Na Joseph Ngilisho,ARUSHA
WABUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki EALA,kutoka nchi za Kenya na Tanzania wamechachamaa wakitaka kuletwa mbele ya bunge hilo hoja ya kujadili baadhi ya nchi wanachama kusuasua katika uchangiaji wa fedha,hali inayolazimu jumuiya hiyo kuendeshwa na michango ya nchi tatu kati ya saba na hivyo kushindwa kufikia malengo.
Hata hivyo wakati hoja hiyo ikiwasilishwa wabunge wa nchi zinazolengwa na hoja hiyo, walipinga isiwasilishwe na kuamua kutoka nje kwa lengo la kukwamisha akidi ya wabunge kuunga mkono hoja hiyo .
Awali hoja hiyo iliwasilishwa na Mbunge wa Kenya Maina Karobia na Dkt Abdulah Makame kutoka Tanzania wakilitaka bunge hilo kujadili kuhusu nchi za DRC Congo, Sudani Kusini na Burundi kushindwa kuchangia jumuiya hiyo tangu zijiunge na kukwamisha utekelezaji wa bajeti ya EAC hukunTanzania ikionesha kuchangia kwa asilimia 100.
Maina Karobia mbunge EALA (KENYA)
Dkt Abdullah Makame Mbunge EALA (TANZANIA)
Akiongea mara baada ya kuahirishwa kwa hoja hiyo katika Mkutano wa kwanza wa kikao cha pili cha bunge la Tano la EALA Jijini Arusha Mbunge wa Bunge hilo James Ole Milya alisema zipo nchi zinasuasua katika michango yao kinyume na mkataba wa jumuiya hiyo .
"Nchi ambazo zimekuwa zikichangia fedha kwa ajili ya uendeshaji wa jumuiya hiyo kiukweli nchi inayoongoza ni Tanzania ikifuatiwa na Kenya ,Uganda na Rwanda ,lakini wengine wanasuasua kwenye michango yao"
Kwa Mujibu wa Ole Milya nchi ya Tanzania inachangia kwa asilimia 100 ikiwemo kutoa Ardhi na ulinzi kwa nia ya kutaka Jumuiya iendelee kuwepo kwa manufaa mapana ya Wananchi wote wa nchi wanachama .
"Kwa hiyo Jumuiya hii kama waasisi wetu Mwalimu Nyerere,Obote na Kenyata wameasisi jumuiya kama tunavyoona wabunge wa Tanzania Kuna faida Kubwa ya kuwepo kwa mtangamano huu"
"Kinachotustaajabisha wenzetu zikitangazwa nafasi za Kazi katika Jumuiya ni wakwanza kuchangamkia na kupigania"
Alisema wabunge wao na watendaji wao wanalipwa na Jumuiya kwa michango ya nchi ya Tanzania fedha zinachochangwa na Watanzania.
Alisema sio kwamba Tanzania ina fedha nyingi ambazo hazina Kazi ,hoja yetu ni kwamba nchi zote wanachama zichangie ili kusukuma jumuiya yetu kwa maslahi ya wananchi wetu.
"Jumuiya hii tunaihitaji kwa sababu imeasisiwa na viongozi wetu ndio maana tunatoa fedha ambazo zingetengeza miundombinu mbalimbali katika sekta za Afya ,Elimu na Barabara tunachukua kidogo na kuweka humu kwa kuwa jumuiya tunaihitaji na tumeipenda".
"Hata hivyo tumesikitishwa sana kuona baadhi ya nchi zinazolengwa na hoja hii zikitoka nje ya Bunge kwa sababu ya diplomasia naomba nisizitaje kwa Sasa lakini utaona wale nchi zao hawachangii wanatoka nje kukwamisha hoja hii"
Awali wakiwasilisha hoja hiyo Mbunge wa EALA kutoka Kenya Maina Karobia na Mwenzake kutoka Tanzania Dkt.Abdullah Makame walitumia kanuni za Bunge hilo ambazo zinaruhusu kuahirisha baadhi ya vifungu katika kanuni za Bunge hilo katika suala la akidi wakizitumia kanuni hizo ili kupata hoja hiyo kuchangiwa na wabunge.
Suala la michango ya nchi Wanachama ndani ya Jumuiya limegeuka mwiba Mkubwa kwa nchi ambazo zimeonesha kutochangia fedha na kujikuta bunge likigawanyika makundi mawili kutokana na baadhi ya wabunge kugomea hoja hiyo na kutoka nje kwa lengo la kukwamisha hoja.
"Mimi sioni haja ya wabunge wa nchi ambazo hazichangii kutoka nje ya bunge kwa sababu wabunge wametumia kanuni za bunge ambazo zinaruhusu kuahirisha baadhi ya vifungu Kwenye kanuni zetu ili hoja ya msingi iweze kusimama na mheshimiwa spika kimsingi amekubali hoja ijadiliwe"
Naye mbunge wa EALA kutoka nchini Rwanda Fatuma Ndangiza alisema mjadala mwingine uliokuwepo ni namna ya kupitisha marekebisho ya kanuni na sheria za bunge ili kuendana na wakati ukizingatia kwamba nchi wanachama zimeongezeka na sasa wabunge wamefikia 63 na nchi wanachama 7.
Ends.......
0 Comments