WANANCHI MLANGARINI, ARUMERU HAWANA BARABARA TANGIA NCHI IPATE UHURU,WALIA NA VIONGOZI WAO,HAWAJAWAHI KUONA GARI,WAGONJWA ,WAJAWAZITO NA MAITI HUBEBWA KWA MACHELA

                          


Na Joseph Ngilisho,Arusha


Wananchi wa Kitongoji cha Majengo katika Kijiji cha Manyire Kata ya Mlangarini Wilayani Arumeru Mkoani Arusha wamelalamika kutokuwepo kwa barabara za uhakika katika kitongoji hicho tangia kuundwa kwa kijjji hicho mwaka 1977 jambo linalowa lazimu kuwabeba kwenye machela akina mama pindi wanapoenda kujifungua.

Wakiongea na waandishi wa habari waliotembelea kitongoji hicho, wakati wakazi hao wakilazimika  kutumia nguvu zao kutengeneza barabara kwa kufyeka mapori ili waweze kupita ,wamewatupia lawama  viongozi kwa kushindwa kupeleka huduma hiyo toka  mwaka 1977.


Baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho,John Mushi na Rajabu Abdalah walimtupia lawama diwani wa kata hiyo kwa kushindwa kutatua kero hiyo licha ya kutoa ahadi hiyo wakati wa kampeni za uchaguzi na kusisitiza kuwa hawatafanya makosa tena wakati wa uchaguzi. 



Mushi alisema na kuutaka uongozi wa Halmashauri ya na Mkuu wa wilaya ya Arumeru, kuhakikisha wanatembelea vitongiji mbalimbali na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi ili waweze kuzipatia ufumbuzi.

Mbali na changamoto hiyo,Fredrick Kisanga  alisema kuwa katika kitongoji hicho wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme  na kuwataka viongozi kuwajibika katika kazi na sio kukaa ofisini.


Akizungumzia kadhia hiyo mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Majengo ,Hilda Kaaya alisema nyakati za masika watoto wa shule hulazimika kukaa majumbani kwa kuwa hawawezi kwenda shule kwa kuhofia maji yanayojaa kwenye mito iliyozunguka kitongoji hicho.


Kaaya alidai kuwa mwananchi hao pindi anapopata msiba hulazimika  kubeba mwili wa marehemu begani umbali wa zaidi ya km 15 ili aweze kupata usafiri kwenda Hospitali huku akidai kuwa diwani wa kata hiyo ameshindwa kuwajibika.

Kiongozi huyo alimtupia lawama diwani wa kata hiyo,Zabedayo Mollel na kusema kuwa toka alipofika katika vitongoji hicho kipindi cha kuomba kura mwaka 2020 hadi kesho hajawahi kufika pamoja na kupewa taarifa mara kwa mara bila mafanikio.

Alisema kutokana na hali hiyo wameiomba serikali ya wilaya kutupia macho katika kitongoji  hicho ili kiweze kupata huduma hiyo kama vitongoji vingine.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Barabara,Rogers Kisanga  alisema amekuwa akihamashisha watu kujitolea kwa hali na mali kukarabati barabara mara kwa mara lakini imefika mahali wamezidiwa kwa kuwa viongozi wa kata  wamekuwa wazito kutoa ushirikiano.

Kisanga alisema na kuuomba uongozi wa serikali wilaya hususani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha{Arusha Dc} kuhakikisha fedha za Maendeleo ya Kata zinafika katika vitongoji hivyo kwa maslahi ya wote kwani hana imani kama fedha zinafika kwa malengo yaliyokusudiwa.

‘’Tunakuomba Mkurugenzi Arusha DC tumia Mamlaka yako kuhakiki fedha za Maendeleo ya kata kufanya kazi inayokusudiwa kwa kuwa hawaoni kama fedha hizo zinawafikia ‘’alisema Kisanga

Alipotafutwa kwa simu diwani wa kata hito Zabedayo Mollel na kuelezwa tuhuma anazotuhumiwa na wananchi wake hakujibu chochote na alikata simu na baada ya kupigiwa tena alizima simu kabisa na kutopatikana jitihada za kimsaka zinaendelea.

Ends. 

Post a Comment

0 Comments