BY NGILISHO TV
CHANZO kifo cha mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, Richard Walalaze (35) anayedaiwa kujiua kwa kujirusha kutoka ghorofani jijini Tanga kimetajwa.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe zinaeleza kuwa mtumishi huyo alijirusha kutoka ghorofa ya pili ya hoteli ya Ocean Breez, jijini hapa usiku wa kuamkia jana. Inaelezwa alikuwa amepanga chumba katika hoteli hiyo tangu Julai 16, mwaka huu.
Mfanyakazi wa hoteli hiyo aliyeomba kutotajwa jina, alisema Richard alipanga chumba namba 124 kilichopo ghorofa ya pili.
Alisema katika ghorofa hiyo, Richard alikuwa jirani na mtumishi mwenzake wa TRA.
Mfanyakazi huyo wa hoteli alieleza kuwa walimtilia shaka Richard kwa kuwa tangu jioni ya siku hiyo alisikika akizungumza kwa sauti kubwa akiwa chumbani kwake akisema anaogopa sana jambo .
“Tulimtilia shaka, alikuwa chumbani kwake anazungumza kwa sauti kubwa akisema anaogopa watu wanamfuata, tukamuomba mwenzake amfuatilie,” alidai mfayakazi huyo.
Alidai mwili wa Richard ulikutwa asubuhi na mfanyakazi aliyekuwa akifanya usafi hotelini hapo ukiwa chini usawa wa dirisha la chumba chake, jambo lililoashiria kuwa alijirusha.
“Tulikuta mwili ukiwa na kovu kichwani na damu nyingi. Alikuwa amevaa fulana na jeans. Mlinzi hakueleza kama alisikia kishindo au la …hata sisi hatuelewi nini kilimtokea,” alisema mtumishi huyo.
Alidai tangu alipowasili hotelini hapo alikuwa akisikitika kwamba hana raha kwa sababu siku chache zilizopita alifiwa na baba yake mzazi na mkewe ambaye ni mjamzito yupo chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Thomas Masese alisema Richard alikuwa miongoni mwa maofisa wa mamlaka hiyo waliokuwa jijini Tanga kwa kazi maalumu. “Tunasubiri vyombo vya dola vinafanya uchunguzi wa chanzo cha kifo chake, lakini Richard ni miongoni mwa wafanyakazi wetu wa TRA kutoka mikoa mbalimbali waliopo jengo la Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kazi maalumu ya kuandaa taarifa," alisema Masese.
Kamanda Mwaibambe alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa baada ya kuukamilisha.
Kwa upande wake, Mchungaji Godfrey Walalaze, ambaye ni kaka wa Richard, alisema taarifa rasmi za mazishi zitatolewa baadaye. Alisema nyumbani kwao ni Kata ya Mlalo, wilayani Lushoto.
0 Comments