SHULE BINAFSI ZATAJWA USHOGA,ZATAKIWA KUFUATILIWA KWA UKARIBU

 


Na! Joseph Ngilisho,ARUSHA


Katibu Mkuu wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof, Carolyne Nombo ameielekeza ofisi ya mthibiti ubora wa elimu hapa nchini kuendelea na kufuatilia shule zote za binafsi ili kuweza kubaini shule zinazo fundisha mapenzi ya jinsia moja (ushoga).

Prof, Nombo ameyasema hayo leo alipo kuwa akifungua mkutano wa 31 wa Baraza la wafanyakazi wa elimu ,Sayansi na Teknolojia Jijini Arusha  kwa niaba ya Waziri wa elimu,Sayansi na Teknolojia Prof, Adolf Mkenda.

Alimwelekeza Mkurugenzi wa Uthibiti ubora kupiga hatua tatu mbele zaidi ili kuweza kukabiliana ipasavyo na changamoto hiyo ambayo hivi sasa inaonekana kukithiri hapa nchini hasa swala zima la unyanyasaji na ukatili wa jinsia kwa wanafunzi mashuleni.

"Nikuombe Mkurugenzi wa udhibiti ubora kuzidi kupambana na suala hili maana tunapambana kukuza elimu yetu niombe ofisi yako isilale izidi kupambana na mambo haya ya ushoga yanazidi kukithiri hasa shule zetu za binafsi zinanyooshewa vidole sana mzifatile na muweze kuzibaini ili tuweze kuzichukulia hatua kwa haraka". Alisema Prof Nombo.

"Pia tuwe wakwanza kuhabarisha umma katika vitendo hivi vya unyanyasaji na mapenzi ya jinsia moja kwa watoto wetu, ulawiti pamoja na ndoa za utotoni, Sisi kama sekta ya elimu tunakutana na mambo haya mashuleni sasa naomba tuwe wa kwanza kuyasemea ili jamii ijue na kuyapinga na mwishowe watoto wapate elimu iliyo bora na stahiki". Aliongeza Prof Nombo.

Aidha Prof, Nombo alisema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamilia kuleta mageuzi makubwa kwa wanafunzi kupata elimu bora ikiwemo kujiamini, kujiajiri na kuajirika kitaifa na kimataifa, Pia amemshukuru Rais kwa kuendelea kutia fedha za miradi mbali mbali ya elimu hapa nchini.

"Serikali kupitia wizara yetu ya elimu,sayansi na teknolojia imedhamilia kuleta mageuzi makubwa kwa wanafunzi na tupo katika hatua ya kukusanya maoni  ya wadau wa elimu ili kuwa na sera mpya ya elimu nchini"Alisema Prof Nombo.

Pia Prof Nombo, alieleza kuwa ili kuweza kukuza ubora wa elimu wizara inaendelea kutoa mafunzo ya vitendo kwa walimu wa sayansi, wakufunzi wa vyuo na wataalamu mbali mbali wa elimu kwa njia ya tehama lengo likiwa ni kuwafikia kwa wigo mpana na kwa wakati.

Prof, Nombo amebainisha kuwa hadi sasa serikali imeweza kununja vifaa visaidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum waliyopo mashuleni pamoja na vyuoni kimasomo lengo likini ni ufanikishwaji wa utoaji elemu stahiki kwa wanafunzi wa aina zote pasipo kuwa ubaguzi maana wote wanaingia katika soko la ajira.

"Rai yangu kwenu niwaombe tuendelee kushikamana katika utendaji kazi wa wizara yetu kuendelea kutoa elimu bora maana wizara yetu ndiyo tegemeo zaidi katika ustawi wa elimu hapa nchini niwaombe tufanye kazi zetu kwa nidhamu kubwa na kupambana na hali iliyopo sasa katika jamii zetu". Alisema Nombo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Arusha , Felician Mtehengerwa alisema kwa sasa elimu ya Tanzania inakuwa na Rais Samia suluhu hajakosea kuwachagua viongozi hao kuisimamia wizara hiyo maana wanafanya kazi nzuri na kuwataka wawe wakali katika usimamizi wa shule binafsi ambazo hadi sasa ndizo zinaongoza kwa janga la mapenzi ya jinsia moja.

Mtahengerwa alisema kuwa kwasasa kuna wimbi kubwa la watu mashuleni kupandikiza mizizi ya  mapenzi ya jinsia moja na kueleza kwamba zipo shule ambazo zimewekwa hadi nembo inayo ashiria mapenzi ya jinsia moja na kumekuwa na watu waokuja kwa nia ya utoaji elimu kumbe ndani yake wanania zao ovu.

"Kuna watu wanakuja kwaajili kutoa elimu wala uongozi haujui wanakuja na mambo yao ya ajabu na maovu kwa watoto wetu jambo ambalo tunaangaika nalo na sisi kama Arusha tayari tumeanza na kwa wale wote watakao bainika tutawachukulia hatua kali za kishelia". Amesema Mtehengerwa.

"Pia kuna jambo ambalo bado linaukakasi katika sekta hii ya elimu ni swala zima la ulawiti na unyanyasaji wanao ufanya walimu wetu mashuleni na pindi mtoto anapo ulizwa akisema ni mwalimu ndiyo kamfanyia utaona shule husika kumficha siri kwa kuogopa sifa mbaya ya shule na taaluma ya mwalimu pasipo kujua yeye ndiyo amevunja sheria". Ameongeza Mtehengera.

Aidha Mtahengerwa alikitaka chama cha wafanyakazi wa sekta ya elimu kufanya kazi yao ya kuwatetea watu wao na kuacha tabia ya kuwa watumwa wa kutumika kisiasa na kuacha majukumu yao ya msingi.

Katika hatua nyingine Mtahengerwa ameiomba wizara ya elimu kuendeleza zaidi utoaji wa elimu bora itakayoleta ushindani  kuzipita nchi za Afrika ya Mashariki ili kuliweka taifa kati soko lisilo shuka kimataifa kwa kuzalisha wataalam bora na wenyesifa za kimataifa.

" Kwasasa elimu yetu ni bora zaidi katika ukanda huu ya nchi za Afrika Mashariki niwapongeze kwa jinsi mnavyo pambana na mitaala ili iweze kuendana na soko la ajira la kimataifa niwaombe muongeze zaidi tuweze kuzishinda nchi zetu tunazo pakana nazo ambao wao wanaongeza kwa lugha ya kingereza kitu ambacho kinatufanya Tanzania tusionekane kama sisi ni bora kuliko wao katika utendaji kazi". Alisema Mtehengerwa.

Ends....

Post a Comment

0 Comments