Na Joseph Ngilisho Arusha
Askari polisi wa kituo kidogo cha Magereza kilichopo Kisongo jijini Arusha, aliyetambulika kwa jina moja la Eliwaha amemuua kwa kumpiga risasi tatu kijana ,Daud Sindio mkazi wa Oloresho,Olasiti wakati kijana huyo akijaribu kumsihi askari huyo kuwaachia mifugo aliokuwa amewakamata.
Kwa mujibu wa diwani wa kata ya Olasiti, Alex Martin, tukio hilo limetokea jana majira ya saa 7 mchana maeneo ya uwanja wa ndege Kisongo jijini hapa na kwamba kijana huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa Mount Meru.
Akizungumzia tukio hilo ,diwani Alex Martin alisema kuwa alipata taarifa juu ya tukio hilo na kufika eneo la tukio lakini alikuta damu nyingi zikiwa zimetapakaa na matundu ya risasi kwenye barabara ya lami huku marehemu akiwa hayupo.
"Nilipofika eneo la tukio niliongea na mashuhuda wakiwemo vijana wawili waliokamatiwa vifugo yao ambao walinieleza kuwa mara ya kwanza askari huyo alimpiga marehemu risasi pajani na kuanguka chini na kisha alimsogelea na kumpiga risasi zingine mbili akiwa chini na baadaye alimburuza na kumpakia kwenye aliyokuja nayo na kuondoka naye"
Diwani alidai kuwa baada ya maelezo ya mashuhuda hao aliamua kwenda katika hospitali ya mkoa Mount Meru na kumkuta kijana huyo akiwa na hali mbaya lakini baadaye usiku alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.
Akifafanua chanzo cha tukio hilo alidai kuwa askari huyo alifika eneo la tukio baada ya kupata taarifa kwamba kuna mifugo imeingia kwenye eneo lisiloruhusiwa kwa malisho .
Alisema askari huyo aliikamata mifugo hiyo na wachungaji wawili na kuanza kuipeleka kusikojulikana lakini ghafla alitokea marehemu akiwa na pikipiki na alipowaona vijana hao aliwatambua na kuamua kwenda kuongea na askari huyo ili kujua kilichotokea na kumsihi askari huyo awaachie na mifugo yao.
"Lakini askari huyo alionekana kuwa mkali ndipo marehemu alipoamua kuondoka na kwenda kuchukua pikipiki yake ili aendelee na safari yake ,lakini kabla hajafika mbali askari huyo alichomoa silaha yake na kumpiga risasi moja kwenye mguu na kijana kuanguka chini ,baadaye alimsogelea na kumfyatulia risasi zingine mbili eneo la mapajani "
Diwani alisema kuwa askari huyo aliamua kumburuza majeruhi huyo hadi alipokuwa ameacha gari na kumpakia na kuondoka naye na baadaye kumpeleka katika hospitali ya Rufaa Mount Meru ,lakini majira ya usiku alipoteza maisha akiwa anapatiwa matibabu.
Ndugu na jamaa walijikusanya na kwenda ofisi ya mkuu wa wilaya ya Arusha,Felisian Mtehengerwa kulalamikia tukio hilo hata hivyo inadaiwa kuwa askari huyo aliweka panga kwenye gari na kulionesha akidai marehemu alitaka kumkata ndio maana walijihami kwa silaha.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya aliamua kumwita ofisini kwake mkuu wa polisi wa wilaya ya Arusha aliyetajwa kwa jina moja la (OCD) Malema ili kupata ufafanuzi wa tukio hilo.
Inadaiwa kuwa OCD Malema baada ya kufika ofisini kwa DC alikuwa mkali kuliko wafiwa akiwafokea walalamikaji akiwemo diwani kwa kuwaambia sio kazi yao kufuatilia na kuchunguza jambo hilo, hatua iliyomlazimu dc kuwasihi ndugu hao wamwachie jambo hilo aweze kulishughulikia kwa kina.
Diwani huyo pamoja na ndugu wa marehemu walikerwa na kitendo cha kufokewa na OCD na kuamua kupiga simu kwa kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo, ambaye aliwasihi watulie na kumwagiza mkuu wa Upelelezi wa mkoa RCO kushugulikia jambo hilo.
Hata hivyo diwani huyo alisema kuwa hilo ni tukio la pili kwa askari huyo kufanya uhalifu katika Kata hiyo ya Olasiti kwani huko nyuma alishawahi kumtisha wananchi kwa silaha na wananchi walijikusanya na kutaka kumdhulu lakini diwani huyo aliingilia kati kumnusuru askari hiyo asiuawe.
"Lakini cha kushangaza askari huyo amerudia tena kufanya mauaji katika Kata hiyo hiyo"
Diwani Alex alitoa wito kwa jeshi la polisi kutotumia nguvu na mabavu kwa raia wake pasipo sababu.
Ndugu wa marehemu wamedai kukosa imani na jeshi la polisi kwa kuwa askari aliyetenda unyama huo bado hajakamatwa yupo uraiani anaendelea na shughuli zake na walidai kuwa askari huyo alikuwa na tabia ya kuwatishia kwa silaha wananchi mara kwa mara , jambo ambalo wameiomba serikali iwasaidie ili haki iweze kutendeka.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Jonh Mongela alipohojiwa juu ya tukio hilo alithibitisha kuwa na taarifa hizo na kudai kuwa anafuatilia na atatoa ufafanuzi hapo baadaye .
Kamanda wa polisi mkoa wa Justine Masejo alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hopitali ya Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Ends
0 Comments