SHAHIDI KESI YA MAUAJI YA DADA WA BILIONEA MSUYA,AONESHA KISU,PILIMBI,CHUPI YA DHAMBARAU,VYENYE DAMU YA MAREHEMU

 

 By Ngilisho TV Dar es Salaam.


Shahidi wa 15 katika kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; amehitimisha ushahidi wake baada ya mahojiano kuhusiana na matokeo ya uchunguzi wa vinasaba (DNA).

Shahidi huyo, Mkemia Dk. Fidelis Segumba, ambaye ni meneja wa  Maabara ya Sayansi Jinai Kemia katika Ofisi ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali amehitimisha ushahidi wake leo, Jumatano, Agosti 16, 2023 baada ya kutumia siku mbili huku akibanwa kwa maswali ya dodoso na Wakili wa utetezi Peter, Kibatala kuhusiana na ushahidi wake.

Mjane huyo wa Bilionea Msuya; Miriam Steven Mrita anakabiliwa na shtaka la mauaji ya wifi yake, Aneth Msuya, yeye pamoja na mshtakiwa mwenzake Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray.

Aneth aliuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, miaka mitatu tangu kuuawa kwa kaka yake, Bilionea Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018 inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Dk Segumba ndiye ndiye aliyefanya uchunguzi wa vinasaba katika vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio la mauaji hayo, alivyovipokea Agosti 30, 2016 kutoka Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi ya Jeshi la Polisi,Temeke,  wakati huo akiwa meneja wa Maabara ya Uchunguzi wa Sayansi Baiolojia na Vinasaba.

Vielelezo hivyo ni kisu chembamba chenye mpini mweusi kilichodhaniwa kutumika kayika mauaji hayo,  chupi ya rangi ya zambarau inayodhamiwa alikuwa ameivaa marehemu Aneth, filimbi iliyodhaniwa alikuwa akiitumia Aneth na  mpanguso wa ndani ya mashavu ya mshtakiwa wa pili, Muyella.

Katika ushahidi wake jana aliieleza mahakama kuwa katika uchunguzi wake ulionesha kuwa kisu, chupi na filimbi vilikuwa na  damu ya Binadamu na kwamba vinasaba katika baadhi ya vielelezo hivyo vilikuwa uhusiano kati ya marehemu na mshtakiwa wa pili Muyella.

Baada kuhitimisha ushahidi wake huo wa msingi ndipo Wakili Kibatala alipomhoji maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake hasa kuhusiana na damu hiyo iliyokuwa kwenye kisu, jana na kuhitimisha mahojiano hayo leo.

Sehemu ya mwisho mahojiano baina ya Wakili Kibatala na shahidi huyo jana  pamoja na maswali ya ufafanuzi kutoka kwa mwendesha mashtaka ilikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala: Ulisema ulisoma kozi ya forensic Genetic in wildlife, ulimaanisha nini?


Shahidi: Ni kozi ya uchunguzi wa vinasaba vya wanyama

Kibatala: Maana yake ni nini? kwamba hata wanyama wana DNA?

Shahidi: Hata mimea inayo.

Kibatala: Kwenye item B chupi ya rangi ya zambarau ulisema uchunguzi ulionesha umiliki wa jnsi mbili, source ilikuwa ni nini?

Shahidi: Source kwangu ni chupi inayodhaniwa alikuwa ameivaa marehemu Aneth Msuya na kuvuliwa kwa nguvu.

Kibatala: Kwa kuwa analysis yako inaonesha genetic profile mbili (ya kiume na ya kike) huwezi kuona kuwa chanzo ni huyo binti kujamiiana na mtu mwingine kabla ya tukio?

Shahidi: Kwa uchunguzi nilioufanya mimi siko katika position ya kusema hilo kama ni kweli au la.

Kibatala:  Na pia huwezi kusema kwamba hiyo chupi ilivuliwa kwa nguvu kama ile barua ya maombi ya uchunguzi iliyoletwa ilivyosema, huwezi kujua ilivuliwa kwa nguvu katika tendo gani? wakati wa kuuawa au wakati anafanya tendo la ndoa?

Shahidi; Hilo siwezi kusema.

Kibatala: Wala huwezi kusema kwa hakika kuwa hizo genetic profile mbili ziliingia kwa wakati mmoja au kwa nyakati tofauti?

Shahidi: Kwa uchunguzi wangu siwezi ku-determine.

Kibatala: Umesema kwenye uchunguzi wako jinsi inaonesha kinamilikiwa na jinsi mbili una maana gani?

Shahidi: Maana yake ni kwamba kielelezo hiki kina  jinsi (tawala/ wamiliki wake) ya kiume na jinsi ya kike.

Kibatala: Kwenye kielelezo C, filimbi ya chuma ambayo inadhaniwa kuwa ilikuwa inatumiwa na marehemu Aneth pia umeyapata kwenye barua uliyoletewa?

Shahidi: Ndio maana yake

Kibatala: Huyu mmiliki mwenye jinsi ya kike wewe unamfahamu?

Shahidi: Labda kwa jibu ambalo ni general kwa vielelezo vyote hivi hakuna ninayemfahamu

Kibatala: Ahaa, sasa shahidi nakupeleka ukrasa wa pili wa hii ripoti yako.umesema uchunguzi wa awali umedhihirisha kuwa kina damu ya binadamu, Unafahamu zilikuwa damu za watu wangapi?

Shahidi: Hapo sijui

Kibatala: Ni sampuli gani iliyoletwa kupima kutoka kwa mshtakiwa wa pili?

Shahidi: Mpanguso kutoka ndani ya mashavu yake.

Kibatala: Katika ripoti yako utangulizi unasema ulipokea kifurushi kilichofungwa kwa lakiri, unafahamu kwa nini kilifungwa kwa lakiri?

Shahidi: Nafahamu

Kibatala: Mwambie Jaji kwa nini?

Shahidi: Ni utaratibu sampuli zinazoletwa maabara kuwa katika hali ambayo siyo easy kuwa tempered

Kibatala: Ulitoa hapa mahakamani hiyo bahasha iliyotoka maabara ili mahakama ijiridhishe kwamba hicho kifurishi kilikuja kwako kikiwa sealed (kimefungwa kwa lakiri? kwa sababu sheria inaelekeza.

Shahidi: Ndio,hivyo nilivyopokea baada ya uchunguzi nikavifunga tena ndiyo niliyoitoa jana.

Kibatala: Wakati una-unseal ulikuwa na mtu mwingine kuhakikisha kuwa ume-unseal?

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Uliifafanulia Mahakama kuwa wakati unapokea na ku-unseal ulikuwa peke yako?

Shahidi: Ndio.

Maswali ya ufafanuzi

Baada ya maswali hayo ya dodoso kutoka kwa Wakili Kibatala, yaliyolenga kutikisha uimara wa ushahidi wake, mwendesha mashtaka, Wakili Kimweli alimuongoza tena kwa maswali kufafanua mambo mbalimbali yaliyoibuliwa na Wakili Kibatala katika maswali ya dodoso.

Sehemu ya mahojiano yao ilikuwa kama ifuatavyo:Kimweri

Wakili: Shahidi nitakuongoza kwenye maeneo ambayo umehojiwa na Wakili (Kibatala).

Uliulizwa na Wakili kuhusiana na umuhimu wa barua ambazo ulikirejea kwenye ripoti yako ( barua ya Polisi kuomba kufanyiwa uchunguzi wa vielelezo husika) ukajibu kwamba kwako wewe hizo barua nyingine zilizoambatana siyo muhimu Sasa ifafanulie mahakama Kwa ni I umesema hivyo?

Shahidi: Barua ambayo ilielekezwa kwangu kwa ajili ya kufanya uchunguzi ndiyo iliyowasilisha vielelezo na kusema uchunguzi gani unafanyika,  hizi nyingine ziliambatanishwa kama vielelezo na hazikuelekezwa kwangu kuniambia nifanye uchunguzi gani.

Kwahiyo ninaandika ripoti yangu Kwa kurejea barua iliyonielekeza kufanyia kazi.

Wakili:  Pia alikuuliza iwapo ulioneshwa au uliziona hapa mahakamani ukasema kwamba hujaoneshwa. Sasa hebu toa ufafanuzi hiyo hoja ya kuoneshwa

Shahidi: Kama nilivyosema awali barua inayonielekeza kufanyia kazi na ninapojibu najibu kwa kurejea hiyo.Sababu ya kutooneshwa ni kwamba hapakuwa na sababu ya msingi sababu sizo nilizofanyia kazi

Wakili: Na kuhusu hilo la kuiambatanisha kwenye ripoti?

Shahidi: Si utaratibu kwenye ripoti kuweka viambatisho, ila naandika ripoti kwa kurejea hiyo barua ya kufanyia kazi.

Wakili:  Pia uliulizwa kuhusiana na matakwa ya kuingiza orodha ya hivyo vielelezo kwenye register na ulijibu kanuni zinataka na kwamba wewe ndio uliingiza na akakuuliza hiyo register hapa, wewe unaieleza nini Mahakama?

Shahidi: Narudia kama nilivyosema awali sijaambatanisha kwenye ripoti kwa sababu si utaratibu kuandika ripoti na kuambatanisha viambatisho.

Wakili: Shahidi uliulizwa pia suala la zile sampuli za DNA kwamba upo uwezekano wa kuwa contaminated na kwamba unafahamu kama zilikuwa contaminated huko zilikotoka ukasema hufahamu sasa ifafanulie mahakama kuhusu hilo.

Shahidi: Kuhusiana na contamination maana yake ni uwezo wa kufahamu kwamba kunakuwepo na profile (taarifa binafsi ya mhusika wa vinasaba vinavyochunguzwa) ambayo hukutarajia iwepo.

Mimi uchunguzi wangu nilioufanya kwa kuzingatia nilicholetewa bila kufahamu kama kilikuwa contaminated na katika majibu yangu nikasema kulikuwa na mwingiliano wa vinasaba. Kwa hiyo siwezi kutolea ufafanuzi suala la contamination.

Wakili: Swali lingine uliulizwa kama ni kweli kabla hazijakufikia wewe (sambpuli/vielelezo) kuna watu wengine kilipitia kwao ukasema ni kweli, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Kabla ya kufika maabara kielelezo lazima kiwe identified, kifungwe na kuletwa sasa lazima kuna watu waliofanya hiyo kazi.

Wakili: Pia uliulizwa kuhusiana na kisu kuwa katika uchunguzi wa awali unaonesha kina damu lakini akakuuliza kwamba hiyo damu unaweza kueleza kwamba ilikuwa ni ya Aneth ulijibu kwamba huwezi kutoa jibu la moja kwa moja kwamba ni ya Aneth, hebu toa ufafanuzi wa hilo.

Shahidi: Ufafanuzi nitakaoutoa utakuwa bado unarudi kwenye maelezo ya kielelezo. Kwa sababu inahusianisha na maelezo yaliyoko kwenye kielelezo kuwa kisu hicho kinadhaniwa kutumika kukata shingo ya marehemu Aneth. Kwa hiyo mahusiano ya damu hiyo na Aneth yanapatikana kwenye kielelezo.

Wakili: Shahidi, Wakili pia alikuelekeza kwenye kielelezo  A (kisu) na kielelezo D (mpanguso wa ndani ya mashavu ya mshtakiwa wa pili) kuwa kuna uhusiano hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Kielelezo A ambacho ni kisu katika sehemu ya mpini (Ai) ilikuwa na uhusiano wa kijenetiki kuchangia na kielelezo D (mpanguso ndani ya shavu la mshtakiwa wa pili)

Wakili: Sasa twende kwenye kielelezo B (chupi inayodhaniwa alikuwa ameivaa marehemu Aneth) na kielelezo D.

Shahidi: Kwa kulinganisha mahusiano ya mpangilio wa vinasaba kutoka kielelezo B na kielelezo D umedhihirisha kuwa vinasaba kutoka kwenye vinasaba hivyo havina uhusiano.

Ends....

Post a Comment

0 Comments