SHISHA, VISUNGURA VYAANGAMIZA MAISHA YA VIJANA




Uvutaji shisha na matumizi ya pombe kali kwa baadhi ya vijana inaonekana kuwa ndiyo kwenda na wakati katika maisha.



Hata hivyo, mtindo huu wa maisha unaelezwa kuchangia ongezeko la maradhi ya moyo.


Wataalamu wa afya wanasema idadi ya wanaougua shinikizo la damu, kiharusi na maradhi ya moyo katika umri mdogo wa miaka 20 hadi 40 inaongezeka.


“Uvutaji shisha na sigara huongeza mara tatu hatari ya mtu kufa mapema kutokana na ugonjwa wa moyo na kiharusi ikilinganishwa na kutovuta,” alisema Dk Upendra Bhalerao, mapema wiki hii alipotoa mada kwenye mdahalo uliowahusisha madaktari wa Tanzania na India, ulioandaliwa na taasisi ya Medeviva.


Dk Upendra, mbobezi wa upandikizaji moyo na mshauri wa magonjwa hayo kutoka Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India, alisema kwa wavutaji sigara na watumia tumbaku ni rahisi kupata changamoto ya mishipa ya damu inayosababisha mshtuko wa moyo na kiharusi.


Alisema uvutaji sigara huongeza kasi ya kuziba kwa mishipa ya moyo, pia huharibu mishipa mingine ya damu.


“Wakati mishipa inayosambaza damu kwenye mikono na miguu inapoathirika, huathiri pia mzunguko wa damu. Acha kuvuta shisha au sigara,” alisema Dk Upendra.


Alisema vijana walio na shinikizo la damu, unene kupita kiasi na kisukari wana nafasi kubwa ya kupata maradhi hatari hadi utu uzima.


Dk Upendra alisema takriban asilimia 80 ya ugonjwa wa moyo wa mapema unaweza kuzuilika kwa kubadili mtindo wa maisha.


“Matumizi mabaya ya vitu, ikiwamo ulaji na unywaji usiofaa, mfadhaiko wa kisaikolojia, kifedha na maisha yanayohusiana na mtindo wa maisha yanaweza kuongeza nafasi kwa kijana kuchochea magonjwa ya moyo mapema,” alisema Dk Upendra.


Kwa mujibu wa wataalamu, vijana wengi hupata dalili za kuhisi maumivu ya kifua na mwili kutokwa jasho lakini huona ni hali ya kawaida.


Wataalamu wanaotoa tiba Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wanasema wengi hufika hospitalini wakiwa wamepata shambulio la moyo au kiharusi, huku wakitaja chanzo kuwa shinikizo la damu la muda mrefu pasipo kugundulika na kuanza tiba.


Takwimu zilizotolewa Mei 17, mwaka huu na Wizara ya Afya zinaonyesha ugonjwa wa shinikizo la juu la damu umeongezeka kutoka wagonjwa 688,901 mwaka 2017 hadi kufikia 1,345,847 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 95.4 katika kipindi cha miaka mitano.


Takwimu pia zinaonyesha watu watatu hadi wanne kati ya 10 wana shinikizo la juu la damu kwa uchunguzi uliofanywa katika jamii mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Iringa na Dar es Salaam pamoja na Zanzibar.


Kwa wagonjwa wanaotibiwa JKCI ambayo ni hospitali pekee ya moyo nchini, kati ya wagonjwa 83,356 waliotibiwa mwaka 2022, asilimia 66.8 (59,022) walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.


Hii ina maana kwa kila wagonjwa 10, sita wana tatizo la shinikizo la juu la damu au madhara ya ugonjwa huu.


Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo JKCI, ambaye pia ni mkuu wa idara ya utafiti na mafunzo, Dk Pedro Palangyo alisema kati ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi, asilimia 50 wamekuwa wakikutwa na changamoto ya dalili ya shambulio la moyo baada ya kuziba kwa mishipa ya damu kwenye moyo.


Alisema shambulio la moyo (heart attack) husababishwa na kuziba kwa mishipa inayopeleka damu kwenye moyo. Hata hivyo, ugonjwa huo unaweza kusababisha kusimama kwa moyo ‘cardiac arrest.’


Post a Comment

0 Comments