VODACOM NA DATA LAB YATOA MAFUNZO KWA WATOTO WA KIKE KUPENDA MASOMO YA SAYANSI,1900 WAMESHANUFAIKA,WALEMAVU WATAKA KUNOLEWA ZAIDI

Na Joseph Ngilisho Arusha 


Kampuni ya VODACOM Tanzania kwa kushirikiana na taasisi  ya Data Lab inayojihusisha na teknolojia kwa mtoto wa kike STEM, imewapatia mafunzo ya teknolojia ya sayansi kwa watoto wa kike na wenye ulemavu kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kupenda masomo ya sayansi na kuweka uwiano sawa kati ya mtoto wa kiume na wa kike.

Aidha wanafunzi wenye ulemavu mkoani ARUSHA wameiomba serikali pamoja na Wadau  kuhakikisha jamii yenye ulemavu haiachwi nyuma na maendeleo ya teknolojia ambayo ni hitaji lao la msingi katika kuwarahisishia ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji.
Akiongea katika hafla ya ufungaji wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha ,mratibu wa mafunzo hayo kutoka taasisi ya Data Lab,Somoe Mkwachu alisema lengo la mafunzo hayo ya siku nne ni kuondoa uwiano baina ya mwanafunzi wakike na wakiume na kumwezesha mtoto wa kike kupenda masomo ya sayansi .
"Tuliona ushiriki wa wanafunzi wa kike katika elimu ya sekondari huwa hawapendi kushiriki masomo ya sayansi wakidai ni magumu kwa hiyo kwa hiyo sisi Data Lab na VODACOM tuliamua kutoa mafunzo haya kwa watoto  wa kike ili kupunguza uwiano uliopo kati ya mtoto wa Kiume na Kike ili kuleta usawa katika ushiriki wa somo la sayansi"

Alisema mafunzo hayo ya siku yamelenga kupunguza uwiano wa masomo ya sayansi kwa mtoto wa kike hasa vyuo vikuu na sekta ya ajira namna ya kumfundisha binti  kutumia Kompyuta na kutengeneza website.
Kwa upande wake Meneja wa VODACOM kanda ya Kaskazini,George Venanti alisema tangia wameanza program  ya mafunzo hayo mwaka 2018  mkoa wa Arusha ni wa tano  na jumla ya wanafunzi wa kike 1900 wamefikiwa na kunufaika na mafunzo hayo.
Alisema wanufaika wa mafunzo hayo ni wasichana wenye umri wa kati ya miaka 14 na 19  na kwa mkoa wa Arusha wanafunzi wapatao 70 wakiwemo 22 wenye ulemavu wamehitimu na kupatiwa vyeti.

Alisisitiza kuwa lengo la VODACOM  ni kuhakikisha mtoto wa kike anajifunza masomo hayo ili kulete usawa kwani wasichana wananafasi ya kujifunza na kuyapenda masomo ya sayansi ili kuitumikia jamii.

Wakiongea kwa niaba ya waliohitimu wenzao ,Jasmine Kombo na Mariamu Rajab walisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa mtoto wa kike karika kumjengea uelewa juu ya masuala ya Teknolojia,Sayansi ,hesabu na uhandisi.

Rajab  mbaye ana ulemavu wa kutosikia aliishukuru VODACOM na Data Lab kwa kuwaongezea uelewa hasa matumizi ya Lugha ya Kompyuta  na kuitaka serikali kuona umuhimu wa kuwawezesha wenye ulemavu kwani wapo tayari kujifunza na wakiwezeshwa wanaweza.

Ends..
.



Post a Comment

0 Comments