Dodoma.
Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo amehoji kwanini Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) haiwakamati watu waliohusika na ubadhirifu wa fedha za waendesha bodaboda jijini Arusha.
Gambo ameyasema hayo leo Alhamis Aprili 20, 2023 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mwaka 2023/2024.
Akichangia hoja hiyo, Gambo amesema kuna masuala yako wazi lakini mchakato wake unakuwa mrefu sana.
Amesema mwaka 2017/2018 kuna mchakato ulianzishwa Arusha bodaboda walichangisha fedha kiasi cha Sh400 milioni ambazo baadaye anadai ziliibiwa na baadhi ya watu.
Ametaja nyakati tofauti fedha zilizochukuliwa na watu ambao wanafahamika ikiwemo Juni 18 mwaka 2021, Sh39.5 milioni na Julai 8,2021 Sh 43.5 milioni, Sh 43.8 zilichotwa Agosti 31,2021 na Novemba 25, 2020 walichukua Sh15 milioni.
“Kuna orodha ndefu hoja ni kwamba fedha za bodaboda zimeibiwa na walioiba wanajulikana wameenda benki wametoa vitambushio vya Nida (vya Taifa) na wamechukua kwa majina yao lakini hadi leo halijapelekwa mahakamani na wahusika hawajakamatwa,”amesema.
Amesema hilo linatoa fursa ya baadhi ya watu kuwachafua watu ambao hawahusiki kwenye jambo hilo.
Gambo amehoji watu walioiba wanajulikana kigugumizi cha kuwakamata na kuwapeleka mahakani kinatokana na nini na kwamba zingepatikana zingewasaidia kuendelea kukopeshana.
Hata hivyo Gambo bado anahoja ya kujibu kwa wakazi wa jiji la Arusha ambao wengi wao wanaamini mbunge huyo ndiye aliyechota fedha hizo ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaomuunganisha na wizi huo.
0 Comments