WACHIMBAJI MADINI RASMI KUANZISHA BENKI YAO,WACHANGA PAPO HAPO BILIONI 2.8 ,MCHIMBAJI SUNDA AJILIPUA KWA BILIONI 1,MBUNGE MSUKUMA AJITOSA KWA RAIS SAMIA


 Na Joseph Ngilisho Arusha

Wachimbaji wa Madini nchini wamekusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuanzisha  benki yao itakayowawezesha kuwapa mitaji ya kuchimba madini kwa tija.


Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (Femata) John Bina ameyasema hayo jijini Arusha  kwenye kikao cha wachimbaji kutoka mikoa mbalimbali cha kujadili uanzishwaji wa benki hiyo ambapo wachimbaji hao walihamasika na kuchanga  papo hapo  sh,bilioni 2.885


Miongoni mwa wachimbaji waliochangia ni pamoja na Mfanyabiashara, Emmanuel Wado maarufu kwa jina la Sunda aliyetoa sh,bilioni 1 na Baraka Ezekiel Nyandu aliyechangia sh,milioni 500.

Mkutano kama huo ulifanyika kwa mara ya kwanza mkoani Mwanza ambapo wachimbaji walijichanga na kukusanya kiasi cha sh,milioni 700.78 na wataendelea kuchanga katika mikoa mingine mbalimbali nchini,ikiwa lengo ni kupata mtaji wa zaidi ya sh,bilioni 15 ili kufikia kuanzisha benki hiyo  kwa mujibu wa kanuni za benki kuu ya Tanzania BOT.


Bina alisema uanzishwaji wa benki hiyo utajibu changamoto mbalimbali za wachimbaji na wadau wote wanaonufaika na mnyororo wa thamani ya madini.

Alitaja wanufaika wa benki hiyo ni wachimbaji madini wakiwemo wamiliki wa leseni, wenye mialo, wenye migodi, miduara, wachenjuaji, wanunuzi wa magonga ya Tanzanite, wanunuzi wakubwa wa madini wa kati na wachuuzi.

"Mchakato wa uanzishwaji benki unahitaji maoni, uzoefu na utaalam ili kujiweka tayari hasa kununua hisa pindi benki hiyo ikianza," amesema Bina.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) Dkt Venance Mwasse alisema uanzishwaji wa benki hiyo ni maendeleo makubwa na umuhimu hasa kwa wachimbaji wadogo nchini kwa kuwa wengi wao wanachangamoto ya mitaji.

Dkt Mwasse alisema wazo la uanzishaji wa benki ni zuri kwani hata mataifa mengine ya nje yataiga kwenu kwani mmetengua mtego mkubwa wa kuwa na benki yenu.

"Mtaona fahari kuwa hata sisi wachimbaji wadogo tunaongeza mtaji wa nchi katika mapato kwa kuwa na benki kwani uchumi mkubwa ulioendelea ni ule uliopo katika mfumo wa benki,"

Alisema wachimbaji madini wakikopesheka wataweza na kwamba tasnia ya wachimbaji wadogo isipoendelezwa haitapiga hatua kwani wengi wao wanafanya shughuli hizo kwa sababu ya kujikimu kimaisha.

Mbunge wa Geita vijijini, Joseph Musukuma (CCM) ambaye amewawakilisha Wabunge wanaotoka kwenye maeneo yenye migodi alisema uanzishwaji wa benki hiyo ni wazo zuri litakuwa kimbilio kwa wachimbaji na atamshauri rais Samia suluhuHassan kuunga mkono mpango huo na kuongoza harambee ya kuchangia .


"Leo tumekutana wadau wa madini 102 tumechangishana na kupata sh, bilioni 2.8 si haba naimani ni mwanzo mzuri na hii benki itakuwa kubwa sana tunatarajia kufanya harambee  na tutamwomba rais Samia kuongoza harambee hiyo na hii ni salamu kwa mabenki ambayo yamekuwa na ukiritimba wa kutoa mikopo na masharti magumu"alisema 

"Tunatarajia kutoa wateja zaisi ya  laki moja kutoka kwenye mabenki hayo" 

Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, Bilionea Saniniu Laizer amesema uwepo wa benki hiyo itakuwa fursa kubwa kwa wachimbaji wadogo wengi wasio na mitaji ya kuchimba.

Naye mwenyekiti wa Taifa wa chama cha wafanyabiashara wa madini(Tamida),Sammy Mollel ,alisema TAMIDA imefarijika kwa wazo la uanzishaji wa benki ya wachimbaji ,kwani benki hiyo itakuwa faraja kwa wachimbaji na watakuwa wameondokana na urasimu uliopo kwenye mabenki kwa sasa.


"Tunajua faida kubwa kwa tasinia ya madini ,wachimbaji wataitumia kuhifadhi fedha watachukua mikopo isiyokuwa na riba chechefu na tutakuwa tumeondokana na urasimu"

Ends..


Post a Comment

0 Comments