Mwathiriwa wa dawa za kulevya mkoa wa Arusha, Judith Uroki ameeleza namna mapenzi yalivyomfanya kuingia kwenye tope la matumizi ya dawa za kulevya aina ya Heroin baada ya mpenzi wake kumshawishi kuvuta sigara bila kujua alikuwa akiichanganya na unga wa dawa za kulevya.
Judith ambaye alijitaja kama MAT namba 1mkoani hapa,ameyasema hayo leo katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya duniani yaliyofanyika jijini Arusha alipokuwa akitoa ushuhuda wa maisha yake mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema wazazi wake walimlea vizuri katika maadili bora, lakini aliingia katika changamoto hiyo pasipo yeye kujua kupitia mwenza wake.
"Nilipohitimu kidato cha nne sikuendelea
nilipata chumba aliyenifanya nikaingia kwenye maharibiko,awali nilipokuwa naye sikujua kama anatumia,baada ya kuingia kwenye mahusiano tukaoana tukawa tunaishi pamoja,alikuwa akivuta sigara na mimi nikawa navuta sigara ,kwenye kuvuta sigara sikuwa najua kama anachanganya"
“Kumbe ile sumu inaniingia taratibu, nilipata msiba Moshi, huko nilikaa siku mbili ghafla nilipata homa kali niliumwa natetemeka nasikia maumivu makali, hali ilikuwa mbaya nilipimwa maradhi yote hayaonekani,” alisimulia.
Alisema siku ya tatu alienda kupima zahanati za huko haina huduma nzuri hiyo akarudi mkoani Arusha na baada ya kurudi nyumbani kwa mumewe na kumweleza hali hiyo akampa avute na baada ya kuvuta dakika tatu alijihisi mzima.
“Mume wangu aliniambia hutakiwi ukae bila kukosa hii kitu, aliniambia ni dawa za kulevya na hapo ndipo nilipojua kumbe nimeingia huko.
“Nilitamani kuacha nilishindwa, baada ya miaka michache hata nyumba za urithi mume wangu alipoteza tukawa hatuna pa kuishi tumedhuulumiwa nyumba sababu ya dawa za kulevya…
“Mume wangu akaenda kuchukua mzigo dar es Salaam yeye akaanza kujificha sababu anauza mimi nikawa natembeza mzigo basi nikawa naongeza dozi zaidi nikaharibika zaidi nimetumia dawa za kulevya miaka 16,” alisema.
Judith alisema alishawahi kuwekwa jela kwa sababu ya dawa za kulevya na huko alikaa miaka minne na alipotoka alipata mimba na akaendelea kutumia dawa za kulevya ambapo alipitia changamoto nyingi kwani alikuwa mwizi na kupitia vipigo akiwa na ujauzito.
Alisema kupitia kituo cha kutoa matibabu ya dawa za kulevya Arusha amefanikiwa kuachana na dawa za kulevya yeye pamoja na mume wake na sasa wana maisha ya furaha na amani.
0 Comments