Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA.
SHIRIKA la Sightsavers limeutambulisha mradi mpya utakaojulikana kama Macho Yangu utakaotekelezwa kwenye mikoa ya Singida, Morogoro na Dodoma ambapo watu 150,000 wanatarajia watapatiwa huduma ya uchunguzi wa macho na wengine 15,000 watafanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho katika mikoa hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Godwin Kabalika, akizungumza jana wakati wa kikao cha kutambulisha mradi huo kilichofanyika mjini Singida na kuwashirikisha
Alisema mradi huo mpya umeanza baada ya ule wa Boresha Macho ulioanza kufanya kazi 2019 na kufikia tamati 2022 ambao uliwa ukitekelezwa katika mikoa ya Singida na Morogoro.Kabalika alisema mradi huo mpya pia utatoa miwani kwa watu 15,000 na kusaidia vifaa tiba vinavyohusika na macho kwenye vituo vya kutolea huduma katika mikoa hiyo ambako mradi utatekelezwa.
“Baada ya mradi wa Boresha Macho kwisha tukaona kuna uhitaji mkubwa wa huduma za macho kwenye mikoa ya Singida na Morogoro tukaona tuanze mradi mpya wa Macho Yangu na tukaongeza mkoa wa Dodoma ambao nako wananchi wake wanakabiliwa na changamoto ya macho,”alisema Kabalika.Kabalika alisema wakati wa utekelezaji wa mradi huo, watoa huduma za macho watapewa mafunzo namna ya kutoa huduma bora ambapo wananchi watakuwa wanahamasishwa kwenda kupata huduma hizo kwenye vituo vya kutolea huduma.
Naye Mratibu wa Mradi wa Macho Yangu Mkoa wa Singida, Upendo Minja, alisema kwa mkoa huu wananchi 50,000 watafanyiwa uchunguzi wa huduma za macho, 5,000 watafanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na wengine 5,000 watapewa miwani katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa mradi huo.Minja aliwaomba viongozi wa halmashauri zote za saba za Mkoa wa Singida kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za macho ili mradi huo uweze kufanikiwa zaidi kama ilivyokuwa wakati wa utekelezaji wa mradi wa Boresha Macho kwani lengo la Sightsavers ni kutaka kuhakikisha tatizo la uono hafifu kwa wananchi linapatiwa ufumbuzi.
Naye Mratibu wa Huduma za Macho Mkoa wa Singida, Upendo Mwakabalile, alisema mradi wa Boresha Macho ambao umekwisha umekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za macho kwa wananchi mfano ulijiwekea lengo la kuwafanyia upasuaji wa mtoto wa jicho watu 5,625 lakini hadi mwisho wa mradi wamefanyiwa watu 7,995 na hivyo kuvuka lengo lililokuwa limewekwa.
Alisema katika huduma ya uchunguzi wa matatizo ya macho, mradi huo ulijiwekea lengo la kuchunguza watu 62,500 lakini wamefanyiwa uchunguzi watu 110,834 huku wengine 3,770 wakipewa huduma ya miwani kati ya lengo lililowekwa la kuwapatia watu 2,500 kutoa huduma hiyo.
Kwa upande wake Afisa Mradi Sightsavers, Sabina Maheke, alisema mbali na mradi wa Macho Yangu, shirika hilo pia limekuja na mradi mpya wa uwezeshaji kiuchumi kwa watu wenye ulemavu ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili katika mikoa ya Singida na Dar es Salaam.
Alisema malengo makuu ya mradi wa uwezeshaji kiuchumi watu wenye ulemavu ni kuongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika soko la ajira na utafanya kazi na vyama vya watu wenye ulemavu na waajiri ili kutoa fursa za ajira kwa jamii hiyo.
Maheke alisema mradi huo pia utafanya kazi na wadau mbalimbali wa kilimo hususani katika kilimo cha zao la mtama kwa mkoa wa Singida na unalenga walemavu wa aina zote wenye umri kuanzia miaka 16 hadi 35 ambao wapo kwenye soko la ajira na wenye umri kuanzia miaka 16 hadi 60 ambao wanaweza kujiajiri wenyewe.
Aliongeza kuwa mradi huo utawafikia watu 360 kwa mchanganuo wa watu 120 kutoka mkoa wa Singida na 240 kutoka mkoa wa Dar es Salaam ambapo kipaumbele zaidi kitakuwa ni kwa wanawake kwasababu ndio wapo nyuma kutokana na mifumo mbalimbali iliyopo nchini Tanzania.
“Tutafanya kazi na taasisi zote zinazojihusisha na walemavu, Maafisa Ustawi wa Jamii, lakini pia tutajumuisha na vyuo vya ufundi stadi vilivyoteuliwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu na mradi huo utatekelezwa kwenye wilaya tano za Mkoa wa Singida na wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji, Stanslaus Choaji, ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo wananchi wake wengi walikuwa na changamoto ya magonjwa ya macho lakini tangu ujio wa Shirika la SightSavers tatizo hilo limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na huduma nzuri zinazotolewa na shirika hilo.
“Sightsavers imekuwa na mchango mkubwa sana katika sekta ya afya kwa mkoa wetu wa Singida imesaidia hata kujenga vituo vya kutolea huduma za macho kwenye Halmashauri ya Singida DC, Mkalama na Ikungi na kuwafikia wananchi kuwapatia huduma za macho hasa kwa wale ambao hawawezi kufika kwenye vituo vya kutolea matibabu,” alisema Choaji.
Choaji aliliomba shirika hilo kama itapendeza kujenga vituo zaidi vya kutolea huduma za macho kwenye halmashauri zaidi za mkoa wa Singida ambazo hazijapata huduma hiyo ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Itigi, Iramba na Manispaa ya Singida.
“Sisi kama serikali tunaahidi kutoa ushirikiano ili malengo ya Shirika la Sightsavers yaweze kutimia na malengo ya serikali ya kuwapatia wananchi huduma bora za macho na afya kwa ujumla ziweze kufikiwa,” alisema Choaji.
Alisema utaratibu wa kuwafuata wananchi waliko na kuwapatia huduma za matibabu ya macho ni mzuri sana na umesababisha kuongezeka kwa watu wanaohitaji huduma hiyo hasa ikizingatia kuwa baadhi wanaishi maeneo ambayo yapo mbali na vituo vya kutolea huduma za macho.
Aidha, Choaji aliwagiza Waganga Wakuu wa Wilaya na Waratibu wa Macho kutoa ushirikiano kwa shirika hilo ili mradi mpya wa Macho Yangu uweze kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, ……………..alilishukru Shirika la Sightsavers kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika utoaji wa huduma mbalimbali za afya ikiwamo huduma za macho na utoaji wa vifaa tiba.
Alisema mradi mpya wa Macho Yangu umeshatambulishwa katika ngazi ya Taifa kwa maana ya katika Wizara ya Afya na katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na sasa ni zamu ya kuutambulisha katika ngazi ya mkoa wa Singida.
Alisema mradi huo utatekelezwa kulingana na malengo yaliyowekwa ili wananchi waweze kupata huduma bora za matibabu ya macho na kuwataka wadau wote wanaohusika na sekta ya afya kutoa ushirikiano kwa Shirika la Sightsavers ili huduma ziweze kutolewa kwa ubora.
MWISHO
0 Comments