Na Joseph Ngilisho Arusha
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kwamba takribani watu 132 ,000 hapa nchini, wanaambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu kila mwaka, huku watu 25,800 wakiripotiwa kufa sawa na wastani wa watu 70 wanaopoteza maisha kila siku.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa makatibu wakuu na waratibu wa mipango ya nchi ya kupambana na kifua kikuu kutoka nchi 11 za Afrika .
Ummy alisema kuwa, lengo la mkutano huo ni kujadili jinsi gani nchi za Afrika zinaweza kuja na ubunifu na mikakati mipya ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu Afrika na duniani kwani takwimu za kidunia zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 10.5 wanaambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu kila mwaka.
Alisema kuwa, kati ya hao takribani watu milioni 1.6 wanafariki kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu kwa mwaka huku serikali ikiendelea mahitaji ya vifaa na matibabu bure sanjari na kufanikiwa kuweza kugundua TB sugu.
"Tulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19 na hatukuwahi kufikia vifo hivi, lakini TB ni kama ugonjwa wa maskini haujapata sauti au mwitikio kutoka kwa viongozi na jamii namna ya kuutokomeza."alisema.
Alisema ,serikali kwa kushirikiana na mfuko wa dunia wa kupambana na kifua kikuu ukimwi na malaria (Global Fund) wameweza kukutana ili kuona jinsi gani ya kufikia malengo ya kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.
"Sisi kama Tanzania tunaona hili linawezekana mwaka 2015 tulikuwa tunaibua wagonjwa wa kifua kikuu kwa asilimia 39 lakini tuliongeza jitihada hadi kufikia asilimia 65 kwa kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii."
Alisema wizara yake ina mkakati wa kuwekeza kwa jamii sanjari na kutoa mafunzo ya miezi mitatu kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 5,000 kila mwaka na kuyatumia maduka ya dawa baridi na waganga wa tiba asili katika mapambano ya TB hala nchini.
Awali mkuu wa kifua kikuu kwenye mpango wa dunia wa TB na Malaria kutoka Global Fund, dkt.Elihud Wandwalo alisema kwamba mfuko huo unasaidia zaidi ya nchi 100 Kote ulimwenguni ikiwemo Tanzania.
Alisema ugonjwa wa kifua kikuu unauwa watu wengi zaidi duniani hasa nchi maskini ambazo zina watu wengi, hivyo mkutano huu wameuleta hapa nchini kwani imeonyesha Tanzania ni kinara wa maambukizi ya TB
Alisema kwamba shirika lao limekuwa likitoa Takribani dola milion 800 kwa mwaka katika mapambano ya kifua kikuu Malaria pamoja na Ukimwi ambapo Takribani dola bilion 4 kwa bara la Afrika.
Alisema nchi ya India ndio yenye maambukizi makubwa ya TB duniani, takribani watu milioni 2 kila mwaka wanaugua TB na katika nchi za Afrika nchi ya Nigeria na Afrika kusini ndio zinaongoza ,na nchi zenye maambukizi makubwa duniani ni 30 zikiwemo 17 kutoka Afrika.
Ends...
0 Comments