TANAPA YASAINI BILIONI 157.29 KUTEKELEZA MIRADI NANE YA NGUVU,WAZIRI MCHENGERWA ATOA ONYO KALI,WAKANDARASI WAAHIDI MAKUBWA

 


Na Joseph Ngilisho,  Arusha


 SHIRIKA la hifadhi za Taifa TANAPA, limesaini mikataba nane yenye thamani ya shilingi bilioni 157.29 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu  chini ya mradi wa kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania(REGROW).

Utiwaji wa saini umefanyika jijini Arusha baina ya shirika hilo na wakandarasi na kushuhudiwa na waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa ambaye  ameelekeza mikataba yote inayohusu fedha za wananchi  ifanyika kwa uwazi na kutoa onyo kwa watakao hujumu miradi hiyo.


Akiongea katika hafla hiyo waziri aliwataka watekelezaji wote wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii kusini (REGROW) kuondoa ukiritimba wakati wa kutekeleza mradi huu ili kukuza na kutangaza mazao mapya ya utalii katika mikoa ya kusini mwa Tanzania vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya uzembe au kuuhujumu mradi huo.


Waziri Mchengerwa aliwataka wakandarasi wote waliosaini mikataba hiyo kutumia vizuri muda waliopewa kwa kufanya kazi nzuri na kwa muda mwafaka na kwamba wasitarajie kuongezewa muda.

Mikataba iliyosainiwa imegawanyika katika makundi mawili; mikataba minne ya ujenzi wa majengo pamoja na mikataba minne ya ujenzi wa viwanja vya ndege ambayo itatekelezwa katika hifadhi nne za Ruaha, Mikumi Udzungwa na Nyerere na Msitu wa Asili wa Kilombero chini ya TFS .


Akifafanua zaidi alisema kwenye mikataba ya ujenzi wa viwanja inatarajiwa viwanja sita vya ndege kujengwa ambapo viwanja vitatu vya ndege vitajengwa hifadhi ya Ruaha , viwanja viwili hifadhi ya Mikumi na hifadhi ya Nyerere kitajengwa kiwanja kimoja cha ndege.

Aidha alisema katika hifadhi ya Udzungwa kutajengwa njia ya juu ya watalii ambayo inakadiriwa kuwa na kilomita moja ambayo inatarajiwa kuwa miongoni mwa njia ndefu zaidi Afrika Mashariki na hata kusini mwa Afrika itakapokamilika.


Mchengerwa amefafanua kuwa miundombinu mbalimbali kama vile majengo ya utalii, mageti, vituo vya habari, nyumba za watalii, hosteli vituo vya askari pamoja na maeneo ya kupumzikia yatajengwa ili kuhakikisha watalii wanafurahia wanapotembelea katika maeneo hayo.

Alisema ujenzi wa miradi hii itasaidia kufungua fursa na kukua kwa uchumi wa mikoa ya kusini na amewaomba wakazi wa mikoa ya kusini kuchangamkia fursa wakati wa utekelezaji wa miradi.



Aidha,ametoa wito kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini kuchangamkia fursa za ajira zitakazotokana na utekelezaji wa mikataba hiyo ambapo amewasisitiza watakaopata kazi hizo wakawe wazalendo na wafanye kazi kwa bidii ili kwa pamoja mradi huo uweze kuchagiza maendeleo ya ukuaji wa Sekta ya Utalii pamoja na kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

Naye katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi alielezea kusikitishwa kwake kwa jinsi ambavyo mradi umekuwa ukishindwa kutekelezwa kwa wakati bila sababu zozote za msingi ambapo hadi Machi mwaka huu mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 43 tu na kuonya kuwa hatamfumbia macho mtekelezaji yoyote wa mradi huo.


Mradi REGROW ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza Sekta ya Utalii katika Mikoa ya Kusini.

Mradi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia.


Awali kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, William Mwakilema, aliishukuru serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii kwa kuwezesha mradi huo na kuichagua Tanapa kuwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza na kunufaika katika mradi huo. 


Alisema mradi huo ukikamilika unalenga kuimarisha utoaji wa huduma za utalii  na kuongeza kipato kwa wananchi waliopo kusini mwa Tanzania .

Alisema TANAPA inakabiliwa na changamoto za ujangili ,ubovu wa miundo mbinu hasa barabara na viwanja vya ndege na changamoto hivyo mradi huo unakwenda  kutatua changamoto hizo.


Mmoja ya wakandarasi anayetekeleza mradi katika hifadhi ya mikumi kutoka kampuni Badr EAST AFRICAN ENTERPRISE LTD ,Richard Magoyo alisema waliomba tenda saba Septembe mwaka huu na wanashukuru wamepata moja ,hivyo aliahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaohitajika.

Ends....







Post a Comment

0 Comments