Na Joseph Ngilisho,Arusha
SERIKALI imesema Tanzania sio kichwa cha mwendawazimu katika michezo, hivyo inastahili kuwa makuu ya kudumu ya Kamati ya Baraza la Wataalamu wa Michezo Kanda ya IV Afrika lengo ni kutaka kuboresha zaidi sekta michezo katika Ukanda huo na nchi kwa ujumla.
"Sababu za kuomba kushika nafasi hiyo tunayo na tupo kwenye hatua nzuri sana ya kuendeleza michezo hapa nchini kwa sababu Tanzania ya sasa sio kichwa cha mwendawazimu tena,timu zetu zinafanya viźuri sana ,timu zikija hapa zinatakiwa zijipange,kwa jitihada za rais Samia soka letu linapanda kila kukicha"
Hayo yalisemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni,Michezo na Sanaa,Said Yakubu wakati akifungua Kikao cha kamati hiyo ambapo wajumbe wake ni Wakurugenzi wa Michezo katika Nchini 14 za Ukanda wa IV Afrika .
Yakubu alisema kuwa Tanzania imewasilisha rasmi ombi kwa kamati hiyo la kutaka Makao Makuu ya kamati hiyo yawe hapa Nchini na Tanzania ina sifa na vigezo vyote kwa kamati hiyo Makao yake kuwa Arusha Jiji lenye sifa ya Geneva ya Afrika.
Alisema moja ya sifa ya Tanzania ni pamoja na kuwa na Diplomasia ya Michezo,Tanzania inaboresha Miundombinu ya Michezo na sekta ya Michezo inakuwa katika ukanda huo hususani katika soka la wanawake kwa umri zote.
Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Kamati hiyo ya Wataalamu imeshaandaa katiba ambayo inatarajiwa kupata baraka na Mawaziri wa michezo,Utamaduni na Sanaa kutoka katika Nchi hizo 14 za Ukanda wa IV Afrika.
Alisema mbali ya hilo kamati hiyo imeboresha uendeshaji wa kamati hiyo ili iweze kwenda na wakati lengo likiwa kukuza michezo yote katika ukanda wa IV Afrika tofauti na zamani.
Yakubu alisema katika Mkutano wa Mawaziri wa Michezo ,Utamaduni na Sanaa wa Nchi 14 za ukanda wa IV wa Afrika unaotarajia kufanyika Mei 4 mwaka huu na kufunguliwa,Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi .
Alizitaja Nchi 14 wanachama ni pamoja na wenyeji Tanzania ,Kenya,Uganda,Rwanda,Ethiopia, Sudan,South Sudan ,Eritrea ,Somalia ,Djibout ,Mauritius ,Madagascar ,Comoro na Seychelleys.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Nchini,Ally Mayai alisema kuwa agenda kuu ya Mkutano wa Kamati ya wataalamu wa Michezo Ukanda wa IV Afrika ni kupitisha mapendekezo ya katiba kabla ya kubarikiwa na Mkutano Mkuu wa Baraza la Mawaziri Michezo wa Ukanda huo unaotarajiwa kufanyika kesho Jijini Arusha.
Mayai alisema kupitishwa kwa katiba hiyo itaongeza ushirikiano katika sekta ya Michezo na Mataifa mengi yameendelea kwa sababu ya ushirikiano kwa kujenga na kusimamia mpango kazi wa Maendeleo ya Ukanda huo.
Alisema baadhi ya wajumbe katika Mkutano huo wamesema kuwa Tanzania katika ukanda wa IV Afrika inaongoza kwa wananchi na wataalamu wenye kupenda michezo.
Ends ..
0 Comments