama za biashara iliyosaidia kuanza kupata faida kwa misimu huu”


Amesema kuwa wamefanikiwa kupunguza kiwango cha hasara hadi kufikia shilingi 1.49 bilioni kwa mwaka 2023 kutoka 11.3 bilioni kwa miaka mitatu iliyopita katika vyanzo vyao vya mapato ikiwemo kodi ya mapango, biashara ya pembejeo na mashine mbali mbali wanazomiliki.


Amesema kuwa Mtaji umefikia kiasi cha shilingi 52.1 bilioni kwa thamani ya majengo, mashine na vifaa mbali mbali wanavyomiliki, na kufanya ongezeko la shilingi 4.6 bilioni kutoka 47.5 bilioni.

“kutokana na hayo tumeripoti ongezeko la shilingi 1.4bilion katika biashara ya pembejeo na 268milioni kwenye kodi ya pango, na malengo yetu ni kuimarika kwa faida katika mwaka ujao wa 2023/ 2024 hivyo kwa matumaini hayo wanachama wajue kampuni inaingiza faida na wataanza kupata gawio” alisema Shirima.


Aidha majibu hayo yametokana na maswali ya wanachama wakiwemo Eugenia Kweka na John Mbaga waliohoji utendaji wa kampuni yao wakidai kuwa hawaoni faida ya hisa zao za umiliki kutokana na hawapati chochote zaidi ya kupewa hesabu za hasara kila mwaka huku viongozi wanaoinga madarakani wakijichotea fedha na kukaa pembeni.


“Hakuna kitu kinauma kama unawekeza mahali jasho lako halafu hakuna unachokiona tunaomba leo viongozi mtupe mwelekeo unaotoa majibu ya hatma ya hisa zetu na kama hazina faida mseme kabisa maana wenzetu wanazidi kufa tulioanza nao” Amesema Eugenia


Kwa upande wake mkurugenzi wa bodi ya TFA, Waziri Barnabas amesema kuwa katika kuongeza ufanisi zaidi wanatarajia kupanua wigo wa kukuza biashara ili kufikia watu wengi zaidi.


“Katika mpango huo tunatarajia kufungua matawi mapya manne katika mikoa ya kigoma, Rukwa, Mwanza na Singida kwa mwaka 2024”


Aliongeza kuwa juhudi kubwa wanayoifanya kwa sasa ni kuhakikisha wanachama wao wanapata mbegu na pembejeo kwa gharama nafuu ili waweze kunufaika na shughuli zao.


Nae Stanley Mwandry alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuwapatia kibali cha uwakala wa pembejeo za ruzuku kwa bei nafuu ili kuwasaidia wanachama wao zaidi ya 4800 na wakulima wengine wanaowazunguka kupata kwa wakati lakini pia bila kuchakachuliwa.


Mwisho…

Post a Comment

0 Comments