JAJI AJILIPUA ,APINGA JAJI MKUU KUONGEZEWA MUDA ,ASAMBAZA BARUA HADI KWA RAIS

 


BY NGILISHO TV Dar es Salaam


Sakata la Profesa Ibrahim Juma kuendelea kuhudumu katika nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania limeibua utata baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Stella Mugasha kudaiwa kuandika barua akieleza uamuzi wa kumwongezea muda ni uvunjaji wa Katiba na kutozingatia misingi ya sheria.


Hata hivyo, barua hiyo inayodaiwa kuandikwa na Jaji Stella isiyokuwa na tarehe kwenda kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel na viongozi waandamizi wa Serikali walisema hawajaipata.

Wengine waliotumiwa nakala ya barua hiyo yenye kurasa kumi ambayo jana ilikuwa ikisambaa mitandoni ni Rais Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Jaji wa Rufani, Augustine Mwarija, Jaji Kiongozi, Mustapger Siyani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi na Katibu Mkuu Kiongozi.

Gazeti hili lilimtafuta Jaji Stella kupitia simu yake ya mkononi kujua usahihi wa barua hiyo akasema, “aaah! Sina barua kwenye gazeti.”

Alipoelezwa barua hiyo inasambaa mitandaoni ambayo ameituma kwa mtendaji mkuu wa mahakama alijibu, “hiyo kwenye gazeti hainihusu, mimi nimeipeleka kwa wahusika.”

Profesa Elisante alipoulizwa na Mwananchi kwa ujumbe mfupi wa maneno, kama ameshaipokea barua hiyo iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii na maoni yake kuhusu barua hiyo alijibu hana maoni.

“Sina comments. Nitumie pia hiyo link kwenye mitandao,” alijibu Profesa Elisante kwa ujumbe mfupi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Feleshi ambaye mwandishi wa barua hiyo ameielekeza nakala kwake, alipoulizwa kwa ujumbe mfupi kama alikuwa ameshaipokea kwanza aliuliza Mwananchi ni wapi limeiona barua hiyo

“Niko kwenye kikao. Wewe umeiona wapi,” aliuliza Dk Feleshi.

Lakini alipoelezwa kuwa Mwananchi limeiona kwa mawakili kadhaa wa kujitegemea kupitia mtandao wa WhatsApp, alijibu kwa kwa ujumbe mfupi, “sijapokea.”

Hatua hiyo ya Jaji Stella inakuja siku chache tangu gazeti hili liripoti juu ya nani kumrithi Profesa Juma ambaye muda wake wa kuhudumu ulikoma Julai 15 mwaka huu.

Profesa Juma alizaliwa Juni 15, 1958, Musoma mkoani Mara na Juni 15, 2023 alitimiza miaka 65.

Aliteuliwa katika wadhifa huo Septemba 10, 2017 na aliyekuwa Rais wa wakati huo, John Magufuli, mara baada ya Jaji Mkuu, Mohamed Chande kustaafu.

Msingi wa Jaji Stella kudaiwa kupinga nyongeza ya muda wa Profesa Juma unaakisi Ibara ya 118 (2) ya Katiba ya Tanzania inayoweka ukomo kuwa Jaji mkuu kustaafu atakapotimiza umri wa miaka 65.

Katika barua hiyo, Jaji Stella anadaiwa kuandika kuwa, “Jaji mkuu amenielekeza kukufikishia salamu, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji Kiongozi kwamba, Rais Samia Suluhu Hassan amemuongezea muda (Profesa Juma) aendelee kuhudumu katika nafasi ya Jaji mkuu baada ya muda wake wa kustaafu ambao ni Julai 15, 2023.

“Jaji mkuu anakushukuru sana wewe Jaji wa Mahakama ya rufani na Jaji Kiongozi kwa ushirikiano mkubwa sana mliompatia kwa muda wote ambao amekuwa katika kutumikia Mahakama.”

Barua hiyo iliyoandikwa kwa mtendaji mkuu wa Mahakama, Profesa Ole Gabriel iliendelea kueleza, “aidha, Jaji mkuu anaomba mumfikishie salamu …kwa majaji wa Mahakama ya Rufani na wale wa Mahakama Kuu…”

Jaji Stella katika barua yake hiyo akinukuu andiko lililoonyesha Profesa Juma kuendelea na kibarua chake, alibainisha kwamba andiko hilo halionyeshi muda alioongezewa kiongozi huyo, akisisitiza hata kuongeza muda ni kuvunja sheria.

“Sina ugomvi wowote na Profesa Juma na nimefanya naye kazi kwa uaminifu kwa zaidi ya miaka 10. Kwa kiapo changu cha kazi ya Jaji ninawajibika kulinda na kutetea Katiba ya nchi. Vilevile, kwa mujibu wa Ibara ya 26 (2) ya Katiba, pia mimi kama raia nina wajibu na haki ya kutetea na kuhakikisha Katiba ya Nchi inalindwa ipasavyo,” aliandika.

Hata hivyo, Jaji Stella akinukuu katiba, aliweka bayana Ibara ya 118 (2) inajitegemea na kusimama yenyewe kwenye ukomo uliotajwa hivyo umri wa kustaafu kwa Jaji wa Rufani uliotajwa ndani ya Ibara ya 120 (1) ya Katiba ndicho kitu pekee cha kuangaliwa ili kufahamu umri wa kustaafu Jaji Mkuu ambao ni miaka 65 tu.

Kutokana na Ibara hiyo, nyongeza ya muda kwa Jaji wa Rufani haimhusu Jaji Mkuu asilani.

“Ukomo wa umri wa miaka 65 uliwekwa kwa makusudi ili kuondoa dhana potofu ya uchifu au usultani katika nafasi hiyo. Hivyo kwa kuwa Bunge lilimaanisha kilichomo katika Ibara ya 118 (2) ya Katiba na si vinginevyo, kitendo cha kumuongezea muda Profesa Juma baada ya miaka 65 ni sawa na kuliwekea Bunge mdomoni maneno ambayo halikusema wala kukusudia na ni uvunjaji wa Katiba,” alibainisha.

Post a Comment

0 Comments