Na Joseph Ngilisho Arusha
Shule yenye mchepuo wa kiingereza ya Tanganyika School iliyopo Njiro jijini Arusha imeingia matatani kwa kujihusisha na utoaji wa huduma ya Bima ya Afya kwa wanafunzi kinyume cha sheria bila kusajiliwa na kukusanya sh,milioni 207.6 kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2014.
Akiongea na vyombo vya habari jijini Arusha Kamishna wa Bima nchini Dkt Baghayo Saqware alisema kuwa shule hiyo imekuwa ikiendesha huduma hiyo kwa kutoza ada ya Bima ya afya ya sh,200,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari na sh,90,000 kwa kila mwanafunzi wa Awali.
Alisema kutokana na kosa hilo la jinai chini ya kifungu cha 161(1)cha Sheria ya Bima sura ya 394 mtuhumiwa huyo anakabiliwa na adhabu ya kufungwa miaka miwili jela,faini ya sh, milioni 5 au vyote kwa pamoja.
Alisema kuwa TIRA imejiridhisha kuwa shule hiyo inaendesha huduma ya Bima kwa kuwatoza wanafunzi ada ya Bima kinyume cha sheria na hivyo alimtaka mmiliki wa shule hiyo kulipa faini ya sh, milioni 5 kwa mamlaka hiyo na kuacha mara moja kukusanya Bima ya Afya kwa wanafunzi hao kabla ya sheria kali dhidi yake kuchukuliwa.
Pia imemtaka Kufanya utaratibu rasmi ili kusajili huduma hiyo kwa TIRA ikiwa kama bado anania ya kuendesha huduma hiyo na pia kurudisha fedha aliyokusanya kwa Alexander Oyuge katika kipindi cha miaka 9 wakati mzazi huyo akiwalipia watoto wake walikuwa wanasoma katika shule hiyo.
Aidha Mamlaka hiyo imeonya kuwa iwapo mmiliki huyo atashindwa kulipa faini hiyo kwa wakati ,TIRA itamfikisha mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi .
Dkt Saqware alisema mnamo januari 16 2023 ,TIRA ilipokea malalamiko kutoka kwa Alexander Lugale Oyuge mkazi wa Sakina jijini Arusha kuwa watoto wake wawili waliokuwa wakisoma katika shule hiyo,mmoja wapo alivunjika mguu lakini uongozi wa shule hiyo uligoma kumhudumia licha ya kupokea ada ya bima ya mzazi huyo.
Alisema shule hiyo imesajili wanafunzi 181 wa elimu ya awali na wanafunzi 1038 wa elimu ya msingi ambao wote wanatozwa Ada ya Masomo ,Ada ya Ukarabati,Ada ya Maendeleo,Ada ya BIMA ,Ada ya Vitabu na Kalamu na Ada ya Tahadhari.
Alisema mzazi huyo aliamini huduma ya Bima anayotozwa shuleni hapo imesajiliwa lakini alipofuatilia kwenye mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania TIRA,alibaini kuwa shule hiyo ilikuwa kiendesha huduma hiyo kinyume cha sheria.
Alisema kuwa mamlaka hiyo kupitia ofisi zake za kanda ya kaskazini ilifanyà ukaguzi katika shule hiyo na baadaye ilimwita kwa barua mmiliki wa shule hiyo aliyetambulika kwa jina la Brenda Mbori .Hata hivyo hakuweza kuitikia wito huo.
Kamishna wa Bima alisema aliandika barua nyingine ya wito septemba 13 na oktoba 10 mwaka huu akimtaka Brenda kufika mbele ya kamati ya Utekelezaji wa sheria ya TIRA ili wakutane pamoja na mlalamikaji kwa lengo la kupata ufumbuzi lakini pia hakuweza kutokea.
Mamlaka ya Bima imetoa onyo kali kwa taasisi, shule ama mtu yoyote anayejihusisha na kutoa huduma za bima bila kusajiliwa kuwa, atachukuliwa hatua kali za kisheria na kuwataka wazazi kujiridhisha na huduma za bima wanazohitaji kabla ya kulipia.
Ends...
0 Comments