Na Joseph Ngilisho Arusha
Mkuu wa wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa amekitaka chuo cha Maendeleo ya Afya, (CEDHA) kilichopo jijini hapa,kuzifanyia tafiti changamoto zilizoko katika sekta ya afya na kutoa majibu yatakayosaidia kuboresha sekta hiyo katika vituo vya afya na hospitali hatua itakayosaidia kuepusha wananchi kukimbilia huduma kwa waganga wa kienyeji na watabibu wasio na taaluma.
Kauli hiyo ameitoa katika mahafali ya 36 ya chuo hicho ,ambapo wahitimu 30 wa ngazi ya stashahada walihitimu mafunzo ya sayansi ya taarifa ya afya,walimu wa vyuo vya afya na usimamizi wa afya yanayotolewa kwa kozi ndefu na fupi.
Alisema nchi nyingi za Afrika hazina watafiti wa kutosha kutatua changamoto zake badala yake zinategemea watafiti kutoka nchi zingine kuwaletea majibu ya changamoto zao jambo ambalo halina tija kwa maendeleo ya taifa lolote .
"Niombe sana vyuo hivi ambavyo vinashughulika na magonjwa ya binadamu, kuzipatia ufumbuzi changamoto za afya zinazotuzunguka na tusipofanya hivyo tutajikuta tunatupwa nje na sekta yetu itakosa thamani, wananchi watakimbilia kwa waganga wa kienyeji ambao sio wanataaluma"
Aidha aliwataka wahitimu wa Mafunzo hayo kuhakikisha wanabeba dhana nzima ya taaluma ya afya kwa kuyaishi waliofundishwa ili kuvisaidia vituo vya afya na hospitali hapa nchini kutoa huduma bora na yenye tija.
"Matarajio yetu, haya mliofundishwa mkayaishi kwa kutoa huduma nzuri ili mkabadilishe mtazamo kwa baadhi yenu ambao wanaelekea kuichafua taaluma yenu"
Katika hatua nyingine alisema kipindi cha mwaka wa fedha, serikali imefanya maboresho makubwa katika vituo vya afya na zahanati za jiji la Arusha, ikiwemo kuteta vifaa tiba baada ya kutoa kiasi cha zaidi ya sh, bilioni 6 .
Awali mkuu wa chuo cha Cedha,dkt Johannes Lukumay alisema kuwa taasisi hiyo ya Cedha iliyopo chini ya serikali imepewa majukumu makuu manne katika uanzishaji wake ambayo ni kutoa elimu kwa wakufunzi wa vyuo vya taaluma ya afya na kuwaendeleza kitaaluma watumishi wa sekta ya afya waliopo kazini.
Alisema majukumu mengine ni kufanya tafiti zenye kutatua changamoto katika sekta ya afya na kutoa ushauri elekezi kuhusu masuala mbalimbali ya afya hatua ambayo chuo hicho kimefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Alisema tangu kuundwa kwa taasisi hiyo mwaka 1983 imekuwa taasisi ya kipekee na yamfano inayotoa mafunzo ya stashahada ya ualimu wa vyuo vya taaluma za afya nchini Tanzania na visiwani.
Alisema hadi sasa jumla ya wakufunzi wapatao 617 walihitimu mafunzo katika taasisi hiyo wakiwemo kutoka nje za nje kama Uganda ,Kenya ,Ethiopia, Sudan ya Kusini ,Malawi,Namibia na Botswana.
Dkt Lukumay alisema Cedha imepiga hatua kwa kufanya tafiti wa kuwaongezea ufahamu wananchi juu ya masuala ya Ukimwi na afya ya Uzazi na kimeongeza kozi katika nyanja ya tiba ,Kinga na tafiti za afya.
Awali kwa upande wa wahitimu kupitia risala yao iliyosomwa na mhitimu Joseph Komba waliiomba serikali kuangalia namna ya kuingiza kozi ya sayansi ya taarifa ya afya kwenye mfumo wa ajira za serikali ili waweze kupata ajira pindi wanapohitimu.
"Tangu kuanzishwa kwa kada ya sayansi ya taarifa ya afya katika chuo cha Cedha, sisi ni wahitimu wa awamu ya nne na kada hii bado haijaingizwa kwenye mfumo wa ajira za serikali ,ombi letu tunaomba kada hii iingizwe kwenye mfumo wa ajira za serikali"
Ends...
0 Comments