Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Mkazi wa kijiji cha Misigiyo wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha,Veronica Makutiani(29) amenusurika kuuawa kikatili kwa kipigo cha baba yake mzazi pamoja na kaka yake ambaye ni katibu wa Mbunge Ngorongoro , wakimlazimisha kurejea kwa mume wake katili aliyekuwa akimtesa kwa kipigo na kumlaza njaa yeye na watoto wake wawili.
Alidai kwamba siku ya tukio oktoba 6 mwaka huu ,baba yake mzazi,Lekerenga Makutiani na Kaka yake Lingato Lekerenga ambaye ni katibu wa mbunge wa Ngorongoro ,walimshambulia kwa kipigo wakitumia vitu vigumu kiasi cha kupoteza fahamu, wakimshurutisha kurejea nyumbani kwa mume wake, Lesineti Koromo .
Alisema alilazimika kuyakimbia makazi yake alikokuwa akiishi na mume wake kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata ikiwemo kipigo ,kushinda na njaa na kunyimwa huduma muhimu kwa madai kwamba amepoteza mvuto baada ya kuzaa.
Alifafanua kwamba aliolewa na mwanaume huyo mwaka 2017 na kubahatika kumzalia watoto wawili lakini katika kipindi chote cha maisha yao ya unyumba maisha yake yalikuwa magumu sana kwani mara nyingi mwanaume huyo amekuwa akimpiga kumnyima chakula na kushindwa kutunza familia yake.
Alisema hivi karibuni mume wake alimtelekeza baada ya kukimbilia nchini Kenya na kumwachia watoto wake bila msaada wowote wa chakula hali iliyomlazimu kushinda njaa na kulazimika kurejea nyumbani kwa wazazi wake.
"Baada ya kufika nyumbani kwa wazazi wangu nikiwa nimedhoofu sana mimi na watoto wangu wawili ,baba yangu alinifukuza na kuniambia nisikae hapo niondoke na nirudi kwa mume wangu"
"Nilikataa kuondoka nikamweleza hali halisi ya nyumbani kwangu na mateso ninayoyapata nikimweleza simtaki tena huyo mwanaume ananitesa sana ,baba yangu na kaka yangu walikataa na kuniambia niondoke hapo vinginevyo wataniua na hawatakuwa na chakupoteza"
Alisema siku hiyo aliamua kuondoka na kwenda kuomba hifadhi ya kulala kwa watu baki na kesho yake alionekana akiranda randa kijijini hapo ndipo kaka yake alipomfuata na kuleta nyumbani na kuanza kumpiga kwa vitu vigumu huku wakimchangia kwa kipigo na baba yake alikuwa akimkanyaga tumboni na kwenye mbavu na damu zikaanza kumtoka sehemu za siri akapoteza fahamu.
"Wakati wakinishambuli
a mama yangu alikuwa akilia kwa uchungu lakini hakuwa na namna yoyote ya kunisaidia kutoka na mfumo dume wa mwanamke kutosikilizwa"
Alisema akiwa hajitambui na akiwa ametelekezwa nje ua nyumba majira ya usiku mama yake alikuja na kumchukua na kuanza kumpatia huduma ya dawa za kimasai ndipo alipozinguka na siku ya tatu wasamalia wema walimwona na kumpeleka katika zahanati iliyopo kijijini hapo kwa ajili ya matibabu.
Mganga mfawidhi wa zahanati hiyo Samweli Panga alipohojiwa na gazeti hili alikiri kumpokea Veronica akidai kwamba alifikishwa katika zahanati hiyo na watu waliodai ni wasamalia wema.
"Baada ya kumpatia vipimo tuligundua kwamba alikuwa na majeraha na uvimbe kichwani na alikuwa akilalamika mbavu kuuma na maeneo mengine ya mwili yanayoinesha alishambuliwa ,tulimtundikia drip chupa tatu na baadaye hali yake ilipotengamaa tulimruhusu kwa kumkabidhi kwa mtendaji wa kata hiyo"
Naye mtendaji wa kata ya Misigiyo, Onesmo Munga alisema alipata taarifa za tukio hilo na kufika katika zahanati hiyo na baadaye walifanya utaratibu wa kuokoa maisha yake kwa kutafuta msaada wa kujikimu ndipo walipomsafirisha hadi mjini Arusha na kumpatia hifadhi wakati taratibu zingine zikiendelea.
Kwa upande kwake Rose Njilo mratibu wa shirika la Mimutie Women Organization alisema ,alipokea taarifa za Veronica kutoka kwa afisa mtendaji wa kata hiyo na alimpokea nyumani kwake akiwa na hali mbaya na alipo mhoji alidai amepigwa na baba yake pamoja na kaka yake wakimlazimisha kuolewa.
Alisema shirika hilo litahakikisha linasimamia haki za mwanamke huyo iliwemo wahusika kuchukuliwa hatua kwa sababu anajua familia za kifugaji
"Sisi kama taasisi tunapambana na haki ya mwanamke kuhakikisha inapatikana na wahusika wa matukio ya ukatili na unyanyasaji wanachukuliwa hatua za sheria "
Kwa upande wake Katibu wa mbunge Lingato Lekerenga alipohojiwa kwa njia ya simu alikiri kumshambulia kwa kipigo dada yake akishirikiana na baba yake akidai ni utaratibu wa mila zao kutoa adhabu hiyo pale inapobainika mhusika wa damu wamekosea.
"Ni kweli Veronica ni dada yangu tena nampenda sana na nikweli nilimpiga ila nilimpiga kidogo tu kwa sababu alitukosea heshima kwa kukataa kwenda alikokuwa ameolewa"
Alisema kwa sasa yupo tayari kumwomba masamaha ili yaish2 na aje kuishi nyumbani mpaka hapo mambo yake ya ndoa yatakapokaa sawa yeye ba mme wake.
Jitihada za kumpata kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Justine Masejo ili kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana .
Hadi sasa watuhumiwa wapo mtaani na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na katibu wa mbunge anatamba kuwa alikuwa akitekeleza takwa la mila na alimtaka mwathirikaa aende popote hayupo wa kufanya chochote .
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Raymond Mangwala alipoulizwa kwa njia ya simu iwapo anataarifa za tukio hilo alisema hana taarifa ndo amefanyakuzikia kwa mwandishi wa habari.
Hata hivyo aliahidi kufuatilia ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Ends
0 Comments