WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA YAJIFUNGIA KUTEKELEZA MAELEKEZO YA RAIS SAMIA,NAIBU WAZIRI KIGAHE NAYE ACHARUKA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA MENEJIMENTI NA TAASISI ZAKE


Na Joseph Ngilisho Arusha

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara , Exaud Kigahe ameiagiza Menejimenti ya Wizara hiyo na Taasisi zake kuhakikisha  zinakuwa mstari wa mbele kuweka mazingira bora na wezeshi katika sekta ya viwanda na biashara nchini ili kuvutia uwekezaji. 


Kigahe ameyasema hayo Agosti 23, 2023  alipokuwa akifungua Kikao Kazi cha Menejimenti na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa CAMARTEC,jijini Arusha ikiwa ni siku chache mara baada ya rais Samia Suluhu Hassan kufungua kikao kazi jijini hapa na kutoa maelekezo ambayo Wizara hiyo imeanza kuyatekeleza .

Alisema kikao kazi hicho kimelenga kujadiliana na kuimarisha ushirikiano katika utatuzi wa changamoto katika sekta ya viwanda ili kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kuwa wizara hiyo inategemewa pia na sekta zingine katika uzalishaji mali.

Aidha, Kigahe amezitaka Taasisi hizo zinazojumuisha TIRDO, TEMDO, NDC , CAMARTEC, TBS, WMA, BRELA, FCC, FCT, TANTRADE na CBE  kuhakikisha zinakuwa mstari wa mbele kuweka mazingira bora na wezeshi katika Sekta ya Viwanda na Biashara inayotegemewa na sekta  muhimu za uzalishaji kama kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili  kwa viwanda vya kuongeza thamani  mazao na masoko ya bidhaa hizo.
 

Vilevile, Wakati akiongea na Benki ya NMB, amezishauri Taasisi za Kifedha kupanua wigo wa utoaji wa huduma za kifedha ndani na nje ya nchi pamoja na kupunguza masharti ya utoaji wa mikopo ili kuwawezesha wafanyabiashara wengi kianzisha na kuendeleza biashara zao na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.


Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah alisema lengo kuu la Kikao Kazi hicho ni kutafsiri majukumu na shughuli zote za Wizara na Taasisi zake kwa kuzingatia maelekezo  yaliyotolewa katika kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma,kilichozinduliwa na rais Samia Agosti 19, 2023 jijini Arusha. 

Alisema katika kikao kazi hicho kilichoshirikisha pia taasisi za fedha ,benki ya NMB kinalenga  kuangalia mahitaji ya kimitaji katika sekta ya viwanda ili kuwezesha sekta binafsi  kuwapatia nyenzo za kufanyia biashara.

"Tumejifungia hapa ili kujadiliana na kupeana mikakati ya kiutendaji na kwenda katika utekelezaji "

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara na Mkurugenzi Mkuu  wa shirika la utafiti na maendeleo ya viwanda Tanzania(TIRDO) Madundo Mtambo  pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA , Stella Kahwa wamesema Kikao kazi hicho ni muhimu kwa kuwa kinawawezesha  kutatua changamoto zinazowakabili na kutekeleza majukumu ya taasisi zao kwa ufanisi.

"Tumeweka utaratibu wa kukutana na kujadili kwa pamoja ili kuona umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi na taasisi hizi  ili kuongezantija katika uchumi kupitia sekta ya viwanda na biashara"alisema Mtambo

Awali, akitoa elimu kwa wajumbe Kikao hicho,  Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Serikali na Binafsi Makao Makuu ya Benki ya NMB,  William Makoresho  alisema NMB iko tayari kushirikiana na Taasisi hizo ili kutimiza adhima ya kusaidia maendeleo ya viwanda na biashara .







Ends...

Post a Comment

0 Comments