ALMC SELIAN ,YASHUSHA MADAKTARI BINGWA 60 KUTOKA MAREKANI ,KUTUA NCHINI WIKI HII ,WATAFANYA UPASUAJI WA MIFUPA NA NYONGA BURE,SERIKALI YABARIKI,WAGONJWA 200 WACHANGAMKIA FURSA CHAP

Na Joseph Ngilisho,Arusha


Madaktari Bingwa wapatao 60 wa Mifupa na Nyongo kutoka Los Angelos Jimbo la Califonia Nchini Marekani wanatarajia kutua  Nchini Agosti 10 mwaka huu kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu bure ya upasuaji wa magoti na nyonga.

Madaktari hao watawasili nchini siku hiyo katika uwanja wa ndege majira ya saa 2 usiku na watafanya shughuli za upasuaji kwa wagonjwa 200 ambao tayari wameshajiandikisha  na shughuli hiyo wataifanya kwa wiki moja katika hospital ya rufaa ya Arusha Lutheran Medical Centre ALMC, (Seliani) inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kiluthei Tanzania {KKKT} iliyopo Jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha,Kaimu Mkurugenzi wa Hospital ya Seliani,Dkt Godwil Kivuyo alisema kuwa ujio wa madaktari hao ni fursa kubwa kwa hospital hiyo na unaweza kusaidia wananchi wengi wenye changamoto ya magonjwa ya magoti na nyonga.

Dkt Kivuyo alisema mbali ya kufanya huduma hiyo ya upasuaji bure kwa wakazi wa Jiji la Arusha na nje ya Jiji hilo kwa magoti na nyonga kwa wiki mbili kwa saa ishirini na nne pia watakuwa wakitoa mafuzo kwa madaktari bingwa wa hospital ya Selian katika huduma za upasuaji.
Alisema ujio wa madaktari hao ni fursa kwa hospital ya Seliani na serikali pia ni faraja kwa wagonjwa wa Mifupa na Nyonga kwa Nchini kwa ujumla na kusema kuwa amewashukuru wale wote waliofanikisha hilo kwani watakuwa wamewaokoa wagonjwa wengi waliokuwa na magonjwa ya mifupa,magoti na nyonga kuepusha gharama kubwa za matibabu zinazofikia takribani elfu 60 hadi 80.

Mkurugenzi Kivuyo alisema kuwa wagonjwa watakaopata huduma ya upasuaji wa magoti na nyonga kwa madaktari hao Bingwa kutoka Marekani ni wale tu wenye uwezo wa hali ya chini kwani ndio walengwa wakubwa.

‘’Ujio wa Madaktari Bingwa wa Mifupa kutoka Nchini Marekani ni fursa kwa Hospital  na pia ni neema kwa watanzania wenye kukabiliwa na magonjwa hayo’’alisema Kivuyo

Naye Lazaro Nyalandu Mdau wa Afya wa hospitali hiyo , alisema kuwa vifaa vyote vya upasuaji,madawa na vitendea kazi vyote serikali imeruhusu kuingia nchini bila kulipia kodi kwani vikishatumika au kubaki vitakuwa mali ya hospital hiyo.

Nyalandu alisema kuwa gharama ya matibabu kwa mgonjwa mmoja aliyefanyiwa upasuaji na madaktari hao ni zaidi ya dola 30,000 hivyo utaona jinsi gani raia hao wa Kimarekani walivyojitoa kwa ajili ya watanzania.

Alisema mbali ya kufanya upasuaji pia watakuwa wakifanya somo darasa kwa madaktari wa Hospital ya Seliani ili kupata uelewa zaidi ya upasuaji wa magoti na nyonga na hiyo ni fursa kwa madaktari wa kitanzania waliopo katika hospitali hiyo iliyopo Jijini Arusha.

Nyalandu aliishukuru sana serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano waliouonyesha kwa kanisa la KKKT na uamuzi wa kuruhusu vifaa tiba kuingia Nchini bila ya kulipia kodi kwani jambo hilo linapaswa kupongezwa sana na kusema kuwa wao watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma ya upasuaji inawafikia walengwa waliokusudiwa na sio vinginevyo.

Alisema na kuwaomba wadau wengi wa afya kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanawaleta Madaktari wengine bingwa kutoka nje lengo ni kutaka kuwasaidiaa watanzania wenye changamoto za magonjwa mbalimbali kwa kufanya hivyo ni kupata Baraka kwa Mwenye Mungu.

Ends..

  

Post a Comment

0 Comments