BABA ALILIA MAITI YA MWANAYE ALIYECHINJWA KAMA KUKU MERERANI

           


Na Joseph Ngilisho,Arusha


Mkazi wa Sanawari katika jiji la Arusha,Edward Mollel{65} ameliomba jeshi la Polisi Mkoani Arusha kumkabidhi maiti ya mwanaye,Faraja Mollel{8} anayedaiwa kuuawa kwa kuchinjwa kama kuku na watu wanaojulikana na Kisha mwili wake kutelekezwa katika moja ya migodi ya Madini ya Tanzanite,Mererani wilayani Simanjiro Mkoani MANYARA.

 

Mollel alisema waliofanya tukio hilo ambao wote wamekamatwa na Polisi Arusha ni pamoja na Amina Poul maarufu kwa jina la Ester ambaye ni mpangaji wake  katika nyumba anazomiliki eneo la nyumbani kwake Sanawari ,Mganga wa kienyeji mkazi wa Babati aliyemtaja kwa jina la John Mtai na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Ramadhani mkazi wa Mirerani wilayani Simanjro Mkoani Manyara.

 

Alisema watuhumiwa wote wamekamatwa na wako katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha lakini Maiti ya mwanaye Faraja haijulikani ilipo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya kitaalamu na madaktari.

 

Mollel alisema kuna njama kubwa zinafanywa na Mfanyabiashara Maarufu wa Madini na baadhi ya Polisi Arusha kukwepesha kuichukua maiti kwenda hospital kwa ajili ya vipimo na aliyehusika kufanya njama hizo ni mfanyabiashara wa madini ili kurahisisha kesi.

 

Alisema ni muda umepita polisi wameshindwa kuipata maiti ya mwanaye lakini yeye anajua kila kitu kinachoendelea ndani ya jeshi hilo na sasa anataka kumwona Rais Dk Samia Suluhu Hassan ili aweze kumsaidia hata kama angepewa hata kidole angemshuruku Mwenyezi Mungu ili aweze kufanya utaratibu wa mazishi yeye na ndugu zake.

 

Mollel alisema kuwa tukio hilo lilitokea march 16 mwaka huu nyumbani kwake Sanawari baada ya mpangaji wake Amina kumwiba mtoto na kwenda naye eneo la Njiro kata ya Engutoto nje kidogo ya Jiji la Arusha na siku hiyo hiyo alisafirishwa usiku majira ya saa 7 kwenda Babati kwa mganga wa kienyeji.

 

Alisema kwa mujibu wa taarifa ndani ya jeshi la Polisi Arusha zilisema kuwa Amina mpangaji wake alikamatwa kwani baada ya kumwiba marehemu alimpeleka kwa njiro kwa mtu aliyemtambua kwa jina la Ramadhani  kabla ya kumpeleka kwa mganga wa kienyeji aliyemtaja kwa jina la JohnMtai mkazi wa Babati Manyara.

 

Mollel alisema Mganga Mtai ndio aliyemchinja mtoto wake kwa msaada wa Ramadhani aliyemshika na baada ya hapo hadi leo mwili wa marehemu mtoto wake haijulikani ilipo.  

 

Mzee Mollel alisema watuhumiwa wote walikiri kuhusika na tukio hilo lakini waligoma kusema Maiti ilipo lakini taarifa ndani ya jeshi la polisi Arusha zinasema kuwa marehemu alipelekwa Mirerani kwenye mgodi wa Mfanyabiashara huyo ila aligoma kumtaja kwa sasa ila anamjua.

Alisema hadi sasa anaishi kwa majonzi na masikitiko makubwa kwa jinsi tukio hilo la kinyama lilivyotokea na kuliomba jeshi la polisi kumkabidhi maiti ya mwanaye ili aweze kufanya taratibu za mazishi.

‘’Nimetumia pesa nyingi sana kujua watuhumiwa wote waliohusika kufanya unyama huo na hata huyo mfanyabiashara wa Madini aliyepelekewa maiti ya mwanaye ninamjua na polisi wanamjua lakini wako kimya‘’

‘’Ninachoomba kwa Rais anisaidie kupata maiti ya mwanangu hata kama ni kidole ntashukuru kwa Mungu ili niweze kufanya utaratibu wa mazishi’’ alisema Mollel kwa machungu

 

Kamanda wa Polisi Arusha,Kamishina Msaidi wa Polisi ,justin Msejo hakuweza kupatikana kuelezea malalamiko ya Mzee Mollel kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila ya kupokelwa mara zote.

 

Hata hivyo juhudi zinaendelea kumsaka Kamanda kuelezea tukio hilo kwani limeleta simanzi na majonzi kwa wakzi wa Sanawari na viunga vyake.

Hata hivyo taarifa kutoka ndani ya jeshi la Polisi Arusha zinasema kuwa watuhumiwa wote wameshafikishwa Mahakamani  kujibu shitaka la mauaji.

 
Ends....

Post a Comment

0 Comments