WAKILI ALIYEKUWA AKISHIKILIWA GEREZANI ATIMUA MBIO MAHAKAMANI,AWAACHA POLISI WAKISHANGAA MATAA

 Na Joseph Ngilisho Arusha 

WAKILI wa kujitegemea, Peter Madeleka amelazimika kutimua mbio mahakamani mara baada ya mahakama kumpa dhamana na hivyo kuwaacha polisi  wakishangaa .

Staili aliyotumia wakili huyo ni pamoja na  kubadili nguo kisha kutoka kwa kasi  na kupanda bodaboda iliyokuwa ikimsubiri nje ya lango kuu la mahakama mara baada ya mahakama kuu kanda ya Arusha kumuachia kwa dhamana.


Hayo yametokea leo Septemba 8, 2023 majira ya saa tisa alasiri mara baada ya Jaji, Yohane Masara wa mahakama kuu kanda ya Arusha aliyesikiliza rufaa namba 87/2023  kumuachia kwa dhamana.

Madeleka aliamua kutumia mbinu hiyo baada ya yeye na mawakili wake kuhofia kuwa huenda akakamatwa tena na polisi waliokuwa wamevaa kiraia walionekana  ndani na nje ya mahakama  tokea majira ya mchana mara baada ya  mahakama kutoa uamuzi wa kumuachia kwa dhamana.

Wakili huyo ambaye kesi yake inafuatiliwa na wengi akiwa mahakamani alikuwa amevaa shati la bluu lenye mistari meupe ambapo mara baada ya kuachiwa kwa dhamana alitoka nje ya chumba cha mahakama akiwa amefuatana na mawakili wake kisha wakaingia kwenye moja ya vyumba vya mahakama.

Baada ya muda Madeleka alionekana akitoka nje ya jengo la mahakama akiwa kavaa koti jeusi miwani meusi na kofia akitembea kwa mwendo wa haraka hali ambayo haikuwa rahisi kutambulika.


Mwandishi wa habari hizi alimshuhudia Madeleka akitoka mahakamani hapo akifuatiwa na mdhamini wake ambapo walipokaribia lango kuu la dhamana walitimua mbio na  bodaboda iliyokuwa karibu na lango kuu kisha kuondoka kwa mwendo wa kasi.

Hata hivyo mawakili wa Madeleka, Boniface Mwabukusi alipoulizwa ni sababu ya hatua hizo, amesema  wamelazimika kutumia mbinu hizo alizoziita za kimedani kutokana na hofu huku akionya vyombo vya dola vinapokuwa mahakamani viuache muhimili huo utende kazi zake.


"Lakini ni vema wanapokuwa kwenye maeneo ya mahakama basi waiache mahakama ifanye kazi yake na watu waweze kuona ile sura ya mahakama. Mahakama ni sehemu ambayo inatafsiri vitabu inatafsiri sheria," amesema Mwabukusi.

"Mimi sifurahi,  mimi ni mmoja wa watu wanaosikitika sana kuona lundo la watu wanaojaribu kuufanya mchakato wa  mahakama kuwa wa kijeshi,"  

...Ila najua polisi wetu wana weledi basi watumie weledi kufanya kazi kwenye maeoneo yao na ya wengine wayaache katika sura yake na wanapolazimika kuwepo wajitahidi wawe katika sura inayomwalika kila raia  kwenye hilo eneo,".

Kuna wakati kwa kutumia mbinu za medani mtu anaweza kufa kwa kihoro anaweza kuruka dirishani vitu ambavyo  si sawa kabisa,".

Awali mahakama hiyo iliporejea majira ya mchana mbele ya Kaimu Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Boniface Semroki  Madeleka alitimiza masharti ya dhamana ambapo alisaini dhamana ya shilingi milioni moja na kudhaminiwa na mtu mmoja, Mzambia Amon Kabuje  ambaye naye alisaini dhamana ya shilingi milioni moja

Post a Comment

0 Comments