Na Joseph Ngilisho ARUSHA
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), anayeshughulikia Afya,Dk.Wilson Mahera,ameagiza timu za uendeshaji wa huduma za afya nchini, kusimamia mfumo mzima wa upatikanaji wa dawa nchi nzima na kudhibiti mianya ya upotevu wa dawa unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio na weledi.
Dkt.Mahera,alitoa agizo hilo, jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya Menejimenti,Uongozi na Utawala yanayolenga kuwajengea uwezo wataalamu wa afya 43 kutoka halmashauri 11 za Mkoa wa Tanga yanayofanyika kwa siku 11 jijini hapa.
Alisema mafunzo hayo pia yanalenga kuzijengea uwezo timu za uendeshaji wa huduma za afya katika ngazi za halmashauri (CHMT) na vituo vya kutolea huduma (HMT) ,kwenye masuala ya uongozi,utawala na usimamizi wa rasilimali na ubora wa huduma ili kuleta tija na ufanisi katika uendeshaji wa vituo vyetu na huduma za afya,ustawi wa jamii na lishe kwa ujumla.
Alisema licha ya serikali kuendelea kuimarisha huduma za kinga,alisisitiza kuimarisha dhana nzima ya ununuzi wa bidhaa za afya kwa kutumia takwimu zilizo sahihi.
Alisema endapo kutabainika kuwapo kwa uzembe katika maeneo ya usimamizi kulingana na uwekezaji serikali itachukua hatua kali kwa wahusika wote.
Alisema upatikanaji wa dawa,vitendanishi na vifaa tiba,kuimarisha hali ya miundombinu ya vituo ,kutaongeza ushiriki wa wananchi kufanya maamuzi na ari ya utendaji kwa watumishi.
“Tuendelee kusimamia ipasavyo mfumo huu ,kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi kwa kuwa itasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji na uwajibikaji katika sekta ya afya".
Alisema serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kupitia dhana ya ugatuaji wa madaraka tangu mwaka 2017 kwa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora na kwa wakati.
Dkt.Mahera,alisema Ofisi ya Rais TAMISEMI,imeandaa na tunawaendelea kutekeleza mpango kazi wa uboreshaji wa huduma wenye maeneo 11 ya kimkakati.
Alisema hadi sasa kuna vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi zaidi ya 7000(vituo vya afya zaidi ya 700, hospitali za wilaya 188 na zaidi ya 5000 ni zahanati).
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha,Mounti Meru,Alex Ernest,alisema serikali katika hospitali hiyo imewekeza katika ujenzi wa miundombinu na kununua vifaa tiba vya kisasa kuhakikisha wanatoa huduma bora.
Alisema hospitali hiyo,ilipatiwa Sh.bilioni 5.4 fedha ambazo walitumia kuboresha miundombinu ya majengo na kununua vifaa tiba.
Awali mratibu wa Mafunzo hayo Vyuo vya Afya, Kanda ya Kaskazini na
mkuu wa Chuo cha Afya cha CEDHA ,Johannes Lukumay
alisema mafunzo hayo wamefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kijerumani (JIZ) nchini Tanzania kwa ajili ya kuwaendeleza kitaaluma ,masuala ya uongozi na utawala watumishi wa sekta ya afya .
Dkt.Lukumay,alisema taasisi hiyo ya serikari,imepewa majukumu ya kuendeleza watumishi wa afya katika kada mbalimbali ambapo serikaki imewekeza katika sekta ya afya ikiwemo kujenga vituo vya afya ili waweze kutoa huduma bora za afya.
Pia alisema taasisi hiyo inajukumu la kuwafundisha wakufunzi wa taaluma za afya ili kuhakikisha wanatoa mafunzo stahiki kwa walengwa,kufanya utafiti wa kutatua changamoto za afya na kutoa mafunzo ya muda mrefu.
Dkt Lukumay aliipongeza serikali kwa kuleta mafunzo hayo katika taasisi ya CEDHA yenye dhamana ya kutoa mafunzo hayo hapa nchini ili kuwajengea uwezo kwa kuwapatia elimu ya utawala na uongozi, kuweza kuelewa majukumu yao.
Ends.
0 Comments