RAIS MWINYI ,SAMIA KUTUA TENA ARUSHA,KUHUSIKA MKUTANO WA KIMATAIFA WA TAKUKURU


 

Na Joseph Ngilisho, Arusha 


RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk,Hussein Ali Mwinyi anatarajia kuzindua maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Rushwa Barani Afrika ambayo yatafanyika mkoani Arusha kuanzia Julai 9 hadi 11 mwaka huu.


Aidha siku ya kilele Julai 11 mwaka huu maadhimisho hayo yatafungwa na Rais Samia  Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 



Akizungumza jana jijini Arusha  na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella alisema siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika,huadhimishwa  Julai 11 kila mwaka, na  tangu ilipoadhimishwa mwaka 2017 na mwaka huu Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo.


Alisema lengo la maadhimisho hayo ni kutoa nafasi kwa nchi wanachama kutafakari juhudi za mapambano dhidi ya rushwa na kuchukua hatua stahiki kuboresha na kuimarisha mapambano hayo.


"Julai 9 mwaka huu maadhimisho haya yatazinduliwa na Rais Mwinyi ambaye ni  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuanza na matembezi ya kupinga rushwa ambayo yataanzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha na kuishia Kituo cha mikutano cha kimataifa Arusha (AICC),".


Alisema Rais Mwinyi katika matembezi hayo ataambatana na mawaziri ,mashirika mbalimbali na watu mbalimbali wa ndani,na nje ya Bara la Afrika.


"Nawaomba wananchi wangu mtoe ushirikiano wa kupokea viongozi hawa kama ilivyo desturi yetu na tuonyeshe ukarimu wetu,".


Rc Mongella alisema sanjari na maadhimisho hayo barani Afrika katika mwaka huu, pia wanaadhimisha miaka 20 ya utekelezaji wa mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (AUCPCC) uliosainiwa mwaka 2003.


Mongella alisema maadhimisho hayo wanatarajia wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania watashiriki wakiwemo viongozi na watumishi wa Taasisi za Serikali, mashirika ya umma pamoja na wakuu wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa za Afrika.


Wengine watakaohudhuria maadhimisho hayo ni wanasiasa,wawakilishi wa mabalozi wawakilishi wa Taasisi binafsi, Viongozi wa dini,vyombo vya habari,wajumbe wa AUABC na watumishi wa sekretarieti ya bodi hiyo.


Aliwasihi wananchi kujitokeza kushiriki matembezi hayo na wageni mbalimbali watakaokuwepo wa ndani na nje ya Bara la Afrika .



Mwisho

Post a Comment

0 Comments