Na Joseph Ngilisho Arusha
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA ,imezifungia laini za simu zipatazo 34,848 zinazodaiwa kuhusika na uhalifu katika kipindi cha Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt Jabir Bakari amebainisha hayo jijini Arusha wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa sekta ya mawasiliano katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24.
Alisema kuwa laini za simu zilizofungwa ni zile zilizoripotiwa kupotea ,kuibiwa au kuhusika katika matukio ya uhalifu ikiwemo wizi na utapeli.
Hata hivyo alisema idadi ya laini zilizofungwa katika kipindi hicho imeshuka kwa asilimia 11.5 kutoka laini 39,394 kwa takwimu za mwezi juni 2023.
Aidha alisema katika kipindi hicho cha Julai hadi Septemba simu zipatazo 23,328 zilibainika kuhusika na matukio ya ulaghai au uhalifu ikilinganisha na simu 23,234 za mwezi Aprili hadi juni mwala huu.
'Ukilinganisha matukio ya mwezi julai hadi septemba utaona kuwa matukio ya uhalifu wa simu umepungua kidogo ukilinganisha na mwezi April hadi Juni hii ni kutokana na elimu juu ya matumizi ya namba 15040 ya kuripoti namba za wahalifu"
Akiongelea mawasiliano ya simu hapa nchini katika kipindi cha mwezi Septemba ,dkt Bakari alisema idadi ya watumiaji imeongezeka kwa asilimia 4.86 na kufikia laini milioni 67.12 kutoka laini 64.01 za mwezi Juni mwaka huu.
"Idadi hii ya laini za simu inahusisha laini kutoka mitandao 6 ya watoa huduma ambayo ni Airtel,Vodacom,Halsted,Ttcl,Tigobna Smile".
"Takwimu za sasa pia zinaonesha kuongezeka kwa watumiaji wa Intaneti kwa asilimia 1.24 kutoka watumiaji 34,047,407 mwezi juni mwaka huu hadi kufikia watu 34,469,022 mwezi septemba mwaka huu"
Alisema ongezeko hilo limetokana na uwepo wa maudhui ya kiswahili kwenye mtandao ikijumuisha kuongezeka kwa programu-tumizi kwa lugha ya Kiswahili.
Akizungumzia matumizi ya miamala ya fedha kupitia mitandao ya simu za mkononi katika kipindi cha robo ya mwaka ,dkt Bakari alisema takwimu zinaonesha kuwa akaunti za simu zimeongezeka kutoka 47,275,660 mwezi juni na kufikia akaunti 51,369,347 mwezi septemba mwaka huu ,sawa na ongezeko la asilimia 8.7.
Alisema katika katika kipindi hicho miamala ya fedha imeongezeka kutoka 420,675,884 kwa kipindi kilichoishia mwezi juni hadi miamala 422,390,546 kufikia septemba mwaka huu 2023.
Wakati huo huo dkt Bakari alisema kuwa jumla ya watoa huduma wa vituo vya radio vipatavyo 80 vimechukuliwa hatua ikiwemo kutozwa faini, onyo na adhabu kutokana na kukiuka wa taratibu za utoaji wa maudhui..
Aidha aliongeza kuwa TCRA kwa kushirikiana na wizara ya maendeleo ya jamii,jinsia,wanawake na makundi maalumu, imekamilisha uratibu wa programu maalumu ya kuandaa vipindi vya maadili vitakavyorushwa na vituo vya Utangazaji vipatavyo 150 vyenye leseni ya kiwilaya.
Alisema mpango huo umelenga kutoa elimu na kujenga jamii inayozingatia maadili ,mila ,destuli na Utamaduni wa mtanzania.
Sambamba na hayo TCRA imewakumbusha wananchi kuepuka kusambaza taarifa zozote zile zisizokuwa na uhakika na za uchochezi,kutambua na kiripoti kuhusu udanganyifu mtandaoni,na endapo yeyote akipokea ujumbe wa kitapeli au simu ya kitapeli atume ujumbe kwenda namba 15040.
Aidha TCRA imeendelea kuwasisitiza wananchi upatikanaji wa leseni za kidijitali kupitia mfumo wa Tanzanite Portal ,pamoja na kuhakikisha kuwa watumiaji hao wa huduma za mawasiliano kutoka TCRA ili kuendelea kuwa salama kupata huduma bora
Vilevile katika sekta ya Utangazaji zinaonyesha kuwa visimbizi 3,631,649 vilikuwa hewani hadi mwezi septemba 2023 ikilinganishwa na visimbizi 3,342,626 kwa.mwezi juni 2023 ambapo kati ya hivyo 1,789,090 ni vya dijitali kwa mfumo wa televisheni wa utangazaji wa mitambo ya ardhini na 1,846,559 ni vya mfumo wa televisheni wa setilaiti .
Alisema Dar es Salaam inaongoza kuwa na visimbizi 1,390,163 ikifiatiwa na Arusha (287,908) mwanza 282,779 na mbeya (229,570) mikoa yenye visimbuzi vichache kuliko yote ni Manyara( 1,816)
Ends..
0 Comments