CHUO Cha Ufundi Arusha (ATC) kimebuni teknolojia mpya ya kutengeneza pikipiki inayotumia nishati ya jua na umeme waTanesco yenye uwezo wa kutembea umbali wa kilometa zaidi ya 100 bila kuchaji na kuwa chuo cha kwanza hapa nchini.
Akizungumza wakati akifungua kongamano la kimataifa la siku nne linalofanyika chuoni hapo,Kamishna wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt,Lybwene Mtahabwa alikipongeza chuo hicho kuwa na teknolojia nyingi ambazo ni mkombozi hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia ya nchi na kuelekea uchumi wa viwanda.
"Nimejifunza mambo mengi yanayoendelea hasa teknolojia ya utengenezaji pikipiki isiyo na sauti wala kutumia mafuta ambayo kwa sasa yanagharama kubwa,mtu akiwa nayo anachaji tu kwa dakika 20 unaenda Km 100 kwa siku huu ubunifu mzuri na mkubwa na wakwanza katika nchi zetu za Afrika Mashariki ,"alisema.
Alisema pikipiki hiyo mkombozi hata kwa vijana waendesha pikipiki kuzitumia katika biashara zao za kusafirisha abiria na mizigo, bila kutumia gharama kubwa na zitasaidia kuepusha uchafuzi wa mazingira.
Aidha alisema ATC imebuni teknolojia ya kutumia maji ya ardhini na juu ya ardhi kumwagilia mashamba na bustani ili kuwezesha mkulima kupata mazao yenye tija na kuondokana na utegemezi wa mvua ambazo zimekuwa za mashaka kwa sasa.
"Mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha kutokua na mvua za uhakika na kwa teknolojia hii, itatuwezesha nchi yetu kuwa na kilimo chenye uhakika na kuleta chachu kwa viwanda na maendeleo zaidi,"alisema.
Aidha alisema kupitia ubunifu na ugunduzi wa chuo hicho, kuna teknolojia nzuri na rahisi za kuwawezesha wakulima nchini kujikomboa na kuondokana na utegemezi wa neema ya mvua.
Alishauri teknolojia ya kutumia maji ya ardhini na juu ya ardhi kusambazwa nchini ili ilete mageuzi makubwa katika kilimo.
"Lakini nashauri tuanze kujenga Shauku kwa watoto wetu wenye umri wa miaka nane, waanze kujifunza masomo kuhusu teknolojia mbalimbali tutaona matokeo mazuri, sababu hata ukitaka fundisha uchawi au utaalamu wowote umri huu ndio mzuri,"alisema.
Alisema Tanzania kwa sasa kwa ubunifu huo ipo katika njia nzuri na sahihi kuelekea mapinduzi ya kweli katika uchumi wa viwanda.
Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha ATC, Dkt.Musa Chacha alisema chuo kimefanikiwa kubuni teknolojia hizo kutokana na ushirikiano wa chuo hicho na vyuo viwili vya nchini Korea Kusini ambavyo ni Hanyang' na Seoul.
"Mashirikiano haya ni ya miaka saba na ya maeneo ya miradi ya elimu na nishati mbadala ili kusaidia maeneo ya vijijini,"alisema.
Naye mwakilishi wa Chuo cha Seoul nchini Korea, Prof.Sung-Hoon alisema wanajivunia ushirikiano huo ambao sasa ni miaka mitatu imepita na tayari matunda yameanza onekana katika kuwezesha vijana kubuni teknolojia zenye ufumbuzi wa matatizo mbalimbali katika jamii.
"Kama ubunifu huu wa utengenezaji pikipiki inayotumia nishati ya jua na haina madhara kwa mazingira ya kutoa moshi wala haina sauti, lakini gharama za uendeshaji ndogo, ukilinganisha na zile zinazotumia mafuta,"alisema
Ends...
0 Comments