Na Joseph Ngilisho Arusha
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Kamati ya Mawakili kuchukua hatua kali za kinidhamu na kisheria dhidi ya mawakili wachache wanaoharibu heshima ya taaluma hiyo kwa kukosa uadilifu na maadili mema.
Amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Amesema kumekuwa na tuhuma kwa baadhi ya Mawakili kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu kwa maslahi yao binafsi ikiwemo kuwasaliti wateja kwa kupokea rushwa kutoka upande wa pili na kuharibu mwenendo wa kesi.
Amesisitiza kwa TLS kuhakikisha inashirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu suala la mihuri ya kielektroniki ili kuondokana na suala la vishoka na mawakili wanaotumia mihuri isiyo halali kufanya kazi za uwakili.
Aidha ameziagiza taasisi zote za serikali pamoja na taasisi binafsi kuhakikisha zinatumia mihuri ya kielektroniki ili kuondokana na kadhia hiyo.
Awali akitoa taarifa ya utendaji wa Chama Cha Mawakili Tanganyika, Rais anayemaliza muda wake wa chama hicho Profesa Edward Hoseah amesema uongozi wa TLS umeweka muhimu na kipaumbele katika kuwa na ushirikiano na serikali pamoja na wadau ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili.
Prof. Hoseah ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha Chama hicho kupata ada za leseni na mahafali ambazo zilikua hazifiki katika chama hicho kinyume na sheria.
Amesema ushirikiano wa kujenga kati ya TLS na serikali umewezesha kupatikana kwa kiwanja katika eneo la mtumba mkoani Dodoma pamoja na kupungua kwa wimbi la kukamatwa kwa mawakili hapa nchini.
0 Comments