Na Joseph Ngilisho Arusha
NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tenkolojia ya Habari,Mhandisi Mathew Kundo amesema Tanzania ipo mbioni kuweka sera, zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia katika uendelezaji wa miji maridadi Duniani.
Akizungumza jana jijini Arusha,katika mkutano wa siku kumi wa Kimataifa wa Shirika la Mawasiliano la Kimataifa la (ITU),uliokutanisha wataalamu wa teknolojia na mawasiliano kutoka ndani na nje ya nchi,Mhandisi Kundo alisema, uchumi wa kidigitali ndio utakaowezesha kuendanana na miji ya kisasa duniani.
Alisema sera hizo zitawezesha nchi ya Tanzania kujipanga zaidi na kuweka sera zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia hiyo, kwani Dunia kwa sasa, inakwenda kwenye uchumi wa dijitali wa kupata huduma yoyote kwa kutumia kadi bila kuwa na fedha tasilimu.
Aidha, alisema miji maridadi itabadilisha teknolojia kuwa za kisasa zaidi, katika ukusanyaji taka,ubora wa miundombinu ikiwemo biashara inayokua kwa kasi, sanjari na utoaji huduma bora za mawasiliano na nyinginezo.
"Ili kufikia hatua hii ni lazima sasa tuwe na sera nzuri, ambazo sasa tunazifanyia maboresho zaidi, ili Tanzania iendane na kasi ya teknolojia, hasa katika upangaji wa miji maridadi,"alisema
Mhandisi Kundo alisema washiriki wa mkutani huo, wanajadili maendeleo na changamoto zinazohusiana na teknolojia za mawasiliano na habari, katika ngazi ya kimataifa ikiwemo kikundi cha utafiti cha ITU-T kinachosimamia masuala ya Internet of Things (IoT) na miji smart.
Alisema vikao hivyo vinawakutanisha kwa pamoja wataalamu na wabunifu kutoka duniani, kujadili mwelekeo wa IoT na jinsi teknolojia hiyo inavyoweza kubadilisha maisha na namna tunavyoishi na kufanya kazi katika miji na jamii.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)Dk.Jabir Bakari alisema kuwa mkutano huo, utachangia kuimarisha uchumi wa kidigitali nchini na fursa ya kujifunza kutoka kwa nchi nyingine na kushirikiana ujuzi wake, katika miji maridadi,kutokana na wataalamu na wabunifu nchini kupata nafasi ya kujadiliana na wenzao kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Pamoja na majadiliano kuhusu IoT na miji smart, mkutano pia unajumuisha masuala mengine muhimu kama usalama wa mifumo ya IoT na faragha, viwango vya teknolojia hizo , na faida za kiuchumi zinazotokana na maendeleo haya.
........Ends.......
0 Comments