Na Joseph Ngilisho Arusha
MAMLAKA ya afya ya mimea TPHPA Mkoani Arusha, imenunua ndege maalumu ya Uchunguzi ili kurahisisha kubaini viashiria vya visumbufu vya mazao visilete madhara kwa wakulima na hivyo kuwezesha kilimo kiwe na tija na kuongeza kipato
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa TPHPA Profesa Joseph Ndunguru,alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya afya ya mimea duniani.
Amesema kuwa mamlaka hiyo imeweka mkakati wa kuhakikisha hakuna visumbufu vya mimea ambavyo vinapunguza uzalishaji na matokeo yake ni kuwepo na upungufu wa chakula hivyo wanatumia mbinu mbalimbali kukabiliana na hali hiyo
Amesema kuwa pia mamlaka hiyo imenunua magari 7,pikipiki 19 na. ndegenyuki (Drons) na kuanzisha maabara 17 ambazo zitawekwa kwenye vituo vya mpakani kwa ajili ya kuendesha uchunguzi wa Visumbufu vya afya ya mimea mashambani
Kuhusu magugu vamizi yanayoathiri mazao na uzalishaji mashambani Profesa Ndunguru,amesema mamlaka hiyo imenunua kifaa maalumu cha Kutambua Magugu vamizi ikiwemo gugu Karoti .
Pia wamefanya utafiti wa mnyauko wa mahindi mashambani uliosababishwa na viashiria zaidi ya kimoja na wameshatoa mbegu kinzani ambazo zimesambazwa kwa wakulima na sasa ugonjwa huo wa mnyauko umepungua.
Kwa upande wake Ofisa Mtafiti Mkuu, Eliningaya Kweka alisema lengo kuu la ukaguzi wa viuatilifu mpakani vinavyoletwa nchini kwa lengo la kibiashara au misaada Ni kudhibiti visiwe na sumu na madhara kwa mazao, mimea na mavuno ya mashambani kwa kuwa nchi inajitahidi kuwa na chakula cha kutosha.
"Maabara pia itachambua viuatilifu vyote vinavyosafirishwa nje ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa viko salama kwa mazingira pia," Kweka alisisitiza
Katika ukaguzi wa hivi karibuni wa mamlaka katika mikoa 18, TPHPA ilipitia maduka 1016, huku maduka 948 kati ya hayo yalibainika kuuza viuatilifu vilivyothibitishwa ambayo ni sawa na asilimia 93.1 ya maduka yote.
"Ni asilimia 6.9 tu ya maduka hayo yalipatikana kuhifadhi bidhaa zenye madhara, nyingi zikiwa ni dawa za kuua wadudu zinazotumika nchini kuua mbu na mende".
Ends..
0 Comments