CEDHA YAENDELEA KUNOA WAKUFUNZI WA AFYA,WANANCHI KUPATA WATUMISHI BORA WA AFYA

Na Joseph Ngilisho Arusha 

Wakufunzi kutoka vyuo vya Afya nchini wametakiwa kukitumia chuo cha Afya cha CEDHA kilichopo jijini Arusha, kujifunza ili kuwaongezea mbinu na ujuzi wa kuwafundisha wataalamu wa afya waendane na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia Suluhu katika sekta ya Afya.

Kauli hiyo imetolewa na katibu Tawala wilaya ya Arumeru, Joseph Mabiti kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo Emanuela Kaganda wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya wiki mbili yanayowahusisha  wakufunzi kutoka vyuo vya serikali ,binafsi na vyuo vya taasisi za dini kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Alisema wakufunzi wamekuwa wakiisaidia sana serikali kwa kuandaa wataalamu bora,watumie mafunzo hayo ya nadhalia na vitendo kupata stadi na mbinu muhimu za kufundishia ili kupata wataalamu wazuri watakaokwenda kuwahudumia wananchi.


"Tumieni elimu na ujuzi utakaopata katika mafunzo haya kama chachu ya mabadiliko ya kuongeza ufanisi katika vyuo vyenu  utakaopelekea kutoa huduma bora itakayoendana na uwekezaji ukubwa wa sekta ya afya uliofanywa na rais Samia"


Aliwaasa wakufunzi hao kuhakikisha wataalamu watakaoenda kuwafunisha wanazingatia weledi wa hali ya juu ili kuondoa manung'uniko kwa kuwa huduma zinapokuwa haziridhishi lawama nyingi humwendea rais Samia bila kujali uzuri wa majengo yaliyopo.


Aliwapongeza wakuu wa vyuo vya afya kwa kuwaruhusu watumishi wao kuja kujifunza  ili baadaye wakatoe elimu walioipata, aliwataka watumie mafunzo hayo kwa kuboresha sekta ya afya ili wananchi wapate huduma bora kwakuwa wanaitegemea serikali yao.


Alisema ni jambo muhimu kwa wakufunzi kujifunza katika taasisi ya CEDHA kwani ni msingi katika uboreshaji wa sekta ya afya,taasisi  hiyo imejipanga kikamilifu kupitia wawezeshaji wake kutoa ujuzi na mbinu  bobezi ili kuimarisha taaluma zao.


Awali Mkuu wa Chuo hicho,Dkt Johannes Lukumay alisema taasisi ya Cedha imeanzishwa na serikali kwa malengo manne ya kuhakikisha inatoa huduma iliyokusudiwa .


Alisema lengo la kwanza ni kufundisha wakufunzi wa afya mbinu mbalimbali za kufundishia ,kutoa elimu ya uongozi kwa watumishi wa afya waliopo kazini,kufanya tafiti kwa ajili ya kutatua changamoto za afya pamoja na ushauri elekezi. 


Katika hatua nyingine  alisisitiza kwa kuwasihi wataalamu wa afya na wakufunzi hapa nchini kuwashauri wananchi kujiunga na huduma ya bima ya Afya kwani hadi sasa waliofanikiwa kutumia huduma hiyo ni asilimia 15 tu kati ya watanzania zaidi ya milioni 61.



Ends..














Post a Comment

0 Comments