MWENYEKITI CCM AWAMWAGIA MAMILIONI WALIMU WA SEKONDARI WAKANYWE SODA

 Na Joseph Ngilisho Arusha 

MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria  Laizer amewapongeza walimu wa shule ya sekondari Naisinyai kwa kuwapatia zawadi ya kitita cha shilingi milioni 2 baada ya wanafunzi 33 wa kidato cha sita wa shule hiyo kufaulu mtihani wao na kuchaguliwa kujiunga na  vyuo vikuu. 


Mbali na mwenyekiti huyo, Diwani wa Kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi, naye  aliwakabidhi walimu wa shule hiyo kiasi cha  sh,300,000 ili kumuunga mkono mwenyekiti  wao katika kuwapongeza walimu hao.

Kiria alisema amejitolea Sh, milioni 52 kwa walimu hao ili wakanywe soda za pongezi kutokana na ufaulu mzuri wa wanafunzi wa kidato cha sita wa shule hiyo.

"Najua shule ya sekondari Naisinyai imefaulisha vyema wanafunzi wa kidato cha sita, hivyo fedha hizo zitachangia furaha yangu kwa walimu kutokana na ufaulu huo mzuri," alisema Kiria 

Mkuu wa shule ya sekondari Naisinyai, William Ombay alisema wanafunzi 33 wa shule hiyo walifanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita na wote wamefaulu kwenda chuo kikuu.

"Kati ya wanafunzi hao 33, watatu wamepata daraja la kwanza, 27 daraja la pili na watatu daraja la tatu, hivyo hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la nne wala sifuri," amesema mwalimu Ombay.

Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer amewapongeza walimu hao kwani wanafunzi wasingefaulu ingekuwa lawama kwao ila hivi sasa pongezi ni za watu wote.

"Kwenye kufanya vizuri tunakuwa tunapata sifa wote pamoja ndiyo sababu hata mimi nimepongezwa kwenye magurupu ya Whatsapp ila wanafunzi wangefeli ingekuwa aibu yenu walimu," amesema Taiko.

Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Mnyawi amemuunga mkono Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya kwa kuwapongeza walimu hao kwa kuwapatia Sh300,000 kwa kufanikisha ufaulu huo.

"Hii natoa changamoto kwa walimu wa shule yangu ya sekondari Tanzanite iliyopo kata ya Mirerani kuhakikisha wanaendelea kufundisha vyema ili wanafunzi wafaulu nao tuwazawadie," amesema Salome.

Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni amesema wanafunzi hao wamefaulu vyema, ingawa ndiyo mara ya kwanza wanafunzi wa Naisinyai kufanya mtihani wa kidato cha sita.

Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni alisema walimu wanastahili kupongezwa kutokana na matokeo hayo kwani wao ndiyo wanaowafundisha wanafunzi.

Ends..

Post a Comment

0 Comments