Na Joseph Ngilisho Arusha
Waziri wa Maliasili na utalii, Mohamed Mchengerwa ameipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa msaada wa pikipiki 15 zenye thamani ya sh, milioni 40 kwa Jeshi la Polisi mkoani Arusha ,zitakazosaidia kuboresha usalama kwa watalii nchini.
Waziri Mchengerwa ametoa pongezi hizo katika hafla ya kukabidhiwa pikipiki hizo,iliyohudhuliwa pia na Mkuu wa wilaya ya Arusha, Felisian Mtehengerwa na mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo pamoja na uongozi wa jeshi hilo.
Waziri alisema sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa katika uchumi na maendeleo ya wananchi nchini kwani ndiyo inayoongoza kwa kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni,ikiwa ya pili kwa kuchangia kwenye Pato la Taifa , na ya tatu kwa kutoa ajira.
“Naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa msaada huu wa pikipiki 15 ambao Benki yetu ya CRDB imeutoa kwa kituo chetu hichi. Pikipiki hizi zitawawezesha askari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Askari watakabiliana haraka na dharula jambo litakalosaidia kuimarisha usalama kwa watalii "
Katika hatua nyingine waziri,aliagiza wizara yake na taasisi zake kusaidia kuboresha miundo mbinu ya kituo hicho cha polisi cha utalii na Diplomasia ikiwemo kujenga ukuta na kugharamia gari moja kwa ajili ya shughuli za kituo hicho.
Awali mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela alisema kuwa benki hiyo ilipokea maombi ya pikipiki 25 lakini imefanikiwa kukabidhi 15 na kusema iwapo zitatumika ilivyokusudiwa zitasaidia kuboresha doria mjini hapa.
Nsekela alisema benki hiyo imekuwa mdau mkubwa katika sekta ya utalii na imeshiriki kutengeneza mifumo rahisi ya ulipaji wa fedha ili kurahisisha shughuli za watalii na kuwaondolea usumbufu wageni wakati wa malipo.
"Najua mahitaji ni mengi ,leo tumetoa pikipiki 15 awamu nyingine tunaweza kutoa zingine na kufikisha idadi ya 25 ,tutaendelea kulisaidia jeshi la polisi na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika maendeleo ya taifa "
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Edith Swebe, alisema jeshi la polisi limekuwa mhimili mkubwa katika kusimamia usalama wa watalii ,hivyo msaada huo utaongeza doria hasa maeneo ambayo magari hayafiki.
Alisema jeshi la polisi kupitia mradi wa utalii salama litahakikisha linaimarisha ulinzi na pikipiki hizo 15 zitasaidia kuboresha doria katika sekta ya utalii.
“Tunachokifanya sasa hivi ni kusimamia mradi wa utalii salama ambao unahitaji askari kuwapo kila walipo wageni. Pikipiki hizi tunazozipokea zitasaidia kuwafikisha askari kwenye maeneo ambako magari hayawezi kufika kwa urahisi zikiwamo barabara nyembamba.
Hata hivyo, aliiomba Serikali na wadau wengine wa utalii kuliwezesha jeshi hilo kupata pikipiki nyingine 10 zitakazofanya kata zote 25 za Jiji la Arusha kuwa na pikipiki moja ya doria itakayosaidia utekelezaji wa mradi wa utalii salama.
Ends....
0 Comments