KESI MKE WA BILIONEA MSUYA :SHAHIDI AELEZA JINSI ALIVYOKAMATA GARI LA MKE WA BILIONEA MSUYA LILILOTUMIKA MAUAJI YA WIFI YAKE


BY NGILISHO TV 

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara (RPC) George Katabazi ameeleza jinsi alivyokamata gari la mjane wa  aliyekuwa mfanyabiashara maarufu na tajiri  wa madini Mirerani, mkoani Arusha, Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya,  anayekabiliwa na kesi ya kumuua wifi yake, linalodaiwa kuhusika katika tukio la mauaji.



RPC huyo mwenye cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), alisimulia tukio wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.


Katika kesi hiyo namba namba 103 ya mwaka 2018, mjane huyo wa marehemu Bilionea Msuya, Miriam Mrita anatuhumiwa kumuua wifi yake, Aneth Msuya; yeye na mwenzake, mfanyabiashara Revocatus Muyella,maarufu kama Ray.

Aneth aliuawa kwa kuchinjwa, Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa kama mnyama nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, na mwili wake ukaachwa ukiwa utupu, bila nguo yoyote, ikiwa ni miaka mitatu tangu kuuawa kwa kaka yake, Bilionea Msuya.


Bilionea Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.


Shahidi huyo wa 11 wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo pia amelikabidhi mahakamani gari hilo la kifahari aina ya Range Rover, lenye rangi ya fedha, kuwa kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.


Katika ushahidi wake wakati akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Marietha Maguta alisema:


Mwaka 2016 nilikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) wa Arusha, nikiwa na cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP).


Agosti 5, 2016 asubuhi nikiwa ofisini, nilipigiwa simu na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman.


Kabla hajafika mbali, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alisisimama na kuieleza Mahakama kuwa shahidi huyo alikuwa na karatasi kizimbani hapo ambayo alikuwa akiitumia kuangalia wakati akijibu maswali ya mwendesha mashtaka aliyekuwa akimuongoza kutoa ushahidi wake.


Kibatala: Mheshimiwa Jaji shahidi ana karatasi hapo kizimbani anayoiangalizia.Tunaomba askari ambaye yuko neutral (asiye na upande katika kesi hiyo) akague hapo kama hakuna karatasi. Intern (mfanyakazi mafunzo I) wangu mmoja amemuona na mshtakiwa amemuona, na nimetuma intern wangu mmoja nje ili kujiridhisha. Amekiondoa amekiweka mfukoni.


Huku akionesha kushangaza, ACP Katabazi alikana kuwa na karatasi kizimbani hapo wala kuiweka mfukoni huku naye akitaka wamkague.


Hata hivyo, Jaji Edwin Kakolaki hakutekeleza ombi la Wakili Kibatala pamoja na shahidi mwenyewe kukaguliwa kama alikuwa na hiyo karatasi, badala yake alimuonya tu shahidi huyo kutokufanya rejea yoyote bila ridhaa ya mahakama.


Jaji: Shahidi unaonywa ukiwa kizimbani hupaswi kufanya reference (rejea) bila kibali cha Mahakama.


Hata hivyo baadaye nje ya Mahakama mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Marietha Maguta, aliyekuwa akimuongoza alimtetea akisema kwamba si kweli kuwa shahidi huyo alikuwa na karatasi.


Badala yake alisema kuwa namna alivyokuwa akiongea akiinanisha kichwa chake chini, juu ya meza ya kizimba ndiko kulikomfanya aonekane kuwa alikuwa anasoma kwenye karatasi.


"Hata mimi mwanzoni kwa jinsi alivyokuwa alianza kuongea anaimanisha kichwa chini nilidhani kuwa alikuwa anasoma kwenye karatasi. Hivyo ikanibidi nimchungulie kumchunguza lakini hapakuwa na karatasi yoyote pale, bali ni style (utaratibu) ya kuongea ndivyo alivyo." alisema wakili Maguta.


Baada ya maelekezo hayo ya Jaji shahidi huyo aliendelea na ushahidi wake kuanzia pale alipoishia kabla ya kukatishwa na Wakili Kibatala, kama ifuatavyo:


DCI alinipa majukumu kwamba nikamate mali inayohusiana na kosa la mauaji ambayo ni magari mawili T429BYY, Range Rover rangi la Silver la pili aina ya Ford Ranger T307 CDH, lenye rangi ya bluu, mtuhumiwa Miriam Steven.


Baada ya maelekezo hayo, Agosti 10, 2016, nilibaini mahali magari yalikokuwa na niliondoka kwenda huko eneo la Sakina.


Nilifika kwenye hotel ya mtuhumiwa inaitwa SG na nilionana na meneja wa hotel anaitwa Omari nikamjulisha kuwa kuna mali nimekuja kuzikamata zinazohusiana na kosa la mauaji nililolitaja hapi awali.


Omari alinipa msaada wa kunionesha mahali gari hilo aina ya Range Rover lilipokuwa limeegeshwa.


Tulifanya upekuzi ndani ya gari mbele ya mashahidi huru.Tulikuta hati ya shamba, kiwanja na barua za mauziano ya shamba na barua zinazohusiana na mirathi ya Erasto Msuya.


Tulijaza hati za kukamata mali na nikaingiza  mali hizo gari pamoja na nyaraka ( kwenye hati ya kukamata mali). Niliandika jina langu na nikasaini pamoja na mashahidi huru waliokuwepo na mali hizo yaani gari na nyaraka tulivichukua na kuvipeleka ofisini kwangu.


Tuliendelea kutafuta gari lingine ambalo lilikuwa kwenye gereji ya CMC Motors lakini lilikuwa na hali mbaya hivyo hatukulichukua.


Niliwapa maelekezo askari Ditektiv Konstebo ( DC) Abel na DC Lukas  walipeleke gari hilo  katika kituo cha Polisi Chang'ombe Dar es Salaam kwa ajili ya upelelezi.


Akiongozwa na Wakili  Maguta, aliiomba mahakama nayo ikubali kuzipokea nyaraka hizo zilizokuwa ndani ya gari hiyo kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka baada ya Wakili Kibatala kueleza kuwa upande wa utetezi hawana pingamizi kupokewa nyaraka hizo.


Jaji Kakolaki: Mahakama imepokea hati hii kama Exhibit P6 (kielelezo cha  sita cha upande wa mashtaka).


Alisema kuwa kwa sasa gari hilo liko kituoni Chang'ombe na kwamba akiliona anaweza kulitambua, hivyo mwendesha mashtaka akaiomba Mahakama hiyo ihamie kwa muda huko Chang'ombe Polosi.


Wakili Maguta. Mheshimiwa Jaji kwa kuwa shahidi wetu amesema anaweza kulitambua gari hilo, tunaomba mahakama yako tukufu ihamie katika kituo cha Polisi Chang'ombe ili aweze kulitambua.


Jaji Kakolaki: Mr Kibatala unasemaje kuhusu hilo ombi?


Kibatala: We have no objection Mheshimiwa Jaji.


Jaji Kakolaki. Maombi ya upande wa mashtaka ya kuhamia kituo cha  Polisi Chang'ombe hayakupingwa basi sasa mahakama inahamia kule. Fanyeni utaratibu wa usafiri kwa ajili ya  wazee wa Baraza na washtakiwa na wasikilizaji wengine kama kuna mtu ana usafiri wake basi anaweza kutumia huo.


Basi Mahakama inaahirishwa kwa sasa hadi itakapoendelea hapo baadaye katika eneo la Chang'ombe.


Mawakili walumbana Kwa hoja kuhusu gari hilo.


Baada ya kufika katika kituo cha Polisi Chang'ombe ziliandaliwa meza na viti Kwa ajili ya Jaji na mawakili pamoja na viti vingine kwa ajili ya wasikilizaji wa kesi hiyo na Mahakama ikaendelea nje ya kituo hicho kwenye maegesho ya magari, mbele ya gari moja aina ya Range Rover lenye rangi ya fedha.


Mwendesha mashtaka alimuuliza shahidi huyo tena kama anaweza kulitambua gari la mshtakiwa alilolikamata huko Arusha, na mambo yanayomwezesha kulitambua.


Shahidi: Kama nilivyosema mwanzo ni gari aina ya Range Rover lenye rangi ya fedha na namba za usajili T429 BYY.


Mwendesha mashtaka: Ukiangalia eneo hili hapa kuna magari mengi hebu angaliangalia na uende ulioneshe gari hilo unalolizingumzia.


Shahidi alilisogelea gari lililokuwa mbele ya Mahakama akalikaguakagua kisha akasema:


Gari ndo hili (akiwa ameligusa ). Ingawa halina plate number (kibao cha namba) lakini namba hizo zinaonekana kwenye sight mirror ( kioo cha kumuongoza dereva kuona nyuma).


Mwendesha mashtaka: Ungependa Mahakama ilifanye nini?


Shahidi: Ningependa mahakama ilipokee gari hili liwe kielelezo cha ushahidi.


Mwendesha mashtaka: Mheshimiwa Jaji, kama shahidi wetu alivyoomba kama wenzetu wa utetezi hawana pingamizi.


Jaji Kakolaki alinyanyuka kitini na kulisogelea gari hilo huku akiwaita na mawakili wa pande zote kusogea, akalikagua kagua kisha akarudi kukaa. Kisha Jaji Kakolaki akamuuliza Wakili Kibatala kama ana lolote kuhusiana na ombi la upande wa mashtaka kulipokea gari hilo kuwa kielelezo upande wa mashtaka.


Wakili Kibatala alipinga ombi hilo kwa madai kuwa kupokewa kwa kielelezo hicho ni kinyume cha matakwa ya kisheria.


Naye alisema: Mheshimiwa Jaji katika committal iliyofanyika katika Mahakama ya Kisutu (Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam) mbele ya Mheshimiwa Simba (Hakimu Thomas Simba), Novemba Mosi, 2018, gari aina ya Range Rover namba hizo haikuwahi kuwa listed (kuorodheshwa kama kielelezo) kinyume cha kifungu cha 246 cha CPA (Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai).


Committal Proceedings ni mwenendo wa kuhamisha kesi inayosikilizwa na Mahakama Kuu, kutoka mahakama za chini inakofunguliwa kukamilisha taratibu za awali ikiwemo kukamilisha upelelezi, na kwenda Mahakama Kuu ambayo ndio ina mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi husika.



Wakili Kibatala aliendelea kusema:


Kuna nyaraka kadhaa tu ndizo zilikuwa listed na mpaka leo hii shahidi huyo anaomba kutoa gari hili kama kielelezo upande wa mashtaka haujatu-serve notice (haujatupatia taarifa) yoyote ya kuomba kuongeza vielelezo particuly (mahususi) gari hili.


Sasa sheria iko wazi kifungu cha 289 cha CPA, na Mahakama iliashatoa uamuzi kuhusiana na kielelezo ambacho hakikuwa listed kwenye committal.


Alirejea kesi ya Said Shaban Malikita dhidi ya Jamhuri, iliyoamuriwa na Mahakama ya Rufani, Juni mwaka huu akisema;


Mahakama ilishatoa uamuzi wa kielelezo ambacho hakijawa listed.  Katika shauri hili Mahakama ya Rufani ilishatoa masharti ya lazima na msimamo wa kisheria katika kesi hii pale ambapo kielelezo hakijawa listed na upande wa mashtaka haujafile notice mahakamani na kui-serve basi kielelezo hicho hakiwezi kupokelewa mahakamani.


Na uamuzi huu ni mwezi huu wa Sita, wiki mbili tu zilizopita. Hata kama Kuna uamuzi mwingine lakini pale inapotokea uamuzi wa mahakama moja unapopingana basi uamuzi wa mwisho ndio unachukuliwa.




Kwa hiyo tunaomba mahakama yako isipokee kielelezo hiki.


Hata hivyo mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Magutu alipinga hoja hizo, akidai kuwa upande wa mashtaka imekidhi matakwa ya kisheria katika kupokea kielelezo hicho.


Wakili Magutu: Mheshimiwa Jaji kwenye committal tulisema kuna physical exhinits (vielelezo halisi) vitatolewa wakati wa usikilizwaji lakini pia tulifile notice (kuwasilisha mahakamani taarifa) Juni 12, 2023 ya kuongeza exhibit na tulimserve Mr Kibatala.


Kwenye open court tuliomba kumserve Wakili wa utetezi lakini akasema hana objection (pingamizi) na kwamba ata-object (atapinga) pale tu vitakapopokewa mahakamani.


Na kwenye notice hii ya additional exhibit imetaja gari hili. Hivyo tumecomply (tumekidhi) na kifungu cha 289 CPA.


Na kesi ya Said Shaban Malikita dhidi ya Jamhuri CA namba 523 ya mwaka 2020, aliyoitaja Wakili wa utetezi, ambayo iko upande wetu utaona kwamba tumecomply na sect 289.


Wakili wa utetezi ame-quote (amenukuu) sect (kifungu) 246 (2) sasa tunashindwa kuelewa alichoki-submit (toa hoja) kwa sababu sect hiyo inaelezea committal na siyo additional exhibit.


Lakini kama Wakili alimaanisha kifungu cha 289 basi tumekicomlpya na tunaomba pingamizi lake litupiliwe mbali kwa kukosa mashiko ya kisheria.


Wakili Kibatala: Mheshimjwa Jaji hakuna ubishi kielelezo hiki hakikuwa listed wakati wa committal. Nilichoelewa wenzetu wame-rely kwenye notice. Kama walitu-serve is well and good.


Jaji Kakolaki: Mey I want to know whether you were served or not.


Kibalata:We were served.Lakini kuwa served bado mahakama ina mamlaka ya kuichanganua, kama imejengewa msingi?


Misingi ya notice imejengewa kwenye kesi ya Malikita imesema katika kesi hiyo Mahakama ilizingatia kifungu cha 246 (2) ambayo inazungumzia ku-list na 289 inatoa remedy (tiba?.


Wakili Maguta: Mheshimiwa hiyo ni facts (kujenga msingi) ni mpya tunaomba isiingizwe kwenye record (kumbukumbu za mahakama) maana hakukuwa amesema kuwa mahakama ili-rely kwenye kesi ya Malikita na sisi hatutapata nafasi ya kuijibu,  Unless (isipokuwa) kama tutapewa nafasi hiyo, kujibu tena.



Kibatala: No problem watapewa right hiyo (kuijibu).


Maguta: Mheshimiwa lakini hiyo ni abuse of court process (matumizi mabaya ya taratibu za mahakama)


Kibatala: Wakili tulia kwanza basi maana bado mimi nina-submit, haina haja kuwa na hasira.


Jaji: Kuna kingine ambacho kitaendelea hapa?


Kibatala: Mheshimiwa Jaji naomba tu iwe notice (ifahamike) hata na wazee wa Baraza kwamba gari haina registration number.


Jaji: Basi ninaahirisha kwa hapa tunarudi Mahakama Kuu nitatoa uamuzi saa 9.




Uamuzi




Katika uamuzi wake Jaji Kakolaki alitupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi, hivyo akalipokea gari hilo kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka. Katika uamuzi huo Jaji Kakolaki alisema:


Kibatala alisema kupokewa kwa kielelezo hicho kunakiuka kifungu cha 246 (2) CPA kwani katika hatua ya Committal proceedings kielelezo hicho hakikuorodheshwa wala kusomwa.


Pia alisema kuwa upande wa mashtaka hawakutoa notisi kutaka kukiongeza na kwamba shauri la Mahakama ya Rufani (Said Malikita dhidi ya Jamhuri alilorejea Kibatala); kwa sababu ni la hivi karibu bado ndilo linalopaswa kuiongoza Mahakama.


Alisema kuwa hata kama (upande wa mashtaka) walitaja kuwepo physical exhibits lakini hawakuainisha kuwa ni kielelezo gani.


Upande wa mashtaka walikiri kuwa kielelezo hicho hakikutajwa kwenye committal, lakini walisema kuwa walisema kuwa kuna vielelezo halisi watavitoa mahakamani.


Hata hivyo walisema kuwa notice ilitolewa kwa mujibu wa kifungu cha 289 cha  CPA, Juni 12, 2023 na wakawapatia nakala upande mwingine, hivyo walitimiza matakwa ya kisheria na kwamba kesi iliyoletwa na utetezi inawaunga mkono.


Kibatala alikiri kupewa notisi hiyo lakini akaiomba Mahakama iangaliwe kama imekidhi matakwa ya kisheria.


Mahakama hii imepata muda kupitia hoja na kusoma sheria na kesi iliyotajwa imeona kuwa kuna mambo mbayo hayabishwaniwi.


Kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 246 CPA, kielelezo kinachokudiwa kutolewa lazima kiwe kimeorodheshwa na kusomwa katika hatua ya committal na madhumuni ya sheria kuweka sharti hilo ni kufanya washtakiwa kuwa na ufahamu wa kile kitakacholetwa mahakamani dhidi yake.


Pia haibishaniwi kuwa pale kitakaposahaulika kuorodheshwa na kusomwa katika hatua ya awali basi mhusika anayekusudia kukileta anapaswa kufuata masharti ya kifungu cha 289 (kuwasilisha notisi ya nyongeza ya kielelezo).


Ubishani uliopo ni kama upande wa mashtaka katika kukitoa kielelezo hicho ambacho ni gari aina ya Range Rover maombi hayo yako sawasawa mbele ya Mahakama au yameletwa kwa mujibu wa sheria.


Kama nilivyoeleza hapo juu kama kumetokea kusahaulikankwa kielelezo husika katika orodha ya vielelezo vinavyokusudiwa njia mbadala ni kupitia kifungu cha 289.


Katika shauri hili hakuna ubishi hata Wakili Kibatala alikubali kuwa notisi hiyo ilitolewa Juni 12, 2023 na kupewa. Kwa hiyo kuna kukidhi matakwa hayo.


Pia Mahakama imeipitia notisi hiyo na kuona kwamba upande wa mashtaka ulitimiza matakwa ya kisheria.


Kwa sababu hizo Mahakama hii inaona kuwa pingamizi hilo hakina mashiko na linatupiliwa mbali na kielelezo hicho kinaweza kupokewa.


Baada ya uamuzi huo, mwendesha mashtaka akimuongoza tena shahidi huyo kuiomba Mahakama hiyo ilipokee kielelezo hicho.


Mwendesha mashtaka: Sasa shahidi kwa kielelezo kile ambacho umekitambua ungependa mahakama hii ikifanyie nini?


Shahidi: Ningependa Mahakama ikipokee.


Jaji Kakolaki: Gari aina ya Range Rover T429 BYY linapokewa na kuwa kielelezo cha saba cha upande wa mashtaka.


Baada ya uamuzi huo Jaji Kakolaki aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, Juni 19,2023 ambapo shahidi huyo ataanza kuhojiwa na upande wa utetezi kuhusiana na ushahidi wake huo.

Post a Comment

0 Comments