Na John Mhala,Longido
Naibu Waziri wa Madini,Dkt Steven Kiruswa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Longido Mkoani Arusha amegoma kuchangia ujenzi wa shule ya Msingi Mundarara mpaka apate maelezo ya kina matumzi ya fedha shilingi milioni 600 zilizotimwa na Serikali Kuu zimetumikaje katika ujenzi wa shule hiyo.
Dkt Kiruswa alisema hayo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea ujenzi wa madarasa nane,ofisi ya utawala,vyumba vitatu vya maabara na vyoo hajijamaliziwa na nyumba ya mwalimu Mkuu haijajengwa,milango hakuna na sakafu haijamaliziwa na zimetumika zaidi ya shilingi milioni 576 katika ujenzi huo.
Alisema na anaambiwa fedha zilizobaki katika akaunti ni shilingi milioni 8 tu na bado shule haijakamilika kabisa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo,kupigwa rangi,sakafu bado,milango na ujenzi wa nyumba ya Mwalimu Mkuu.
Alisema katika kata zingine katika Jimboni la Longido fedha za Serikali Kuu zilizopelekwa katika kata kiasi kama hicho kilichopelekwa Mundarara shule ya Msingi kila kitu kimekamilika ikiwa ni pamoja na kuomba usajili wa shule na umekubaliwa na serikali na januari wanafunzi wanaanza shule lakini hilo ni tofauti katika shule ya Mundarara.
Waziri alisema kutonana hali hiyo alisema hatawezi kuchangia chochote hadi ufanyike ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha zote zilizotumika na apate majibu kwani kamati ya ujenzi wa shule hiyo haishirikishwi.
‘’Mimi sichangii fedha yoyote hapa mpaka nipate taarifa ya mkaguzi wa mahesabu kujua fedha zote zilizotumika katika ujenzi wa shule hiyo na pia nipate taarifa kwa nini kamati ya ujenzi wa shule haikushirikishwa na shughuli zote zinafanywa na Mwalimu Mkuu’’
Dkt Kiruswa alisema iwapo itabainika kuwa fedha zimeliwa hatua kali lazima zichukuliwe dhidi ya wahusika kwani serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inatoa fedha kwa maendeleoi ya wananchi lakini kuna wajanja wachache wako kwa ajili ya kujinufaisha na fedha hizo hilo halitakubalika.
Akizungumzia mgodi wa madini ya Ruby unaomilikiwa na Kijiji na mbia mwenza Rahmu Mollel maarufu kwa jina la Pendeza aliwataka wote kuheshimu mkataba ili kuepuka maneno maneno yasiyokuwa na msingi.
Dkt Kiruswa alisema katika mgodi huyo wa Kijiji Pendeza anahisa asilimia 75 na Kijiji kinamiliki hisa asilimia 25 lakini shughuli zote za uendeshaji zinafanywa na Pendeza na uzalishaji ukipatikana kila mmoja anapaswa kupata haki yake kwa mujibu wa mkatana.
Alisema madini ya ruby yanayozalishwa yanapaswa kuwekwa mezani ili bodi ya usimamizi wa mgodi ya Kijiji ijue na kabla ya mgao na shughuli zote zisimamiwa na maofisa wa Wizara ya Madini kabla ya serikali kuchukua kodi yake.
Waziri Kiruswa aliwataka waendesha shughuli za uchimbaji kushirikiana na Bodi ya Kijiji yenye wajumbe tisa katika shughuli za kila siku na uzalishaji ukipatikana ili kuondoa malalamiko kwa baadhi ya viongozi na wananchi kwa ujumla.
Naye Diwani wa Kata ya Mundarara,Alaise Mushao kabla alidai kuwa Pendeza hatoi ushirikiano na uongozi wa Kijiji na amekuwa akichukua pesa za viroba kwa wananchi na anazalisha na kuuza madini ya ruby bila kushirikisha viongozi kama mkataba unavyosema .
Mwisho
0 Comments