RAIS SAMIA AWANYOSHEA KIDOLE MAWAZIRI WANAOGEUZA MASHIRIKA YA UMMA KUWA VYANZO VYAO VYA MAPATO

Na Joseph Ngilisho ARUSHA


RAIS Samia Suluhu Hassan amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Mawaziri na watendaji wa Wizara kugeuza Mashirika ya Umma kama vyanzo vyao vya mapato akisisitiza mpango huo umekuwa ukidhoofisha mashirika kuchangia katika mfuko mkuu wa serikali.


Akifungua Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma jijini Arusha, Rais Samia amesema kumekuwa na baadhi ya Wizara ambazo zimekuwa zikiomba michango kutoka katika taasisi zilizo chini ya Wizara zao kipindi zinapoishiwa bajeti ya matumizi mengineyo (OC).


Wizara nyingi zimefanya mashirika kuwa vyanzo vya mapato. Mashirika yanapaswa kuchangia gawio … Wizara zinaweka mikono katika mapato ya mashirika hii haitakiwi kama tunataka mashirika yazalishe tusiyaingilie,” alisema Rais Samia jijini Arusha.


Kwa mujibu wa Rais Samia kuna mashirika yaliundwa kujitegemea lakini yameshindwa kujitegemea na leo ni tegemezi serikalini na pia hayazalishi vizuri.


Rais Samia alisema Serikali imeshatoa pesa nyingi na sasa haiwezi kuendelea kutoa pesa kwa taasisi ambazo hazizalishi. 


Aliwatahadharisha Wenyeviti wa Bodi kuwa hatasita kuwafikisha katika mamlaka za sheria wenyeviti wanaoshindwa kuwajibika huku akieleza kuwa Wakuu wa Taasisi zitakazoshindwa kufanya vyema pia wataondolewa.


Taasisi za Umma zimechangia zaidi ya Sh trilioni 1 katika mfuko mkuu wa serikali na Rais Samia anaamini Taasisi hizo zinaweza kuchangia zaidi.

Naye msajili  wa hazina ,Nehamiah Mchechu aliswma jumla ya kampuni 28 za serikali likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yatakuwa huru wiki hii.


Taasisi hizo ambazo majina yake yote hayajawekwa hadharani ni pamoja na Vyuo 13 vya Elimu ya Juu vya Umma. Mchechu alisema maendeleo hayo mapya ni matokeo ya mabadiliko yanayoendelea katika taasisi za umma nchini kote.


“Tumefikia muafaka na Wenyeviti na Wakurugenzi wa taasisi hizi. Tunataka kuona makampuni mengi yanafanya kazi kwa uhuru,” alisema.


Mchechu aliendelea kubainisha kuwa baadhi ya taasisi hata hivyo zimeomba kuongezewa muda wa hadi miaka miwili ili kuwa huru kikamilifu.


Ends....

Post a Comment

0 Comments