By Ngilisho TV
Shahidi kesi ya mauaji ya inayomkabili mjane wa Bilionea Msuya, awasilishe mahakamani kisu kinachodaiwa kufanya mauaji, nguo ya ndani ya marehemu na filimbi.Aelezea uchunguzi aliuoufanya kuhusu uhusiano wa vinasaba katika vielelezo hivyo.
Pia Mahakama imeipokea nguo ya ndani (chupi) inayodaiwa kuwa ndiyo aliyokuwa ameivaa marehemu Aneth ambayo inadaiwa alivuliwa kwa nguvu wakati wa tukio la mauaji hayo, pamoja na filimbi ambayo pia Inadaiwa alikuwa akiitumia marehemu Aneth.
Vifaaa hivyo vimewasilishwa mahakamani hapo na shahidi wa 15 wa upande wa mashtaka Mkemia Dk. Fidelis Segumba, ambaye ni Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai Kemia katika Ofisi ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wakati akitoa ushahidi wake leo Jumanne Agosti 15,2023.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni mjane wa Bilionea Msuya; Miriam Steven Mrita, ambaye anatuhumiwa kumuua wifi yake, Aneth, akidaiwa kushirikiana mshtakiwa mwenzake, mfanyabiashara, Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray.
Aneth aliuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, miaka mitatu tangu kuuawa kwa kaka yake, Bilionea Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.
Kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018 inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake akiongozwa na Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri,Dk. Segumba ameieza Mahakama kuwa ndiye aliyefanya uchunguzi wa vinasaba katika vifaa hivyo vinavyodaiwa kuhusiana na tukio la mauaji hayo.
Ameeleza kuwa Agosti 30, 2016 wakati huo akiwa meneja wa Maabara ya uchunguzi wa Sayansi Baiolojia na Vinasaba, alipokea vielelezo hivyo kutoka vilivyoambatana na barua ya maombi ya kufanya uchunguzi wa vielelezo hivyo kutoka Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi ya Jeshi la PolisiTemeke.
Amevitaja vielelezo hivyo kuwa ni kisu chembamba chenye mpini mweusi kinadhaniwa kutumika kumchinjia Aneth, chupi ya rangi ya zambarau inayodhamiwa alikuwa ameivaa marehemu Aneth aliyovuliwa kwa nguvu.
Vielelezo vingine amevitaja kuwa vilikuwa ni filimbi ya chuma yenye rangi ya fedha inayodhaniwa kuwa alikuwa akiitumia marehemu Aneth na mpanguso wa ndani ya mashavu ya mshtakiwa wa pili, Muyella.
Ameeleza kuwa baada ya kuvihakiki alivisajili vielelezo hivyo kwa kuvipa namba za herufi ambapo Kisu alikipa namba A, chupi akaipa namba B, filimbi akaipa namba C na mpanguso wa shavuni kwa mshtakiwa Muyella akaupa namba D.
Alibainisha kuwa vielelezo hivyo kwa mujibu wa barua hiuo vilikuwa vinahitaji kufanyiwa uchunguzi kuona mahusiano ya vinasaba katika vielelezo hivyo,hivyo akifanya uchunguzi Kwa kufuata hatua zotena alipomaliza aliandika ripoti ya matokeo ya uchunguzi wake.
"Baada ya kupata tafsiri ya matokeo ya uchunguzi niliandika ripoti ya matokeo ya uchunguzi. Niliandaa Machi 15, 2017", alieleza shahidi huyo na kubainisha kuwa alivifunga tena vielelezo hivyo kisha akavikabidhi kwa Kamisheni hiyo ya Polisi iliyoomba uchunguzi huo.
Baada ya maelezo hayo, shahidi huyo ameongozwa na mwendesha mashtaka kuvitambua, kisha akaiomba mahakama ivipokea vielelezo hivyo, kisu, chupi, pamoja na taarifa yake ya uchunguzi kuwa sehemu ya vielelezo vya upande wa mashtaka.
Upande wa utetezi unaongozwa na Wakili Peter Kibatala haukuwa na pingamizi,hivyo Mahakama ikabipokea na kusajiliwa kama vielelezo vya upande wa mashtaka.
Baada ya vielelezo hivyo kupokewa mahakamani shahidi huyo akiongozwa na mwendesha mashtaka ameisima kwa sauti ripoti ya uchunguzi wake huo kisha akiongozwa na mwendesha mashtaka alitoa ufafanuzi wa matokeo ya uchunguzi wake huo.
Akisoma ripoti hiyo alieleza kuwa uchunguzi uneonesha kuwa kisu, chupi na filimbi vilikuwa na damu ya binadamu.
Akitoa ufafanuzi wa hitimisho la ripoti yake hiyo,shahidi huyo ameema kuwa Vinasaba katika kielelezo B (chupi ya marehemu Aneth) hakina uhusiano na kielelezo D( mpanguso wa shavuni kwa mshtakiwa Muyella).
Pia amesema kuwa vinasaba kutoka kielelezo C (Filimbi) vina uhusiano na kielelezo D (mpanguso wa shabuni kwa mshtakiwa Muyella) na kwamba vinasaba toka kielelezo A (kisu) bunanuhhsiano na vya kielelezo B yaani chupi ya marehemu Aneth.
Baada kuhitimisha ushahidi wake huo wa msingi Wakili Kibatala alipomhoji maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake pamoja na mambo menhine kuhusiana na damu hiyo iliyokuwa kwenye kisu,chupi na filimbi kuwa ilikuwa ni ya nani, maswali ambayo hakuweza kuyatolea ufafanuzi Kwa uhakika.
Sehemu ya mahojiano baina ya Wakili Kibatala na shahidi huyo ilikuwa kama.ifuatavyo
Kibatala: Shahidi hii barua ( ya maombi ya uchunguzi ya Agosti 29, 2016 kutoka Polisi Temeke) wewe binafsi uliiona na ulishughulika nayo?
Shahidi: Niliiona na nilishughulika nayo.
Kibatala:Kwa nini umeona umuhimu wa kuitaja katika ripoti yako?
Shahidi: Nimeitaja kwa sababu niliipokea.
Kibatala: Wakati unatoa ushahidi wako umeionesha hapa mahakamani?
Shahidi: Sikuonesha.
Kibatala: Pia umetaja polisi fomu namba 180 ya Agosti 28, 2016, mwa nini uliona umuhimu kuitaja kwenye ripoti yako?
Shahidi: Nimeitaja kwa sababu ni viambatanisho( vya barua ya maombi ya uchunguzi wa vielelezo) nilivyopokea.
Kibatala: Kwa ufahamu wako Kwa nini ilikuwa ni muhimu hiyo fomu ije kwako kwa nini asingeleta sampuli tu?
Shahidi: Nashindwa kujibu kwa sababu hiyo ni sababu yake.
Kibatala: Kwa hiyo ni sahihi wewe haufahamu madhumuni ya hii fomu katika mchakato wa collection of samples?
Shahidi: Nafahamu
Kibatala: Umuhimu wake ni nini?
Shahidi: Ni mojawapo ya fomu inayotumika kuonesha aina ya vielelezo.
Kibatala: Ambayo hukuwahi kuionesha hapa mahakamani japo ulishughulika nayo?
Shahidi: Hapana sijaionesha
Kibatala: Hii barua ya Agosti 30, 2016 ( Polisi kuomba kufanyiwa uchunguzi wa vielelezo hivyo takwa) ina umuhimu gani kisheria?
Shahidi: Hiyo ni barua ambayo imeomba kufanyika uchunguzi wa vielelezo.
Kibatala: Ni sahihi requesting letter ndio inakuwa imeonesha aina ya sampuli ambazo zimeletwa na terms of reference?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Kwa hiyo ni sahihi kwamba hata ripoti yako ilipaswa kuji-confine kwenye terms of references?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Na ndio ilipaswa hata kutaja majina ya watuhumiwa?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Kwa Umuhimu huo wa barua hiyo umeitoa hapa mahakamani?
Shahidi: Hapana
Kibatala: Ulitoa ufafanuzi kwa mahakama where about?
Shahidi: Sikuzungumzia hiyo.
Kibatala: Lakini ni wewe binafsi uliyepokea hiyo barua na kushughulika nayo?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Unakubaliana na mimi wewe kama msomi mzuri eneo la DNA ni eneo muhimu sana, yaani namna gani sampuli zinatoka na kuhifadhiwa?
Shahidi: Ni kweli
Kibatala: Shahidi, katika hii ripoti mara kadhaa umezungumziwa chupi ambayo ilivuliwa kwa nguvu (kutoka kwa marehemu Aneth) haya maneno uliyatoa wapi kwamba hii chupi ilivuliwa kwa nguvu?
Shahidi: Nyaraka iliyowasilishwa(barua ya Polisi kuomba uchunguzi) ndio ilivyoelezwa hayo maelezo
Kibatala: Kwa hiyo unazungumzia hi requesting letter?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Ambayo tumekubaliana wewe hujaitoa wala kuielezea?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Ni sahihi kwamba Kanuni ( Uchunguzi wa Vinasaba) inaeleza kwamba sampuli zinapopokelewa zinasajiliwa kwenye register?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Ni sahihi register hii ni mojawapo ya mchakato wa kumanage mchakato huu au ni pambo tu?
Shahidi: Siyo pambo
Kibatala: Register ina- record nini nini?
Shahidi: Register inarekodi tarehe aina ya vielelezo na maombi ya uchunguzi
Kibatala: Nani aliyeijaza siku hizi sampuli zinapokelewa?
Shahidi: Mimi ninayepokea ndiye ninajaza kwa kuvipa namba
Kibatala: Mwambie Mheshimiwa Jaji iwapo ripoti yako inaambatana na hiyo register
Shahidi: Haipo
Kibatala: Mwambie Mheshimiwa Jaji labda kama uliitoa kama kielelezo kingine?
Shahidi: Haipo
Kibatala: Ulitoa ufafanuzi kwamba sijaitoa kwa sababu yoyote ile?
Shahidi: Sijaitoa (ufafanuzi) wa sababu sijaizungumzia.
Kibatala: Shahidi ni kweli kwamba DNA sample ziko substantive na contamination (zina uwezekano wa kuathiriwa kwa kuguswaguswa) na ndio maana wewe hata kabla ya kuzifungua ulivaa glove?
Shahidi: Ni kweli
Kibatala: Ni kweli kwamba wewe huna utaalamu wa kujua kama.kabla ya kuletwa kwako zilikuwa contaminated?
Shahidi: Ni kweli
Kibatala: Kwa mujibu wa hizi nyaraka (barua kutoka polisi na viambatanisho vyake) vielelezo hivi vilishaanza kufanyiwa kazi mahali fulani hata kabla ya kufika kwako?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Kwa kuangalia requesting letter, kisu, chupi na filimbi ulifahamu kuwa vilichukuliwa mahali fulani?
Shahidi: Sikufahamu
Kibatala: Sasa shahidi, katika ripoti ya uchunguzi wako kuna mahali umesema kuwa uchunguzi wa awali ulidhihirisha kuwa kielelezo A kisu kinachodhaniwa kukata shingo ya Aneth ina damu ya binadamu, hii taarifa uliipata wapi?
Shahidi: Hayo maelezo yameandikwa kwenye hiyo barua mimi siwezi kujua.
Kibatala: Kuwa uchunguzi wa awali imeonesha kielelezo A kina damu ya binadamu Jaji akisoma wapi ataona kuwa hii damu ni ya nani?
Shahidi: Damu ni ya kielelezo
Kibatala: Damu ni ya kielelezo?
Shahidi: Ndio
Kibatala: Ahaa
Kibatala: Kuna namna yoyote Kwa kusoma ripoti hii katika kielelezo chochote ( kisu, chupi na filimbi) kuna damu ya marehemu Aneth Msuya?
Shahidi: Siwezi kusema hivyo
Kibatala: Kwa hiyo hakuna uwezekano?
Shahidi: Siwezi ku-conclude mimi nilifanya uchunguzi wa kile kielelezo nilicholetewa.
Kibatala: Lakini damu ni ya nani huwezi kusema?
Shahidi: Kielelezo hakusema hivyo.
Kibatala: Kielelezo B (chupi ya rangi ya zambarau) pia umesema uchunguzi wa awali ulionesha ilikuwa na damu ya binadamu, nitakuwa sahihi nikisema nikisoma ripoti yako siwezi kujua ni damu ya binadamu gani?
Shahidi: Ni damu iliyokuwa kwenye kielelezo.
Kibatala: Ni kweli hii ripoti nikiisoma mwanzo mpaka mwisho hakuna mahali ambako naweza kupata kwamba ni damu ya Aneth Msuya au ni ya nani?
Shahidi: Hilo swali mpaka nifikiri.
Kibatala: Mimi sitaki ufikiri, nataka ujibu kulingana na ripoti hii.
Shahidi: Damu hii ni ya chupi inayodhainiwa kuwa alikuwa ameivaa marehemu Aneth Msuya.
Kibatala: Item B ya ripoti yako umesema chupi ya rangi ya zambarau inayodhamiwa kuwa ndiyo alikuwa amevaa marehemu Aneth Msuya na kuvuliwa kwa nguvu, mpangilio wa vinasaba umedhihirisha ni ya mmiliki zaidi ya mmoja wa kike na wa kiume. Unafahamu identity (utambulisho) za hawa watu wa kike na wa kiume?
Shahidi: Siwafahamu. Hiyo ni description (maelezo) ya kielelezo
0 Comments