PROF MKENDA AVUTIWA NA KITUO CHA UMAHIRI KATIKA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA,ATAKA VIJANA WAKACHUKUE UJUZI

Na Joseph Ngilisho Arusha 

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda ameahidi kuimarisha ubunifu wa  Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Umoja wa Wakandarasi wazawa Tanzania (ACCT) kwa kuanzisha kituo cha mafunzo ya umahiri kwa ajili ya kuendeleza vijana kiufundi ili kuwaimarisha katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.


Aidha amekitaka chuo cha Ufundi Arusha kuongeza mashirikiano na kampuni mbalimbali za magari duniani ili kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa hapo ili waweze kupata ujuzi na kutengeneza magari ya kisasa na mitambo mikubwa hapa nchini.

Prof.Mkenda ameyasema hayo wakati  alipotembelea Chuo hicho na kujionea kazi wanazofanya chuoni hapo ikiwemo kituo hicho na kusema kwamba ni ndoto ya serikali kukuza ujuzi kwa vitendo.

“Kinachofanyika hapa ndio ndoto ya serikali na hata ukikumbuka ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan alisema tutaimarisha ubora wa elimu yetu na kuongeza ujuzi wa wahitimu katika taasisi zetu za elimu, kinachofanyika hapa ni kujenga mahusiano makubwa Zaidi kati ya kinachofundishwa humu na kinachohitajika sokoni” alisema Prof. Mkenda.

Aidha Prof. Mkenda aliahidi serikali kurudisha mahusiano yaliyokuwepo baina ya kituo hicho na Wakufunzi wastaafu kutoka Uholanzi (PUM) ili waendelee kuleta wakufunzi wao kwenye kituo hicho na pia wakufunzi wetu wa ndani wapate fursa ya kwenda kuona kinachofanyika Uholanzi.

"Kwa upande wa chuo hiki sipendi kuwakoromea ila narudia kwa mara ya mwisho,napenda chuo kiongeze mashirikiano na kampuni mbalimbali za magari kama Toyota,Nissan,Kia ili kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa hapa waweze kumudu magari ya kisasa"


Awali aliyekuwa mkuu wa chuo hicho ambaye ni mwanzilishi wa kituo hicho,Mhandisi dkt Richard  Masika,alisema kituo hicho kimeanzishwa kwa msaada wa wakandarasi kwa lengo la kuandaa mafundi ,wataalamu bobezi wakiwemo mafundi mchundo.

Alisema utaratibu wa kujiunga katika kituo hiki ni wakandarasi kuleta mafundi wao kwa ajili ya kuongezewa ujuzi na mafundi wengine wa kujitengemea wanaohitaji kujifunza Teknolojia  mbalimbali. 


Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja huo wa Wakandarasi wazawa Tanzania Mhandisi Milton Nyerere alisema , lengo la kituo hicho ilikua ni kuongeza uwezo wa ndani wa Wakandarasi wazawa.

“Lengo la kituo hiki ni kuongeza uwezo wa wakandarasi wazawa na kuondoa ile dhana kuwa wandarasi wazalendo wanafanya kazi mbaya, sasa tumeboresha uwezo wetu kwa kuongeza ujuzi kwa mafundi wetu ili tukienda kwenye ushindani wa soko tatizo la ubovu wa kazi tuwe tumeliondoa” alieleza Mhandisi Nyerere.










Kituo hicho cha Mafunzo cha Umoja wa Wakandarasi wazawa Tanzania ACCT kilianzishwa mwaka 2015 na kipindi chote kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi ya ujenzi kwenye fani za upigaji plasta, uwekaji wa marumaru, kupaka rangi pamoja na kupamba kuta na kwamba hadi sasa wanafunzi zaidi ya 300 wamefuzu mafunzo hayo.


Ends..


Post a Comment

0 Comments