Na Joseph Ngilisho Arusha.
Hatima ya kupata dhamana Wakili maarufu nchini Peter Madeleka anayeshikiliwa katika gereza la Kisongo Arusha, itajulikana leo Agosti Mosi, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Madeleka anayeshikiwa mahabusu tangu Julai 17, 2023 baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha baada ya uamuzi uliotolewa na Jaji Aisha Bade wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, katika kesi ya kupinga makubaliano ya kukiri kosa 'Plea bargaining'.
Jana Jumatatu Julai 31, 2023 kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 40/2020 inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Madeleka anawakilishwa na jopo la mawakili watano wakiongozwa na Wakili Boniface Mwabukusi akiwa pamoja na mawakili Simon Mwambo, Joseph Ole Shangai, Dennis Mosses na Kenedy Chando.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa, Jamhuri iliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Upendo Shemkole, Mahfudhu Mbagwa na Tony Kilomo.
Baada ya kutajwa kesi hiyo jana, Wakili Upendo aliieleza mahakama kuwa shauri limepangwa kwa ajili ya kutajwa na kuwa upelelezi haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine ya kuitaja.
Kwa upande wake Wakili Mwabukusi aliwasilisha ombi la dhamana akisema, kwa kuwa shtaka linalomkabili mteja wao lina dhamana na kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika, mahakama impe mteja wao haki yake ya dhamana kwa masharti nafuu yatakayomwezesha kufikia haki hiyo.
Hata hivyo, Wakili Upendo aliwasilisha ombi kwa Mahakama hiyo akitaka imnyime dhamana washtakiwa akidai katika kesi inayomkabili ana makosa10 ikiwemo utakatishaji fedha ambalo halina dhamana.
Amedai kuwa, kilichoamuliwa na Jaji Bade kuondoa makubaliano ya plea bargaining, yaliyofanyika Aprili 27, 2021 na kuwa baada ya kufutwa kwa mwenendo mzima ikiwemo makubalino ya kukiri kesi hiyo kutakiwa kuendelea katika mahakama hiyo ya chini, hivyo hati inayomshitaki ni ya awali ambayo ina makosa10 likiwemo utakatishaji fedha
Akijibu hoja za Wakili wa Serikali, Wakili Mwabukusi ameieleza mahakama kwamba, hati ya mashtaka siyo sehemu ya plea bargain na kuwa hati iliyopo mahakamani hapo ni ya Aprili 27, 2021 ambayo ina kosa la uhujumu uchumi lenye dhamana.
Hakimu Mbelwa aliahirisha kesi hiyo hadi kesho Agosti Mosi, 2023 kwa ajili ya kutoa uamuzi mdogo iwapo mshitakiwa huyo atapewa dhamana au la.
Awali kesi hiyo iliahirishwa kwa muda wa dakika 20 baada ya Wakili Mwabukusi kuieleza mahakama kuwa askari Magereza waliwafukuza na kuwanyima fursa ya kukutana na mteja wao kwa ajili ya mazungumzo ya faragha hivyo kuomba mahakama iwape muda wa kukutana na mteja wao.
Kabla ya ombi hilo, Wakili Madeleka alinyoosha kidole mahakamani hapo, hali iliyofanya Hakimu Mbelwa kuwataka mawakili wake kuzungumza na mteja wao na baada ya majadiliano mafupi ndipo Wakili Mwabukusi aliwasilisha ombi hilo.
"Tuna ombi mbele yako ili tuweze kujibu alichozungumza mwenzetu. Tulinyimwa fursa ya kukutana na mteja wetu na wenzetu wa Magereza tulijitahidi muda wote lakini tuliishia kufukuzwa kwa hiyo tunaomba ikupendeze tupate ahirisho la dakika 20 au 15 ili tuzungumze faragha na mteja wetu," aliomba Wakili Mwabukusi
Julai 17, 2023 Madeleka alikamatwa na Polisi baada ya kutoka Mahakama Kuu katika kesi yake ya kupinga makubaliano ya kukiri kosa ‘Plea bargaining na kushitakiwa tena.
Wakili Madeleka aliwasilisha maombi namba 80 ya mwaka 2021 kutokana na kesi aliyokuwa amefunguliwa ya uhujumu uchumi namba 40/2020.
Wakili Madeleka pia aliiomba Mahakama Kuu itoe amri ya kurejeshewe faini ya Sh2 milioni, kwa madai kuwa mchakato mzima ulikuwa ni kinyume cha sheria.
0 Comments