WAZIRI NDALICHAKO AITAKA OSHA KUKOMESHA VIFO NA MAGONJWA MAHALA PA KAZI,TAKWIMU ZA KIDUNIA INATISHA

 Na Joseph Ngilisho,ARUSHA


Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu Kazi ,Vijana,Ajira na wenye Ulemavu Prof Joyce Ndalichako amemtaka wakala wa usalama na Afya Mahala pa Kazi,(OSHA)kukabiliana na vihatarishi mahala pa kazi ili kuepuka kuwa sehemu ya kuzalisha wagonjwa na wenye ulemavu bali patumike kukuza uwekezaji na kulinda nguvu kazi ya Taifa.


Prof Ndalichako ameyasema hayo jijini Arusha,wakati akifungua mafunzo maalumu ya Osha kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti yakiyolenga kuwapatia elimu  juu ya utendaji kazi wa Osha ili kuweza kuishauri serikali katika masuala mbalimbali ya bajeti.
Alisema ulimwengu wa sasa unakabiliwa na vihatarishi vingi mahala pa kazi kutokana na kukua kwa uchumi na mabadiliko ya teknolojia na hivyo akisisitiza kwa kuitaka Osha kujikita zaidi  kubuni mbinu mpya,kufanya ukaguzi wa mara kwa mara mahala pa kazi ,kutoa mafunzo na  elimu,kuweka mifumo ya udhibiti ili kulinda afya ya mfanyakazi .

Katika hatua ngingine waziri Ndalichako alisema kuwa serikali kupitia Osha imeondoa tozo zipatazo 13 na kuleta unafuu kwa wafanyabiashara ,wawekezaji nchini kwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa zaidi ya sh, bilioni 35.



"Sisi tunatamani pasitokee ajali kazini ama magonjwa ndio maana nawataka osha kutoa elimu zaidi ili kuwepo na uwekezaji mkubwa"

Awali katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu kazi ,vijana, ajira na wenye ulemavu,Cyprian Luhemeja alisema uwepo wa mafunzo hayo kutasaidia katika kusimamia usalama wa afya mahala pa kazi katika kuzuia ajali na magonjwa yatokanayo na kazi 

Alisema takwimu za kazi kwa mwaka duniani zinaonesha kuwa wafanyakazi takribani 2,300,000 wanakufa kutokana na ajali na magonjwa katika mazingira ya kazi .

Alisema wafanyakazi 350,000 na magonjwa yatokanayo na kazi yanakaribia kufikia 1,900,000 hivyo wafanyakazi 6400 hupoteza maisha kila siku duniani kutokana na magonjwa na ajali kazini.

Alisema kwa hapa nchini hali inaridhisha japo jitihada zaidi za pamoja  zinahitajika kukabiliana na hali hiyo .Hata hivyo alisema  gharama za fidia kwa wafanyakazi zimeongezeka kutoka bilioni 13.19 kwa kipindi kinachoishia juni 20/21 na kufikia bilion 17.9 kwa kipindi kinachonishia juni 20/23.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya bajeti, Daniel Sillo alishukuru kwa kamati hiyo kupata mafunzo hayo ikiwa ni matokeo ya kikao chao na Osha kilichoketi mkoani Dodoma na kuahidi kuisaidia Osha katika kutekeleza majukumu yake katika kulinda afya za wafanyakazi mahala pa kazi. 

Kwa upande wake mtendaji mkuu wa Osha,Hadija Mwenda alisema lengo la kuendesha  mafunzo hayo ni mpango mkakati wa kuongeza uelewa kwa wadau mbalibali ikiwemo kwa kamati ya bunge ya Bajeti ambao ndio watunga sera na ndio wanaopitisha bajeti ya serikali waweze kuwa na uelewa wa kutekeleza majukumu yao na kuishauri serikali.

Alisema kazi ya Osha ni pamoja na kulinda uwekezaji na kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi unakuwa na kuimarika na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji.

Hata hivyo aliishukuru serikali kuendelea kuiamini Osha na kuwapatia vifaa vya kisasa vyenye thamani ya sh bilioni 4.3 pamoja na magari 13 waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Ends...



















 


Post a Comment

0 Comments